Mafie atuliza presha Pamba Jiji
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, Mafie aliifungia Pamba bao hilo ambalo ni la kusawazisha dakika ya 24, baada ya winga nyota, Benno Ngassa kuitanguliza kuifungia Dodoma Jiji mapema dakika ya 17.
MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, Deogratius Mafie amesema kipindi hiki cha kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kimekuwa kizuri kwao kwa ajili ya kujadili mipango mbalimbali, hasa baada ya kuanza vibaya msimu wa 2026-2027.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mafie amesema mechi sita za Ligi Kuu Bara zimekuwa ni ngumu kwao kutokana na ushindani mkubwa walioupata, lakini mapumziko ya takribani wiki tatu yametoa nafasi kwa wachezaji kujipanga upya ili kuja na nguvu mpya.
"Tumekuwa na mwanzo mbaya sana lakini bado tuna muda wa kurekebisha changamoto mbalimbali zilizojitokeza, kipindi hiki cha mapumziko tumekitumia vizuri na benchi la ufundi, ili Ligi Kuu Bara itakaporejea tena tuwe tayari," amesema Mafie.
Nyota huyo aliyejiunga na Pamba Jiji, Agosti 3, 2026, akitokea Kagera Sugar, amesema shida kubwa ya timu hiyo ni kukosa muunganiko mzuri katika safu ya kujilinda na ya ushambuliaji, jambo ambalo benchi la ufundi limeendelea kulifanyia kazi.
"Nafasi tuliyopo hatustahili kutokana na ubora wa wachezaji tulionao, hii ni changamoto kwetu ya kujipanga ili kurejea tukiwa imara zaidi, wengi wetu ni wapya hivyo, inahitaji muda zaidi kuzoeana aina ya uchezaji wa kila mmoja," amesema.
Katika mechi sita timu hiyo ilizocheza za Ligi Kuu Bara, haijashinda na imetoka sare moja na kupoteza tano, ikiwa mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi yake moja, huku kikosi hicho kikifunga jumla ya mabao manne tu na kuruhusu 13.
Tangu ajiunge na Pamba, nyota huyo aliyeichezea pia Biashara United, ameifungia bao moja la Ligi Kuu wakati wa sare ya 1-1, dhidi ya Dodoma Jiji, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini, Mwanza, Agosti 14, 2026.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, Mafie aliifungia Pamba bao hilo ambalo ni la kusawazisha dakika ya 24, baada ya winga nyota, Benno Ngassa kuitanguliza kuifungia Dodoma Jiji mapema dakika ya 17.