Balinya ,Sibomana kazi kwao tu
Muktasari:
Abdul amejiunga na Yanga hivi karibuni baada ya kupunguziwa malimbikizo ya madeni yake aliyokuwa akiidai na kuingia moja kwa moja kikosini baada ya Paul Godfrey ‘Boxer’ kuwa majeruhi na Kocha Zahera alisema urejeo wa beki huyo na Kelvin Yondani ni faida kwa timu yake iliyokimbilia Kanda ya Kaskazini kunoa makali kwa mechi mbili maalumu.
KAMA Township Rollers inapiga hesabu za kuing’oa Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikitaka kurudia ilichokifanyia mwaka jana, basi ijue mapema inakula kwao, kutokana na mpango kamambe aliousuka Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera .
Zahera na jeshi lake likiwa limeshatua Kanda za Kaskazini ili kunoa makali kwa mchezo huo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo, amesuka mpango mmoja matata ambao labda tu mastraika wake kina Juma Balinya ‘JB’, Patrick Sibomana na Sadney Urikhob washindwe kufanya mambo mjini Gaborone.
Kocha huyo amelidokeza Mwanaspoti jana Jumatano kuwa, kurejea kwa beki wake wa kulia, Juma Abdul ni mkakati wake maalumu wa kuhakikisha wanaing’oa Township kwao kitakachobaki ni washambuliaji wake kuwa na kazi ya kutupia tu nyavuni.
Abdul amejiunga na Yanga hivi karibuni baada ya kupunguziwa malimbikizo ya madeni yake aliyokuwa akiidai na kuingia moja kwa moja kikosini baada ya Paul Godfrey ‘Boxer’ kuwa majeruhi na Kocha Zahera alisema urejeo wa beki huyo na Kelvin Yondani ni faida kwa timu yake iliyokimbilia Kanda ya Kaskazini kunoa makali kwa mechi mbili maalumu.
Alifichua anataka kumtumia Abdul kwenye mechi hiyo ya ugenini kumimina krosi zenye macho ambazo zitakuwa zikiwafikia mastraika wake watakaokuwa na kazi ya kufunga tu, baada ya kubaini kwenye mchezo wa kwanza wiki iliyopita walizikosa krosi hizo.
“Kikosi chetu kilikuwa kikimtegemea zaidi Boxer ambaye atakuwa nje kwa muda baada ya kuumia goti kwenye mchezo wa awali ulioisha kwa sare ya 1-1, lakini hata wale ambao niliwatumia kuziba nafasi yake hawakufiti ndio maana nimefurahi Abdul kurejea,” alisema.
Zahera alisema kwa jinsi alivyowasoma wapinzani wake amegundua ni wabovu kwenye mipira ya krosi, hivyo ujio wa beki huyo anayefanya vizuri eneo hilo inaweza ikawa dawa dhidi ya wapinzani wao kuweza kupatia matokeo katika uwanja wao wa nyumbani.
Kuhusu Yondani, Zahera alisema pia ana nafasi ya kucheza itategemea na mfumo atakaoutumia, huku akiwamwagia sifa mabeki Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro jinsi walivyocheza kwa kuelewana hawakuwa na makosa mengi kwenye mchezo huo.
Alisema kwa mfumo wa kuchezesha mabeki watatu Yondani anaweza kufiti kwa kukaa kati huku Sonso na Moro wakiwa pembeni yake, lakini alisisitiza mchezo unaofuata unahitaji mawinga wenye kasi sambamba na mabeki wa kupanda kupitia pembeni.
Akizungumzia maandalizi kwa ujumla alisema wanaendelea kujiandaa na wanatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki ukiwamo wa kesho dhidi ya Polisi Tanzania kabla ya kumalizana na AFC Leopards ya Kenya.
Katika mechi yao ya kwanza jijini Dar es Salaam Yanga ililazimika kusawazisha kwa penalti dakika za jioni na kutoka sare ya 1-1, ikiwa na kazi ya kwenda kupata matokeo ya ushindi ama sare ya mabao zaidi ya mawili kama inataka kufuzu raundi ya kwanza.
Mwaka jana Township iliing’oa Yanga katika raundi ya kwanza ya michuano huyo baada ya kupata ushindi wa 2-1 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na Yanga kufanikiwa kwenda kulazimisha suluhu ugenini.
Hata hivyo, Yanga iliy mwaka huo iliangukia playoff ya Kombe la Shirikisho na kuitoa Welaita Dicha ya Ethiopia na kutinga makundi.