Julio, Chambua kusaka vipaji mikoa minne
WACHEZAJI wa zamani, Jamhuri Kihwelo, Sekilejo Chambua wamepewa kazi ya kusaka vipaji katika mikoa minne kwa lengo la kuunda kikosi cha wachezaji 22.
Zoezi la utafutaji wa wachezaji hao wenye umri kuanzia miaka 18 linatarajia kuanzia Mkoani Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam litafungwa.
Wakizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa mashindano makubwa ya mpira wa miguu yajulikanayo kama Safari lager Cup walisema mchakato huo utasaidia kuunda kikosi bora cha timu ya taifa.
Julio alisema ni fulsa kwa vijana wengi hasa mikoani kupata nafasi ya kuonyesha vipaji vyao na hatimaye kufikia malengo yao ya kulitumikia taifa kutokana na vipaji vyao.
“Naipongeza Safari kwa kuona umuhimu huu wa kuibua vipaji miongoni mwa vijana kwani kuna vipaji vingi mno mikoani lakini hakuna wa kuviibua na kuviendeleza.” alisema.
Chambua alisema “Ni heshima kubwa kwetu kupata fursa hii ya kutafuta vipaji Mikoani na kuunda timu hii ya Safari Lager Champions ni matumaini yetu kuwa vijana watajitokeza kwa wingi kwenye usaili ili washiriki katika mashindano haya.”
Meneja wa Chapa ya Safari lager, Pamela Kikuli alisema wameamua kuja na kampeni hiyo ili kuibua vipaji vya mpira wa miguu kwani wanaamini kuna vipaji vingi nchini.
Alisema mashindano hayo yatafanyika katika mikoa minne Mbeya Oktoba 7 uwanja wa FFU Polisi, Arusha Oktoba 27 uwanja wa Ngarenaro, Mwanza uwanja wa Nyamagana Novemba 4 na Dar es Salaam Novemba 18 kwenye viwanja vya Kinesi.
“Timu za mikoa yote minne zitatoa vijana ambao wataunda timu moja kubwa ya wachezaji 22 ambao watacheza mechi ya kirafiki na timu moja wapo ya ligi kuu bara ambayo itatangazwa hapo baadae;
“Pia mchezaji mmoja atapata fursa ya kuchaguliwa na mawakala wa ligi kuu ili kuweza kucheza timu kubwa hapo baadae mawakala watakuwa wakifuatilia vipaji vya wachezaji wa Safari Lager Cup.” alisema.