Maajabu mabao ya Jabir
Muktasari:
- Mabao hayo saba yaliyofungwa na mshambuliaji huyo aliyetamba na timu za Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, yamemfanya kuongoza katika orodha ya ufungaji bora, akimzidi moja nyota wa Yanga, Peter Shalulile mwenye sita.
MSHAMBULIAJI wa Polisi Tanzania, Anuary Jabir, ameendelea kufanya vizuri na kikosi hicho baada ya kukifungia mabao saba ya Ligi Kuu Bara tangu ajiunge nacho msimu huu wa 2026-2027, akitokea Dodoma Jiji.
Mabao hayo saba yaliyofungwa na mshambuliaji huyo aliyetamba na timu za Kagera Sugar na Mtibwa Sugar, yamemfanya kuongoza katika orodha ya ufungaji bora, akimzidi moja nyota wa Yanga, Peter Shalulile mwenye sita.
Katika mabao saba yaliyofungwa na mshambuliaji huyo, yana maajabu mawili tofauti, ambapo kati ya hayo manne ameyafunga kwa penalti ikiwa ni mchezaji anayeongoza, huku matatu yaliyobakia akiyafunga kwa kichwa akiwa ndiye anayeongoza pia.
Polisi Tanzania inaongoza kwa kupiga penalti msimu huu katika Ligi Kuu Bara, ikiwa na nne, ambazo zote mshambuliaji huyo amefunga, huku mabao matatu yaliyobaki akiyafunga kwa kichwa, akiwa ndiye anayeongoza pia kufunga kwa staili hiyo.
Katika timu zilizopiga penalti nyingi, ni Azam FC iliyopiga pia nne, imefunga tatu na kukosa moja, huku Namungo nayo katika nne, imekosa mbili, imefunga mbili.
Mshambuliaji huyo amekuwa tegemeo katika kikosi cha Polisi Tanzania kinachofundishwa na Kocha Mkuu, Mbwana Makata, ambapo amechangia mabao manane kati ya 13, baada ya kufunga saba na kuasisti moja.
Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya sita na pointi 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, mechi 11 ilizocheza imeshinda nne, sare tatu na kupoteza nne, imefunga mabao 13 zaidi ya nusu akifunga Jabir, huku ikiruhusu 12.