Prime
Kiungo Stars mlangoni Simba
SIMBA imetupa jicho lake mapema pale Coastal Union na taarifa zinadai kwamba imeshamalizana na kiungo mshambuliaji, Bakari Selemani Msimu.
Kiungo huyo aliyejumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kwa ajili ya mechi za kirafiki dhidi ya Uganda na Rwanda zinazotarajiwa kuchezwa hivi karibuni, ndiye nyota pekee kutoka Coastal Union aliyeitwa na Kocha Miguel Gamondi.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinabainisha kwamba, viongozi wa klabu hiyo wamekubaliana na Msimu kumpa mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao.
“Simba imevutiwa na uwezo wa Msimu ambaye amekuwa akifanya vizuri ndani ya Coastal Union. Tayari mazungumzo ya yamefanyika akipewa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza mmoja.
“Zoezi hilo lilifanyika kwa haraka mara tu baada ya mchezo ulipomalizika pale Mkwakwani siku ambayo Simba ilishinda 2-1 dhidi ya Coastal Union,” kilisema chanzo hicho.
Siku hiyo katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Mei 21, 2026, Msimu alitoa asisti ya bao lililofungwa na Maabad Maulid mapema tu dakika ya nane, kabla ya Libase Gueye hajaisawazishia Simba dakika ya 36 na Anicet Oura kuweka la ushindi dakika ya 43.
Msimu amekuwa na nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha Coastal Union kinachonolewa na Fikiri Elias, amekuwa akitumika zaidi akitokea kushoto, huku winga nyingine akicheza Shiza Kichuya.
Kiungo huyo amefunga mabao matatu na asisti mbili, akicheza mechi zote.
Simba inamuhitaji Msimu kama mchezaji wa kumtumia kipindi kirefu kwani kiungo huyo hivi sasa ndio kwanza ana umri wa miaka 19, mbali na kuitumikia Taifa Stars, pia ni mchezaji wa kikosi cha timu ya taifa chini ya miaka 20.
Meneja wa Coastal Union, Abdulrahman Ubinde, alisema Msimu bado ni mchezaji wao wa timu ya vijana, lakini amepata nafasi ya kupandishwa kikosi cha wakubwa kutokana na uwezo wake.
Ubinde alisema, kwa Msimu haitakuwa mara ya kwanza kwao kuuza mchezaji kwa timu kubwa za Dar es Salaam kwani walishafanya hivyo kwa Abdi Banda (Simba), Juma Mahadhi (Yanga), Abdul Suleiman ‘Sopu’ (Azam), Victor Akpan (Simba) na Semfuko Charles (Simba).
“Msimu tumemkuza wenyewe, tupo naye kwa muda mrefu. Kweli watu wameanza kumfuatilia muda mrefu ingawa bado naweza kusema ni mchezaji wetu,” alisema Ubinde.