Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kagere aliamsha mapema Simba

Muktasari:

  • Kagere yupo nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu nyuma ya Salum Aiyee kinara mwenye mabao 13 na Heritier Makambo aliyefunga 12.

KIKOSI cha Simba kilichokuwa kimepiga kambi ya muda mfupi mjini Morogoro, mchana wa jana kimetua salama mkoani Iringa, huku straika wake matata, Meddie Kagere akiliamsha mapema akiwatahadharisha washambuliaji wengine wa Ligi Kuu, kuwa hapoi mpaka kieleweke.

Simba inajiandaa na mchezo wao wa kiporo dhidi ya Lipuli utakaochezwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa ambapo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Aussems ameweka hadharani kuwa ataendelea kuisuka kikamilifu safu yake ya ushambuliaji ili kuweza kufunga mabao mengi zaidi.

Lakini wakati Aussems akichimba mkwara huo, kinara wa mabao wa Simba, Meddie Kagere ‘MK14’ amewatahadharisha mapema mastraika wa timu nyingine akiwamo nyota wa Yanga, Heritier Makambo, kuwa kasi yake haipoi na wala hataboa mashabiki wa klabu yake.

Kagere alisema moja ya malengo yake ni kuhakikisha Simba inapata ushindi katika kila mechi ili liwezekana kwani ndivyo ilivyo kwa kila mchezaji anayejitambua katika kutimiza majukumu yake, lakini kubwa kwake ni kufunga kadri anapopata nafasi.

Alisema kama itashindikana kufunga kwa upande wake basi aweze kutoa mchango kwa kutoa pasi ya mwisho au kutengeneza nafasi kwa mwingine ili aweze kufunga na timu kupata kile ambacho ilijiwekea kabla ya mchezo husika.

“Kama mshambuliaji katika nafasi yangu ambayo nacheza jukumu langu lingine ni kufunga katika kila mchezo hapo ndio yataweza kutokea mambo mawili timu kupata ushindi na lingine kuwa mfungaji bora kwani hiyo ni miongoni mwa malengo yangu,” alisema.

“Nilikuwa nyuma ya waliokuwa wanaongoza katika kufunga kutokana hatukuwa tunacheza mechi za ligi, lakini sasa tunacheza na nadhani timu yangu ina nafasi ya kufanya vizuri, pia naona kabisa kiatu cha dhahabu kinanihusu kama nikiendelea na moto huu huu,” alisema Kagere.

“Washambuliaji wote ambao wapo juu yangu ni wazuri ndio maana wameweza kufunga zaidi yangu, ila nikicheza mechi kama ambazo wamecheza wao naweza kuwafikia na kuwa juu zaidi yao, kifupi ni kwamba sipoi safari hii, hadi kieleweke,” alisema Kagere mwenye mabao 11.

Kagere yupo nafasi ya tatu katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu nyuma ya Salum Aiyee kinara mwenye mabao 13 na Heritier Makambo aliyefunga 12.

MBELGIJI HUYU HAPA

Naye Kocha Aussems akizungumzia mchezo wao kesho, alisema wanajua ugumu uliopo mbele yao na mechi nyingine ijayo dhidi ya Stand United kabla ya kusafiri kwenda Algeria kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saoura, lakini lengo lake ni kupata pointi tatu.

“Washambuliaji wote wamekuwa wakifanya kazi yao ipasavyo ya kufunga na naweza kusema tulikuwa na wiki bora kabisa katika mechi tatu tulizocheza kila mchezaji ndani ya kikosi alifanya kazi yake vizuri na timu iliweza kufikia malengo yake,” alisema.

“Nitaendelea kuwaelekeza mastraika na kikosi kizima kuwapa mbinu zaidi ili kufanya kile ambacho wanatakiwa kufanya katika kila mechi iliyokuwa mbele yetu, lakini akili yetu kwa sasa ipo katika mechi na Lipuli na baada ya hapo itaamia kwa Stand kisha ndio tutaanza kuifikiria JS Saoura,” alisema Aussems.

Mastraika wanne wa Simba wamefunga jumla ya mabao 29, kati ya 38, yaliyofungwa na timu nzima katika mechi 18 walizocheza na anayeongoza ni Meddie Kagere mwenye 11, John Bocco na Emmanuel Okwi kila mmoja ana saba na Adam Salamba akiwa na manne.