Kiungo Yanga aibuka kwenye ndondo
Muktasari:
- Abushiri, aliyesajiliwa na Yanga akitokea Fountain Gate FC imeonekana alisahau taratibu za timu hiyo kubwa kuwa ukishasajiliwa na Wanajangwani hao ni marufuku kucheza mashindano ya Ndondo.
SAA chache baada ya kiungo mpya wa Yanga, Juma Issa Abushiri, kutambulisha juzi aliibukia kwenye mchezo wa ndondo kwenye mashindano ya Imbeju Ndondo Cup na timu yake ya Mzimuni FC kuchapwa bao 1-0 na Madenge FC katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Abushiri, aliyesajiliwa na Yanga akitokea Fountain Gate FC imeonekana alisahau taratibu za timu hiyo kubwa kuwa ukishasajiliwa na Wanajangwani hao ni marufuku kucheza mashindano ya Ndondo.
Awali, Abushiri alipangwa katika kikosi cha kwanza, hata hivyo, alikumbana na pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Yanga waliokuwa uwanjani hapo kuwa wachezaji wao hawaruhusiwi kucheza Michuano hiyo na benchi la ufundi la timu ya Mzimuni kulazimika kumuondoa katika orodha ya wachezaji waliopangwa kuanza na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Ramadhan.
Hata hivyo, baada ya kufungwa bao na Madenge mchezaji huyo ambaye ni mmoja kati ya viungo mahiri alionekana kuwabembeleza baadhi ya viongozi hao ili acheze mcheza huo, haiafahamiki kama baadaye alikubaliwa au alikataliwa, lakini Mwanaspoti lilimuona akiingia uwanjani kujaribu kuinusuru timu yake, lakini mambo yakawa magumu baada ya kulala kwa bao 1-0.
Hata hivyo uwanjani hapo kiungo huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia macho ya mashabiki waliojitokeza kushuhudia ufunguzi wa msimu wa 13 wa mashindano hayo.
Mbali na kushuhudia mwanzo wa changamoto kwa Abushiri, mchezo huo uliweka wazi ubora wa vipaji vinavyoshiriki mashindano hayo, jambo lililomfanya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, TullyEsther Mwambapa, kutangaza mpango wa kuanzisha Imbeju Football Academy kwa ajili ya kuendeleza wachezaji watakaobainika kuwa na uwezo mkubwa.
Kiungo huyo aliitumikia Fountain Gate msimu uliopita na kuonyesha kiwango bora kwenye michezo mikubwa ya timu hiyo dhidi ya Simba, Yanga, Singida na Azam FC na alikuwa sehemu kubwa ya kuisaidia timu hiyo kuepuka kushuka daraja.