Kimoto aifungia kazi Maniema
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti Kimoto alisema uamuzi wa kufanya mazoezi katika muda huo umetokana na tathmini ya hali ya hewa ya DR Congo, ambayo kwa sasa ina joto kali linalofanana na la Dar es Salaam, hivyo anataka wachezaji wake wazoe mazingira hayo mapema kabla ya kuingia kwenye mtihani wa kwanza wa kundi hilo.
KOCHA wa Singida Black Stars, Papy Kimoto, ameanza kuweka mikakati ya kuhakikisha kikosi chake kinakuwa tayari kukabiliana na AS Maniema Union ya DR Congo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, akipanga kutumia siku tano kufanya mazoezi ya mchana Dar es Salaam kabla ya safari ya kwenda Congo Novemba 27.
Akizungumza na Mwanaspoti Kimoto alisema uamuzi wa kufanya mazoezi katika muda huo umetokana na tathmini ya hali ya hewa ya DR Congo, ambayo kwa sasa ina joto kali linalofanana na la Dar es Salaam, hivyo anataka wachezaji wake wazoe mazingira hayo mapema kabla ya kuingia kwenye mtihani wa kwanza wa kundi hilo.
Kocha huyo alikiri kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi, lakini kwake unaongeza hisia kutokana na kwamba aliwahi kuifundisha Maniema, timu ambayo anaifahamu vizuri na inayokwenda kukutana naye katika mazingira ya mashindano ya kimataifa.
“Hapa na Congo hali ya hewa ni ya jua, ni sawa. Tumefanya baadhi ya tathmini msimu huu ni mgumu kwenye michuano ya kimataifa na nimeifundisha Maniema, lakini pia ni furaha kwangu kukutana na timu ambayo niliwahi kuifundisha kabla na msimu uliopita ilifika robo fainali.”
Kocha huyo alianza kuifundisha Maniema Januari 2022 na katika kipindi chake cha takribani miaka minne aliweza kuijenga kuwa miongoni mwa timu zinazoshindana katika soka la DR Congo.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuifikisha Maniema kwa mara ya kwanza katika historia yake hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25. Katika hatua hiyo ilikutana na vigogo Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Raja Casablanca na AS FAR za Morocco, ingawa ilimaliza mkiani mwa kundi ikiwa na pointi tatu.
Baada ya uzoefu huo msimu jana aliiongoza Maniema kucheza robo fainali ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza. Timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili katika kundi B ikiwa na pointi 12, nyuma ya Wydad Casablanca iliyokusanya pointi 15.
Kimoto alikiri mwanzo wa msimu haukuwa mzuri kutokana na maandalizi ya awali (Pre Season) na usajili kutokuwa mzuri, hali iliyochangia timu kupata matokeo yasiyoridhisha. Alisema wameanza kurekebisha eneo la utimamu wa mwili na sasa wanahitaji kujenga uimara katika maeneo mengine ya kikosi.
“Tunapaswa kutengeneza timu vizuri kwa sababu mwanzoni mwa msimu tulifanya makosa mengi. Pre-season yetu haikuwa nzuri, usajili haukuwa mzuri, ndiyo maana tumekuwa na matokeo ya kupanda na kushuka. Tumerekebisha kwenye fiziki na tutapambana kurekebisha maeneo mengine,” amesema Kimoto.
Alieleza kuwa changamoto nyingine aliyokutana nayo ni kutowafahamu vizuri wachezaji wake mwanzoni, jambo lililomlazimu kufanya mabadiliko ya kikosi mara kwa mara huku akitumia mazoezi kutathmini uwezo wa kila mchezaji na nafasi anayoweza kuitumikia vizuri.