Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Feisal aweka wazi kilichomshusha

FEISAL Pict

Muktasari:

  • Hali hiyo imekuja wakati Kocha Mkuu wa JKU, Abdul-Saleh Mohamed akieleza kutoridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo, ambaye kwa sasa amekuwa akipoteza mipira mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa awali.

CHANGAMOTO za kifamilia alizokuwa akipitia nje ya uwanja zimeelezwa ni miongoni mwa sababu za kushuka kiwango cha mshambuliaji wa JKU, Feisal Hilali Nassor, ambaye sasa amesema mambo yamekaa sawa na yuko tayari kurejea katika ubora wake.

Hali hiyo imekuja wakati Kocha Mkuu wa JKU, Abdul-Saleh Mohamed akieleza kutoridhishwa na kiwango cha mshambuliaji huyo, ambaye kwa sasa amekuwa akipoteza mipira mara kwa mara tofauti na ilivyokuwa awali.

Abdul-Saleh amesema Feisal alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa na kiwango kizuri katika kikosi hicho, lakini kwa sasa amekuwa akishindwa kuonyesha ubora wake licha ya kupewa nafasi ya kutosha ya kucheza.

Amesema amekuwa akizungumza naye na kumpa muda wa kujitathmini ili arejeshe kiwango chake, lakini bado hajaona mabadiliko aliyokuwa akiyatarajia.

"Nasikitishwa kuona kiwango cha Feisal kimeshuka, hana mazoezi ya mwili. Nimejaribu kuzungumza naye lakini bado hajabadilika," amesema.

Kocha huyo ameongeza kuwa anaamini Feisal ana uwezo wa kufanya makubwa kutokana na umri wake, lakini anapaswa kuondokana na mambo yanayomchanganya ili kurejesha kiwango chake.

Mwanaspoti ilipomtafuta mshambuliaji huyo, alikiri kupungua kwa kiwango chake na kufafanua changamoto za kifamilia alizokuwa akipitia zilichangia kumvuruga kisaikolojia na kuathiri utulivu wake nje na ndani ya uwanja.

Feisal amesema kwa kipindi hicho alipitia mambo yaliyomfanya ashindwe kuwa na utulivu wake wa kawaida, lakini kwa sasa changamoto hizo zimepata ufumbuzi.

Amesema hali hiyo imemfundisha umuhimu wa uvumilivu na kutenganisha masuala binafsi na majukumu yake ya kila siku kama mchezaji wa kulinda heshima ya timu yake.

Ameongeza kwa sasa anajisikia kuwa na utulivu na yuko tayari kurejea katika majukumu yake kikamilifu, huku akiamini kurejea kwa hali nzuri ya maisha yake kutampa nguvu mpya ya kuimarisha kiwango chake uwanjani.