Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makata alia na Cedric Kaze

Muktasari:

  • Polisi Tanzania inakutana na Kagera Sugar Oktoba 17, 2026 ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao 1-2 dhidi ya Mashujaa Oktoba 8, 2026 matokeo yaliyowafanya kusaka namna ya kurekebisha makosa kabla ya mchezo unaofuata.

KOCHA wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, akiamini kina uwezo wa kurejea kwenye matokeo mazuri baada ya kupoteza dhidi ya Mashujaa.

Polisi Tanzania inakutana na Kagera Sugar Oktoba 17, 2026 ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao 1-2 dhidi ya Mashujaa Oktoba 8, 2026 matokeo yaliyowafanya kusaka namna ya kurekebisha makosa kabla ya mchezo unaofuata.

Hadi sasa, Polisi imecheza mechi saba za ligi, ikishinda tatu, sare moja na kupoteza tatu. Imefunga mabao 10 na kufungwa tisa, ikiwa na pointi 10 na tofauti ya bao moja.

Makata alisema mchezo huo hautakuwa mwepesi kutokana na ujio wa kocha mpya wa Kagera Sugar, Cedric Kaze, lakini ana imani na wachezaji wake katika kupambana kutafuta matokeo yatakayowarejesha kwenye njia ya ushindi.

“Tunajua mchezo hautakuwa rahisi kwa sababu Kagera Sugar ina kocha mpya, lakini tunaamini katika uwezo wa wachezaji wetu. Tumepoteza mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa na sasa tunataka kurekebisha makosa yetu ili kupata matokeo mazuri,” amesema Makata.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Makata amesema wamejikita kuboresha utengenezaji wa nafasi za kufunga pamoja na uimara wa safu ya ulinzi, akieleza kuwa maeneo hayo ni muhimu katika kuhakikisha timu inapata matokeo inayoyahitaji.

“Katika mazoezi tumefanya kazi kubwa kuboresha namna tunavyotengeneza nafasi za kufunga na pia eneo la ulinzi. Tunataka wachezaji wawe makini katika maeneo hayo ili tuweze kutumia nafasi tunazopata na kuzuia wapinzani wetu wasifunge,” alisema Makata.

Kocha kutoka Burundi, Kaze, ana rekodi ya kutwaa Kombe la Mapinduzi 2021, akiwa na Yanga na baadaye kuhudumu kama kocha msaidizi chini ya Nasreddine Nabi ambapo walishinda mataji ya Ligi Kuu, Kombe la FA, na kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho la CAF (2022-2023).

Baada ya hapo, Kaze alielekea nchini Afrika Kusini ambako alihudumu kama kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs na kufanikiwa kubeba Nedbank Cup 2025, kisha akapitia Sekhukhune United kwa muda mfupi kabla ya kurejea rasmi nchini Tanzania mnamo Septemba 2026 kuwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar.