Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fei Toto ateseka na majeraha aking’ara Azam

Muktasari:

  • Kiungo huyo kinara wa ufungaji Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga mabao 14 pia akiongoza asisti akikusanya nane, imeelezwa kwamba hivi sasa anacheza akiwa na majeraha.

NYUMA ya kile anachokifanya Feisal Salum ‘Fei Toto’ katika kufunga mabao na kuasisti ndani ya Ligi Kuu Bara, hivi sasa kuna maumivu anakabiliana nayo lakini hana budi kuipambania timu kufikia malengo.

Kiungo huyo kinara wa ufungaji Ligi Kuu Bara msimu huu akifunga mabao 14 pia akiongoza asisti akikusanya nane, imeelezwa kwamba hivi sasa anacheza akiwa na majeraha.

Fei Toto ambaye msimu uliopita alimaliza kinara wa asisti Ligi Kuu Bara akiwa nazo 13 huku pia akifunga mabao manne, mechi mbili zilizopita hakumaliza dakika tisini, zote akitolewa kabla ya kufika dakika ya 80.

Akizungumzia hali hiyo, Kocha wa Azam, Florent Ibenge, alisema sababu ya kufanya hivyo ni kumlinda Fei Toto asiumie zaidi kwani anacheza na majeraha.

Alisema licha ya kutamani kumuona akiwa mfungaji bora msimu huu, lakini anaogopa asije akaumia zaidi wakati anategemewa na timu.

“Natamani afunge mabao mengi zaidi na ikiwezekana achukue kiatu kwani hilo litampa thamani kubwa, lakini timu pia inamtegemea ndiyo maana nampa nafasi zaidi ya kupumzika,” alisema Ibenge.

Baada ya Azam kutoka kuichapa Mashujaa kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Azam ilipocheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, Fei Toto alitolewa dakika ya 77, nafasi yake ikachukuliwa na Charles Alobogast.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Mei 22, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Azam ilishinda 2-0, Fei Toto akianza kufunga dakika ya 15 kwa penalti, kisha Idd Seleman ‘Nado’ akamalizia dakika ya 62.

Baada ya hapo, Mei 25, 2026 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Azam Complex ambapo Azam ilishinda 3-0, Fei Toto alitolewa dakika ya 71, akaingia Ashraf Kibeku, kabla ya kutolewa, alifunga mabao mawili dakika ya tatu na 17.

Kiungo huyo amekuwa na kiwango bora kila msimu kwani ilishuhudiwa 2023-2024 akimaliza na mabao 19 na asisti saba, akiwa mfungaji namba mbili nyuma ya kinara Aziz KI aliyefunga 21 wakati anaichezea Yanga.

Kutokana na muendelezo wa kiwango chake, aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Azam, Gibril Sillah anayecheza Al Ahly Benghazi ya Libya, alisema miongoni mwa vipaji alivyoviona Tanzania ni Fei Toto.

“Nimebahatika kucheza na kipaji kikubwa siyo Tanzania pekee bali kwa Afrika ndiyo maana unaona anatakiwa na timu kubwa. Huwa namfuatilia na wakati mwingine namtafuta tunawasiliana namwambia ana kipaji kikubwa na anafanya vizuri,” alisema Sillah aliyewahi kucheza na Fei Toto ndani ya Azam kwa misimu miwili 2023-2024 na 2024-2025.