Dube aipa ubingwa Hardrock
Muktasari:
- Msimu bora kwa Dube katika Ligi Kuu Bara ni wa 2020-2021, alipojiunga na Azam FC kwa mara ya kwanza akitokea Klabu ya Highlanders ya kwao Zimbabwe, ambapo nyota huyo alionyesha kiwango bora na kumaliza nafasi ya tatu kwa wafungaji bora.
ALIYEKUWA mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, ameendeleza kiwango bora na kikosi hicho cha Hardrock FC, baada ya kuchangia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zimbabwe kwa msimu huu wa 2026.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na timu hiyo ya kwao Zimbabwe baada ya kuachana na Yanga Julai 2, 2026, alifunga bao la dakika ya pili katika mechi ya mwisho ya ushindi wa 1-0 dhidi ya FC Platinum, Novemba 21, 2026 na kutwaa taji.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chahwanda uliopo Mji wa Kwekwe, Zimbabwe, Dube alifunga bao hilo dakika ya pili na kuihakikishia ubingwa Hardrock baada ya kufikisha pointi 73, ambazo hazijafikiwa na timu nyingine.
Hardrock FC iliyopanda daraja msimu huu chini ya Kocha Mkuu, Kelvin Kaindu, ilijihakikishia ubingwa huo mechi yake ya mwisho, ikimaliza kwa tofauti ya pointi mbili mbele ya mabingwa watetezi, Scottland FC iliyomaliza ya pili na pointi 71.
Pia, Dube ana nafasi nyingine ya kutwaa taji lake la pili msimu huu akiwa na kikosi hicho cha Hardrock FC, kwani imefuzu tena kucheza fainali ya Chibuku Super Cup watakayocheza dhidi ya Highlanders FC, Jumamosi ya Novemba 28, 2026.
Dube aliyeachana na Yanga baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, alikuwa na ofa mbalimbali kutoka katika klabu zilizomuhitaji, ingawa alichagua kujiunga na Hardrock FC ya kwao Zimbabwe akiamini ni sehemu nzuri kwake.
Nyota huyo alijiunga na Yanga, Julai 6, 2024, akitokea Azam FC na kutwaa mataji mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo.
Katika misimu yake miwili aliyoichezea Yanga, nyota huyo alihusika kwenye mabao 37 ya Ligi Kuu Bara, baada ya msimu wa kwanza wa 2024-2025, kufunga 13 na kuasisti manane, huku msimu uliopita wa 2025-2026, akifunga 10 na kuasisti sita.
Msimu bora kwa Dube katika Ligi Kuu Bara ni wa 2020-2021, alipojiunga na Azam FC kwa mara ya kwanza akitokea Klabu ya Highlanders ya kwao Zimbabwe, ambapo nyota huyo alionyesha kiwango bora na kumaliza nafasi ya tatu kwa wafungaji bora.
Kwa msimu huo wa 2020-2021, mshambuliaji huyo aliifungia Azam FC mabao 14 ya Ligi Kuu Bara, akizidiwa na Chris Mugalu aliyekuwa na 15 na mfungaji bora msimu huo, John Bocco aliyefunga 16, wote wakicheza Simba.