Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KVZ yatangaza ujio mpya ikiwakabili Walibya CAF

Muktasari:

  • KVZ itakuwa mwenyeji wa Asswehly kesho Jumapili saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ikiwa na kazi ya kugeuza matokeo ya mchezo wa kwanza ambao ilipoteza kwa bao 1-0 nchini Libya.

KOCHA Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali, amesema wamebadili mbinu kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asswehly ya Libya, wakitamba sasa watashambulia ili kusaka ushindi wa mabao 2-0.

KVZ itakuwa mwenyeji wa Asswehly kesho Jumapili saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ikiwa na kazi ya kugeuza matokeo ya mchezo wa kwanza ambao ilipoteza kwa bao 1-0 nchini Libya.

Hababuu amesema katika mchezo wa kwanza walitumia mfumo wa kujilinda zaidi kwa lengo la kuhakikisha hawapotezi kwa tofauti kubwa ya mabao, jambo ambalo kwa kiasi fulani walifanikiwa.

“Tulikwenda na mpango wa kujilinda kwa sababu tulijua tunacheza ugenini. Tulitaka kama tutapoteza, basi isipite kwa mabao mengi. Tumepoteza 1-0 na hilo linatupa nafasi ya kurekebisha makosa yetu nyumbani,” amesema Hababuu.

Amesema safari hii wamejipanga kwa mpango tofauti, wakilenga kuutumia uwanja wa nyumbani kutafuta ushindi utakaowapeleka hatua inayofuata.

“Kwa sasa tunakwenda kushambulia. Lengo letu ni kushinda 2-0 kwa sababu tumeangalia makosa tuliyofanya kwenye mchezo wa kwanza na tumeyafanyia kazi. Wachezaji wapo tayari na tunataka kutumia vizuri nafasi tuliyonayo nyumbani,” amesema.

Hababuu ameeleza kuwa, mechi za kimataifa ambazo KVZ imecheza zimekuwa sehemu ya kujifunza na kufanya tathmini ya timu, akisema kila mchezo umewapa kitu kipya cha kujiandaa nacho.

“Mechi hizi za kimataifa tunazitumia pia kujitathmini. Kila mchezo tunapata kitu kipya, tunaona wapi tumekosea na tunarekebisha. Hilo ndilo tunalolifanya kuelekea mchezo huu,” amesema.

Kocha huyo amesema kikosi chake kitawakosa wachezaji wawili, Abdallah Idd Mtumwa ‘Pina’ na Samir Caragher ambao ni majeruhi.

Naye nahodha wa KVZ, Bashir Muslim Darwesh 'Iker', amesema wachezaji wamejipanga kupambana kwa nguvu zote ili kutimiza malengo ya timu hiyo.

“Tumejipanga kupambana. Kwenye mechi iliyopita tumefungwa kutokana na makosa yetu wenyewe, lakini tumejifunza na tumeyarekebisha. Hatutaruhusu makosa yale yajirudie kwenye mchezo huu,” amesema Iker.

Amesema wachezaji wanaelewa ukubwa wa mchezo huo na wanatambua kuwa wanahitaji ushindi mbele ya mashabiki wao ili kuendelea na safari ya kimataifa.

Kwa upande wake, Katibu wa Kamati ya Habari na Masoko wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa nguvu KVZ.

Kabwanga amesema mchezo huo hautakuwa na kiingilio, hivyo ametoa wito kwa vijana na mashabiki wa soka Zanzibar kutumia nafasi hiyo kwenda kuishangilia timu yao.

“Tunawaomba vijana na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi uwanjani. Mchezo huu hauna kiingilio, hivyo hakuna sababu ya kubaki nyumbani. Tuiunge mkono KVZ ili wachezaji wetu wapate nguvu ya ziada kutoka kwa mashabiki,” amesema Kabwanga.

Wakati huo huo, Mkuu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar, Luteni Kanali Said Shamhuna, amenunua tiketi 15,000 kwa ajili ya mchezo huo, hali inayofanya mashabiki kuingia bure kwani Uwanja wa New Amaan Complex una uwezo wa kuingiza idadi hiyo.

Hatua hiyo imeongeza hamasa kuelekea mchezo huo ambao KVZ inahitaji ushindi wa angalau mabao 2-0 ili kufuzu hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.