Chama wa moto, Simba ikiifanyia ukatili Prisons
Muktasari:
- Ushindi huo wa Simba ikicheza mchezo wake wa kwanza kwenye Uwanja wa KMC Complex tangu irejee hapo kutoka Meja Jenerali Isamuhyo, unakuwa wa 14 msimu huu kwenye mechi 22, ikiendelea kusalia nafasi ya pili ikifikisha jumla ya pointi 49 ikiifukuza Yanga iliyo juu kwenye nafasi ya kwanza na pointi 54.
SIMBA imeendelea kutamba nyumbani ikiichapa Tanzania Prisons mabao 4-0, huku kiungo wake Clatous Chama akizidi kuibeba timu hiyo.
Ushindi huo wa Simba ikicheza mchezo wake wa kwanza kwenye Uwanja wa KMC Complex tangu irejee hapo kutoka Meja Jenerali Isamuhyo, unakuwa wa 14 msimu huu kwenye mechi 22, ikiendelea kusalia nafasi ya pili ikifikisha jumla ya pointi 49 ikiifukuza Yanga iliyo juu kwenye nafasi ya kwanza na pointi 54.
Mapema tu Simba ikapoteza nafasi nzuri ya kupata bao la kutangulia dakika ya 12 kupitia penalti lakini mshambuliaji wake Seleman Mwalimu akapaisha.
Hata hivyo, Simba ikapata bao lake la kwanza dakika ya 27 mfungaji akiwa kiungo Morrice Abraham akimalizia mpira uliokuwa ukiokolewa na mabeki wa Prisons.
Bao hilo ni la pili kwa Morrice msimu huu akiwa Simba huku pia ameshatengeneza asisti moja kwenye mechi alizocheza.
Simba ikapata bao la pili mfungaji akiwa Chama akifunga bao lingine Kali ndani ya wiki moja, akimnyanyulia mpira kipa Mussa Mbisa aliyetoka kwenye eneo lake.
Kabla ya mapumziko Mwalimu akafanikiwa kusahihisha makosa yake akifunga bao zuri akimalizia asisti nzuri ya Libase Gueye na Wekundu hao walienda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Simba ikaonyesha bado inataka ushindi mkubwa ambapo dakika ya 62 beki Ismael Toure akamalizia msumari wa mwisho kwa kichwa akitumia kona iliyopigwa na Chama.
Hiyo inakuwa asisti ya nne kwa Chama msimu huu akiwa na mabao sita na kumfanya kiungo huyo kuhusika kwenye mabao 10 mpaka sasa.
Chama ameendeleza moto wake ambapo amefunga mechi tatu mfululizo akitangulia kuifunga Yanga, JKT Tanzania na leo Prisons.
Prisons haikuwa na ugumu wowote mbele ya Simba, ambapo kazi kubwa imekuwa kwa kipa wake Mbisa ambaye amefanya kazi kubwa ya kuzuia mashambulizi makali ya wenyeji.
Kipigo hicho kinaicha Prisons nafasi ya 15 na pointi 14 baada ya kucheza mechi 22. Bado ina kazi ya kufanya kujiokoa na janga la kushuka daraja.