Kama utani Kitenge atakipiga Yanga SC
Muktasari:
- Kocha huyo wa Yanga, ameoneshwa kukunwa na soka la Kitenge na kutamani atua kikosi na haikushangaza mara baada ya pambano hilo alimsaka Uwanja wa Taifa na kufanya naye mazungumzo mafupi na ya siri akimchombeza atue Yanga.
NI kweli Ibrahim Ajibu aliwakosha mashabiki wa Yanga kwa soka alililopiga juzi wakati Yanga ikishinda mabao 4-3 dhidi ya Stand United, lakini kile alichofanya Alex Kitenge kimemfanya Kocha Mwinyo Zahera kushindwa kujizuia.
Kocha huyo wa Yanga, ameoneshwa kukunwa na soka la Kitenge na kutamani atua kikosi na haikushangaza mara baada ya pambano hilo alimsaka Uwanja wa Taifa na kufanya naye mazungumzo mafupi na ya siri akimchombeza atue Yanga.
Kitenge alifunga mabao yote ya Stand wakati timu yake ikifa kibingwa kwenye Uwanja wa Taifa, jambo lililomfanya Zahera amsake na kuzungumza naye huku akibadilishana namba zao za simu kwa mawasiliano zaidi.
Jambo hilo lilifanya Mwanaspoti kuzungumza na Zahera kutaka kujua alichozungumza na straika huyo Mrundi naye akafafanua kuwa, alikunwa na soka la Kitenge, aliyemtaja kama mshambuliaji mzuri, ana uwezo mkubwa wa kuliona goli na kufunga.
“Mastraika wa aina hii ya Kitenge ndio natamani kuwa nao katika timu yangu, nilikuwa namfahamisha ana uwezo wa kucheza Yanga kama atakuwa na kasi hiyo ya kufunga mpaka wakati wa dirisha dogo nitawapatia jina hilo Kamati ya Usajili.
“Nitaendelea kumfuatilia mechi za Stand msimu huu ili kuona uwezo wake zaidi wa kufunga kama alivyofanya katika mechi yetu na msaada wake ndani ya timu na nimefungua mawasiliano naye, ikibidi aje kucheza Yanga.”
Kocha Zahera alisema kwa kuwa timu yake itasajili straika dirisha dogo ili kuongeza nguvu na aina ya anaowataka ni kama kina Kitenge wenye jicho la kufunga.
“Angalia hata bao lake la kwanza alivyofunga akiwa na beki na alilazimisha kupiga shuti, lakini hata mabao mengine mawili yote ni umakini wa hali ya juu alionao katika kufunga,” alisema.
Kitenge aliyewahi kufunga hat-trick alipokuwa akiichezea AFC Leopard walipocheza na Gor Mahia, alisema kufunga mabao sio kitu kigeni na kukiri kuhitajiwa na Zahera Jangwani.
“Maneno aliyoniambia kocha wa Yanga Zahera ni kwamba atanifuatilia zaidi na kama nitafanya vizuri zaidi kwa kufunga magoli na kutoa msaada ndani ya timu anawezaa kunisajili wakati wa dirisha dogo. “Maneno hayo yataniongeza morali ya kujituma zaidi ingawa nilikuja hapa nchini nikiwa na malengo hayo na kutamani kuwa mfungaji bora pia,” alisema Kitenge.