Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kisa Morrison, Nabi awaka

KOCHA Mkuu wa Yanga ameshtushwa sana kusikia kwamba winga wake kutoka Ghana, Bernard Morrison ‘BM33’ atakosa mechi tatu za Ligi Kuu Bara na kuwaka akiwa Ulaya alikoenda kwa dharura wakati ligi ikiwa imesimama kupisha mechi za kimataifa kwa kalenda ya FIFA.

Kocha huyo, Nasreddine Nabi alizipata salamu hizo za kifungo cha Morrison kutokana na kosa alilolifanya kwenye mechi ya ligi kati kikosi hicho na Azam na kumalizika kwa sare ya 2-2 na kugeuka mbogo juu ya hukumu hiyo iliyotolewa na Kamati ya Kusimamia na Kuendesha Ligi ya Bodi ya Ligi (TPLB) akisema anaona ni kama Yanga inaandamwa lakini akaanza mikakati mipya.

Morrison amesimamishwa mechi tatu na faini ya Sh1Milioni baada ya kukutwa na hatia ya kumkanyaga kwa makusudi beki wa Azam, Lusajo Mwaikenda akiwa chini katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Septemba 6.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Ubelgiji alipo, Nabi alisema adhabu hiyo ilimshtua kwani alipata taarifa hizo akiwa mezani na familia yake na kuharibu furaha yake yote.

Nabi alisema wakati huu Yanga ikielekea katika ratiba ngumu ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Bara, timu yake ilihitaji wachezaji wote muhimu na inatakiwa kuwa sawa jambo sasa limeanza kubomolewa kwa hukumu za aina hiyo.

“Nilipata hizo taarifa bahati mbaya zilinikuta nikiwa mezani na familia, ziliniumiza sana huu ni wakati ambao kwa mechi zilizo mbele yetu kocha yoyote angependa kuwa na wachezaji wake wote. Kuna kitu ambacho huwa kinanishtua sana naona kama timu yangu inaandamwa sana, wachezaji wangu wanaumizwa sana lakini kwa kiasi kikubwa huwa sioni sana maamuzi kama haya yakifanyika, nimeamua kuwaachia viongozi hili nitaendelea na majukumu yangu uwanjani,” alisema Nabi.

Kocha huyo aliyeongoza Yanga kucheza mechi 41 mfululizo za Ligi Kuu Bara tangu Aprili 25, 2021 bila kupoteza alisema hata hivyo Nabi alisema tayari ameshaanza mikakati mipya ambapo Morrison na menzake kama Tuisila Kisinda watakuwa na maandalizi maalum kwa kutafutiwa mechi mbili za kirafiki kuwapa ufiti wa mechi.

“Hapa sasa tutalazimika kutafuta mechi mbili au zaidi, Morrison hatacheza mechi za ndani tatu maana yake tutatakiwa kuwa na mechi za kirafiki kwa ajili yake ili kabla ya kukutana na Al Hilal awe tayari.

“Kuna Tuisila naye hajacheza muda mrefu, tutalazimika pia wakati huu kabla ya ligi kuendelea apate mechi za kirafiki ambazo pia zitawasaidia na hata wachezaji wengine, ukija kuongeza na mechi za ligi zitakuwa zimesaidia sana kumweka tayari.

“Kuna mechi za ligi tutawatumia Tuisila, Moloko, Nkane (Denis), Ambundo (Dickson) nafikiri bado tutakuwa salama ingawa suala la kuwa na wachezaji wako wote lilikuwa bora zaidi.

“Napata ripoti yake kila baada ya mazoezi yake kuna mpango maalum wa mazoezi unafanyika unazidi kumweka tayari kwasasa tofauti na alivyofika, unajua ni muda hakucheza tangu ligi ya Morocco imalizike.”


Mastaa wote kikaoni

Katika kupambana na suala la nidhamu ambayo inachangia kusimamishwa kwa wachezaji, Nabi amepanga kuitisha kikao maalum na nyota wa kikosi hicho mara baada ya kurejea ili kuwataka wawe makini na maamuzi yao uwanjani ili kuepusha kuigharimu timu.

“Nitakaa na wachezaji wote nikirejea, ni lazima tuzungumze kama familia moja, kuna wakati ukiona jirani yako anawaumiza sana watoto wako, ni vyema ukakaa chini na watoto wako na kuzungumza nao, kitu bora hapa ni sisi wenyewe kujiweka salama kwanza, licha ya kwamba na wao wanaumizwa sana, hatuna namna zaidi ya kuwa wapole na kutofanya vitu vitakavyotuumiza zaidi,” alisema Nabi.