Ibenge aitaka Simba, asema ni balaa

KOCHA wa timu ya Taifa ya DR Congo na klabu ya AS Vita Club, Florent Ibenge ameonyesha kukimezea mate kibarua cha kurithi mikoba ya Sven Vandenbroeck  ndani ya kikosi cha Simba kufuatia kauli aliyoitoa jana uwanja wa Benjamini Mkapa mara baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars.

Kocha huyo ambaye alikuwa akiiongoza DR Congo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Taifa Stars, alisema kumekuwa na tetesi nyingi juu yake, ikiwemo kuhusishwa na klabu za Simba na Yanga lakini hana tatizo juu ya kufanya kazi na miongoni mwa klabu hizo kubwa nchini.

Ibenge ambaye alizungumzia hilo mara baada ya mchezo huo wa kirafiki alisema, "Huwa sipendi kuongelea tetesi lakini niseme wazi kuwa mimi ni kocha wa DR Congo kwa ajili ya Chan na Vita club, sipo hapa kuongelea tetesi kwa sababu nimekuwa nikihusika na klabu za Simba na Yanga na kuna muda hata Azam,".

Kwa sasa Simba ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya, kufuatia kuachana na Sven ambaye ametimkia zake Morocco ambako ametangazwa kujiunga na FAR Rabat kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

"Nitakuja Tanzania nikiwa na AS Vita Club. Kiukweli natambua kuwa Simba, Yanga na Azam ni klabu kubwa kwa hapa Tanzania kwa hiyo inawezekana labda siku moja nikaja kufundisha," alisema kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika.

Kuhusu  kundi A  walilopangwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Ibenge alisema ni gumu na hakuna timu ambayo unaweza kusema ni nyepesi huku ikiwa ni mara ya pili kwa kikosi chake kupangwa tena na Simba kwenye hatua hiyo.

"Timu zote ni ngumu  nakumbuka Al Ahly ni timu bora Afrika lakini tuliwafunga Kinshasa, tukiwa nyumbani tuliwafunga Simba kwa mabao 5-0, matokeo hayo hayakutusaidia kusonga mbele na wao wakavuka makundi, tunapaswa kuuchukulia kila mchezo nimgumu," alisema kocha huyo.

Kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mbali na klabu za Simba ya Tanzania na AS Vita ya DR Congo klabu nyingine ambazo zipo kundi hilo ni pamoja na Al Ahly ya Misri na  Al Merrikh ya Sudan.


Imeandikwa na Eliya Solomon, Olipa Assa na Thomas

Ng'itu