M’mombwa aanza kazi Zabbar, licha ya utata Floriana
Muktasari:
- Hadi sasa Zabbar imecheza mechi mbili za ligi na kiungo huyo akiwa kikosi cha kwanza alianza kwenye mechi dhidi ya Valletta chama lake likipoteza kwa mabao 4-2 mechi iliyopigwa Agosti 16, alicheza dakika 90 tena dhidi ya Birzebbuga, Zabbar ikiondoka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
KIUNGO wa Taifa Stars, Charles M’Mombwa ameanza msimu mpya akiwa na kikosi cha Zabbar huku sakata lake na timu yake ya zamani Floriana likiwa haijawekwa wazi.
Hadi sasa Zabbar imecheza mechi mbili za ligi na kiungo huyo akiwa kikosi cha kwanza alianza kwenye mechi dhidi ya Valletta chama lake likipoteza kwa mabao 4-2 mechi iliyopigwa Agosti 16, alicheza dakika 90 tena dhidi ya Birzebbuga, Zabbar ikiondoka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani.
M’Mombwa alitangazwa na Żabbar mwezi Juni atakuwa sehemu ya usajili wao kwa msimu mpya, baada ya uliopita kuitumikia Floriana na kusaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Malta.
Hata hivyo, siku chache baada ya Żabbar kumtambulisha, Floriana ilitoa taarifa ikidai M’Mombwa bado alikuwa na mkataba halali wa klabu hiyo.
Floriana ilieleza kiungo huyo alikubali kuongeza mkataba mapema mwaka huu na nyongeza hiyo ilisajiliwa na kuthibitishwa na Shirikisho la Soka Malta (MFA) Februari 2026. Klabu hiyo ikasema hatua ya M’Mombwa kuondoka ilikuwa ukiukwaji wa majukumu yake ya kimkataba.
Hata hivyo, bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kutoka Floriana au MFA inayoeleza mgogoro huo umemalizika kwa makubaliano kati ya pande zote.
M’Mombwa, mwenye uzoefu wa kucheza soka Australia na Malta, alicheza mechi 32 na kufunga mabao matatu katika msimu wake wa kwanza Floriana, akichangia timu hiyo kutwaa ubingwa.