JKT Tanzania yamnyemelea kiungo Coastal Union
Muktasari:
- Kiungo huyo alitua Coastal Union dirisha dogo akiwa na rekodi ya kuwa miongoni mwa viungo wakabaji bora ndani ya kikosi hicho, huku akisaini mkataba wa miaka miwili na kufanikiwa kupata nafasi ndani ya timu hiyo.
KIUNGO mkabaji wa Coastal Union, Luician Kilua, ameweka wazi kuwa huenda akaondoka ndani ya kikosi hicho baada ya kuvunja mkataba wake timu hiyo, huku akithibitisha kuwa tayari kuna timu zinazomfuatilia kwa ajili ya msimu ujao.
Kiungo huyo alitua Coastal Union dirisha dogo akiwa na rekodi ya kuwa miongoni mwa viungo wakabaji bora ndani ya kikosi hicho, huku akisaini mkataba wa miaka miwili na kufanikiwa kupata nafasi ndani ya timu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti Kilua amesema bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yake msimu ujao, licha ya kuwa alivunja mkatana ambao ulibakiza takribani mwaka mmoja na miezi kadhaa kwenye mkataba wake na Coastal Union.
“Nilikuwa nimebakiza mwaka na miezi ila kwa makubaliano tayari umevunjika,” amesema kiungo huyo.
Nyota huyo ambaye ni mmoja wa viungo wanaofanya kazi kubwa ya kulinda eneo la katikati akiwa na Coastal Union, amesema kwa sasa hajafunga milango kwa timu yoyote na anaendelea kutazama chaguo bora litakalomfaa.
“Sina pa kwenda kwa sasa, naangalia mbadala wowote utakaotokea,” amesema.
Habari ambazo Mwanaspoti imezipata zilieleza kuwa JKT Tanzania ni miongoni mwa klabu zilizoonyesha nia ya kutaka huduma za kiungo huyo, ingawa mazungumzo rasmi bado hayajafikia hatua za mwisho. Kilua mwenyewe alikiri kuwepo kwa mawasiliano ya awali kutoka kwa timu hiyo, lakini akiweka wazi kuwa bado hakuna makubaliano ya moja kwa moja yaliyofikiwa.
“Nina timu moja ambayo imeonyesha nia ya kunihitaji ila kwa sasa siwezi kuitaa kwa sababu bado hatujamaliza mazungumzo vizuri.” Coastal Union imekuwa ikipitia kipindi cha mabadiliko ya kiufundi na kiushindani katika misimu ya karibuni huku ikipambana kuhakikisha inabaki kuwa na ushindani kwenye Ligi Kuu Bara ambapo ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya 08.