Derby ya Mji Mkongwe ZNZ hakuna mbabe
Mechi kali ya derby Zanzibar inayozikutanisha timu za Mlandege FC dhidi ya Malindi FC imemalizika kwa sare ya 0-0 ikiwa ni mechi ya kundi B kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup.
Timu zote zitajilaumu kwa kutotumia nafasi za wazi walizopata na kufanya mchezo huo kumalizika sare.
Mlandege maarufu Watoto wa Majumba marefu walifunguka mara nyingi na kulisakama lango la Malindi 'Wazoa Dagaa' na mabeki walikuwa makini kuondoa mashambuli huku nao wkaitengeza ila hayakuwa na madhara.
Shambulizi la Mlandege dakika ya 55 ambapo nyota Rashid Mandawa alipoudokonyoa mpira uliompita kipa wa Malindi ila beki alikaa vyema na kuuondosha katikatika ya mstari.
Mchezo huo uliwavuta mashabiki wengi kutoka na maufundi yaliyokuwepo kwa wachezaji wote huku uwepo wa nyota Rashid Mandawa uliwashangaza wengi.
Rashid Mandawa aliyekuwa anacheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini alirudi nchini na kusajiliwa Ruvu Shooting leo ameongoza safu ya ushambuliaji ya Mlandege.
"Ligi imesimama Afrika Kusini hivyo nilirudi nchini na kusajiliwa Ruvu Shooting ila vibali vyangu havikukamilika ikabidi nitafute timu nayoweza kucheza kwakuwa nimekaa nje kwa miezi sita bila kucheza," amesema Mandawa baada ya kuhojiwa.
Kikosi cha Mlandege kilichoanza; Is-haka Hassan, Ali Mwadini, Masoud Juma, Abdallah Janja, Bruno Coster, Hafidh Abdi, Fahad Hassan, Jafar Abdul, Nasir Asaa, Rashid Mandawa, Omar Makungu.
Kikosi cha Malindi kilichoanza; Yussuf Abdu, Abubakar Nyakarungu, Nassor Juma, Ibrahim Abdallah, Muharam Issa, Zuberi Mkombozi, Msati Hamis, Omar Ame, Nassor Juma, Seleman Kassim, Juma Hamad
Mchezo wa kesho Januari 7 utazikutanisha Azam FC dhidi ya Mlandege FC saa 2:15 usiku