Kocha Black Sailors lawama zote kwa wachezaji
Muktasari:
- Black Sailors ilikubali kipigo hicho katika mechi iliyopigwa Septemba 3, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, kisiwani Unguja na Wembe ilitumia vizuri nafasi ilizozipata na kuondoka na ushindi huo.
KOCHA wa Black Sailors, Mohammed Ali Tedy amesema moja ya sababu za timu hiyo kufungwa mabao 2-0 na Wembe katika Ligi Kuu Zanzibar, ni kukosa utulivu.
Black Sailors ilikubali kipigo hicho katika mechi iliyopigwa Septemba 3, 2026 kwenye Uwanja wa Mao B, kisiwani Unguja na Wembe ilitumia vizuri nafasi ilizozipata na kuondoka na ushindi huo.
Kocha Tedy amesema wachezaji walishindwa kucheza kwa utulivu katika vipindi muhimu vya mechi, jambo lililowafanya wapoteze uelekeo na kuruhusu wapinzani wao kutumia makosa hayo.
"Licha ya maandalizi yaliyofanywa kabla ya mechi, timu haikuonyesha kiwango nilichokitarajia hususan kipindi cha kwanza ikiwemo namna ya kusimamia mechi na kufanya maamuzi sahihi wakati wa kushambulia na kujilinda," amesema.
Amesema kipigo hicho ni somo kwa kikosi chake na wanahitaji kurekebisha upungufu uliojitokeza ili kurejea katika hali nzuri kwenye mechi zinazofuata za ligi.
Tedy aliwataka wachezaji kuongeza umakini na nidhamu ya mchezo huku akisisitiza kutumia vizuri nafasi zinazopatikana pamoja na kudumisha utulivu wakati timu inapokuwa chini ya presha.
Black Sailors iliyopanda daraja msimu huu, katika mechi mbili za Ligi Kuu Zanzibar ilizocheza, imepata pointi moja, ikishika nafasi ya 12 kwenye msimamo.