Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dar City yatinga nusu fainali Elite 16 Division East

Muktasari:

  • Ushindi huo unaifanya Dar City kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo licha ya kubakiza mchezo mmoja ambao utakwenda kuamua kuongoza Kundi B endapo ikishinda na ikipoteza itakuwa nafasi ya pili, ambayo kikanuni itacheza nusu fainali.

DAR City imeendelea kuonyesha dhamira yake ya kufanya vizuri katika mashindano ya Elite 16 Division East, baada ya juzi Jumanne Novemba 24, 2026 kushinda mchezo wa pili wa Elite 16 Division East kwa pointi 91-76 dhidi Namuwongo Blazers ya Uganda mchezo uliochezwa Kasarani Indoor Arena, Kenya.

Ushindi huo unaifanya Dar City kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo licha ya kubakiza mchezo mmoja ambao utakwenda kuamua kuongoza Kundi B endapo ikishinda na ikipoteza itakuwa nafasi ya pili, ambayo kikanuni itacheza nusu fainali.

Katika mchezo huo, Dar City ililazimika kufanya kazi kubwa kabla ya kupata ushindi wa pointi 91-79. Namuwongo ilionyesha upinzani mkali kwa muda mwingi wa mchezo na hata kuingia robo ya mwisho ikiwa mbele kwa pointi 67-66.

Hata hivyo, robo ya nne ilikuwa tofauti kabisa. Dar City iliongeza kasi ya mashambulizi, ikatumia vizuri makosa ya wapinzani na hatimaye kupata ushindi wa pointi 12.

Katika mchezo huo, Tyler Bey na Nisre Zouzoua walikuwa vinara wa ufungaji kwa Dar City baada ya kila mmoja kupata pointi 24.

Jean-Jacques Boissy aliongeza pointi 20, huku Youssou Ndoye akichangia pointi 18, takwimu zinazoonyesha namna Dar City ilivyokuwa na njia tofauti za kupata vikapu.

Ushirikiano wa wachezaji hao ulikuwa sehemu muhimu ya ushindi huo, hasa katika robo ya mwisho ambayo Dar City ilifanikiwa kujitenga na wapinzani wake.

Kwa upande wa Namuwongo, Franck Nyembo alikuwa mchezaji aliyefunga pointi nyingi zaidi kwa kupata 27, lakini juhudi zake hazikutosha kuizuia Dar City kupata ushindi.

Moja ya mambo yaliyoigharimu timu hiyo ya Uganda ni makosa ya kupoteza mpira, ambayo Dar City iliyatumia kupata pointi muhimu na kubadilisha mwelekeo wa mchezo.

Katika michezo mingine, Ferroviario da Beira ya Msumbiji iliichapa Dolphins BC ya Botswana kwa pointi 94-62, matokeo yaliyoiweka Beira katika nafasi nzuri ya kuwania tiketi ya nusu fainali.

Patriots ya Sudan Kusini ilipata ushindi wa kusisimua wa pointi 109-108 dhidi ya Urunani ya Burundi katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa hadi dakika za mwisho.

Matokeo hayo yanaonyesha ushindani mkubwa uliopo katika mashindano hayo, ambako tofauti ndogo za pointi zinaweza kuwa na athari kubwa katika msimamo wa makundi.

Baada ya kujihakikishia nafasi ya nusu fainali, macho ya Dar City sasa yanaelekezwa katika mchezo wake wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Dolphins BC ya Botswana utakaochezwa leo Alhamisi, Novemba 26, saa 9:00 alasiri.

Licha ya kuwa tayari imefuzu hatua inayofuata. Ushindi katika mchezo huo unaweza kuipa nafasi nzuri ya kumaliza ikiwa kileleni mwa Kundi B na kujiweka katika mazingira mazuri zaidi kuelekea nusu fainali.

Dolphins kwa upande mwingine, itakuwa na jukumu gumu la kutafuta matokeo mazuri baada ya kupoteza dhidi ya Ferroviario da Beira kwa tofauti kubwa ya pointi 32.

Kwa mfumo wa mashindano, timu mbili zitakazomaliza nafasi za kwanza na pili katika kila kundi zitafuzu nusu fainali itakayochezwa Novemba 28, 2026.  Washindi wa michezo hiyo miwili watajihakikishia tiketi ya kushiriki Basketball Africa League (BAL) 2027, wakati timu bora iliyomaliza nafasi ya tatu kati ya Division East na Division West itapata nafasi nyingine ya kufuzu.