Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bado kidogo tu, Ajib atakifukuza kivuli cha Mhilu

Muktasari:

Huko nyuma ungepata kigugumizi kikubwa pale unapotakiwa kujibu, nani mwenye kipaji halisi cha soka kwenye kila nafasi, angalau utaje wachezaji wawili tu.

BILA ya shaka unapotaka kuanza kuzungumzia vipaji hasa vya wachezaji wazawa wa Kitanzania huwezi kukosa kulitaja jina la Ibrahim Ajibu, anayeichezea Yanga kwa sasa. Nchi hii ina wachezaji wengi kwenye nafasi mbalimbali ndani ya uwanja ambao wana vipaji halisi vya kuzaliwa vya soka, ingawa kwa miaka ya karibuni vipaji hivyo vimeanza kupotea kwa kasi.

Huko nyuma ungepata kigugumizi kikubwa pale unapotakiwa kujibu, nani mwenye kipaji halisi cha soka kwenye kila nafasi, angalau utaje wachezaji wawili tu. Ni wazi usingeweza kumaliza kwa sababu kila eneo lilikuwa na wachezaji zaidi ya kumi wenye vipaji halisi vya hali ya juu kuwazidi wenzao nchi nzima.

Ajib anayecheza nafasi ya ushambuliaji, kweli ana kipaji kikubwa cha soka na ni aina ya kina Haruna Moshi ‘Boban’ wachezaji waliopata bahati ya kuwa na kipawa cha soka lakini hawakukitumii ipasavyo.

Ajibu ndiye aliyekuwa na mvuto mkubwa kipindi cha usajili wa dirisha kubwa lililopita, kwani jina lake aligonga vichwa vya habari nchi nzima, yeye na Haruna Niyonzima wakionekana ndio usajili mkubwa na muhimu zilizofanywa na klabu za Simba na Yanga.

Ajib aliendelea kuonekana ni mchezaji aliyesajiliwa na kuipa faida timu aliyokwenda, yaani Yanga, huku akiifungia timu yake hiyo mabao muhimu na mazuri, kuanzia zile faulo mbili zinazofanana moja dhidi ya Njombe Mji, mjini Njombe na nyingine dhidi ya Stand Utd kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga.

Bila shaka Ajib akawa ndiye mshambuliaji mbunifu zaidi ndani ya Ligi Kuu ya Vodacom kwa kipindi hicho, lakini taratibu kadri Ligi Kuu ilivyokuwa ikiendelea na uwezo wake aliokuwa ameuonyesha ukawa unapotea taratibu.

Ajibu kwa sasa si mshambuliaji anayetisha ndani ya uwanja, ameanza kushambulia kurudi anakotoka au kurudi langoni kwake. Ajib wa sasa hamfuati beki au mchezaji wa timu pinzani kumpunguza na kuingia kwenye eneo la mwisho.

Hatengenezi nyendo nyingi kwenda langoni kwa wapinzani na wala hapigi mashuti na hana mipango ya kulazimisha kuingia golini. Kwa kifupi Ajib huyu wa miezi hii ya mwishoni mwa ligi, sio yule wa miezi ya mwanzo ya ligi, amepungua sana makali.

Inawezekana benchi la ufundi limesaidia kumpungizia makali kutokana na kutompa nafasi huru ya kucheza uwanjani, hasa pale walipokuwa wakimfanyia mabadiliko, hata kama siku hiyo kiwango chake kilikuwa kipo vizuri sana, bado walimu walikuwa wakimpumzisha.

Inawezekana pia kupungua kwa kiwango chake kulitokana na nafasi aliyokuwa akicheza ambako kule alikokuwa akitakiwa kutokea bado makocha waliwaweka mawinga kama kina Mwashiuya na Mahadhi ambao wote ni wachezaji wanaocheza wakitokea pembeni kabisa sehemu ambayo Ajib hupenda kufungulia.

Hata hivyo, sasa kuna ingizo moja la mchezaji kijana kutoka kikosi cha pili cha Yanga, Yusuf Mhilu. Huyu ni kijana ambaye kiuhalisia sio mbunifu wala mwenye kipaji lakini ni kijana anayejituma sana. Ni mchezaji mshambuliaji anayeonekana kukubali kuwa bado kabisa hajajua mpira, lakini ni wazi jitihada zake ndizo zitakazomtoa.

Huko nyuma kipindi Ajib anahesabika kama mchezaji wa Simba mwenye kipaji, kule Yanga kulikuwa na mchezaji anayeitwa Simon Msuva.

Msuva hakuwa na jina kubwa kulinganisha na Ajib na hata ilipotokea Msuva kaongoza kwenye jopo la wafungaji bora huku Ajib hafungi sana, bado Msuva hakuwa na bahati ya kusifiwa.

Silaha kubwa aliyokuwa nayo ndani ya uwanja ni kasi na kujituma zaidi huku akipitia changamoto nyingi ikiwamo kuzomewa kila alipofanya kosa, wakati mwenzake Ajib kwa Simba akifanya kosa mashabiki na wanatulia na akifanya vizuri wanashangilia kwa nguvu.

Kuzomewa kwa Msuva kulimfanya kutokukata tamaa na badala yake aliongeza bidii kila siku na kufanikiwa kuwa ndani ya chati ya wafungaji bora kwa misimu mitatu mfululizo.

Alichokuwa akikifanya Msuva kwa sasa kinaanza kuonekana miguuni mwa Mhilu. Ni kweli Mhilu bado hajaiva kabisa, anafanya makosa mengi ya kiuchezaji ndani ya uwanja, hana uwezo mkubwa wa umiliki wa mpira na sio mbunifu kama Ajib, lakini moja kati ya faida alizonazo ni kutokukata tamaa.

Mhilu ni mchezaji asiyerudi nyuma kirahisi ana kasi nzuri na kimo kizuri kabisa, anaweza kupambana na sio mtegeaji ndani ya uwanja. Pia bado anajiona hajajua mpira na ndiyo maana imekuwa rahisi kumshauri na kushaurika.

Kinachoendelea kwa Mhilu ni kuanza kuzoea kufunga na ikiwa atakuwa akifunga kila mara, bila shaka kwa bidii aliyonayo isiwe ajabu kumwona akiwa nyota mkubwa baadaye wa klabu ya Yanga. Bahati aliyonayo ni kuwa hawezi kupitia changamoto za Msuva za kuzomewa kwa kuhisiwa ana vinasaba vya Usimba. Pia Msuva aliyekuwa akidhaniwa hakutakiwa kucheza Yanga kutokana na historia yake kuonyesha mwanzo hakuwa mchezaji kabisa bali alikuwa akijihusisha na muziki.

Mhilu anaweza kubadilika zaidi huko baadaye kwa kuwa haogopi kumfuata mpinzani, haogopi kushambulia kwa kurudi nyuma na bado ana kiu ya kuwa mchezaji mahiri baadaye. Muda si mrefu nyota wa soka kwa wachezaji wazawa ndani ya Yanga atabadilika kutoka kuwa na mategemeo kwa Ajib hadi kuanza kumtegemea Mhilu. Ajib anatakiwa kujitambua sasa kuwa kaka zake wengi wamepitia Simba na Yanga, lakini bado wapo nchini, kina Boban, Jerrison Tegete, Mrisho Ngassa hawa ni mfano kwake kwa wachezaji wa miaka ya hivi karibuni ambao walikuwa nyota wa kweli kwenye klabu zao hasa Yanga lakini kwa leo wapo wapi.

Kipindi anaingia Msuva, Yanga nyota wa kweli alikuwa Ngassa huku Msuva akiingia pale kujaribu bahati yake kwani ilikuwa hakuna namna kuishusha nyota ya Ngassa.

Fikra kubwa kwa watu wengi wa Yanga walikuwa wakimtegemea Msuva kurithi nafasi ya Ngassa mara tu atakapokuwa ameihama klabu hiyo na kwenda nje ya nchi, hakuna mtu aliyekuwa akitegemea kumwona Msuva akiwa anacheza nje ya nchi huku Ngassa akiwa anacheza Ndanda, huku Tegete akiwa anaichezea Majimaji na Boban akiwa pale Manzese.

Kipaji ni kitu kingine na bidii ni kitu kingine cha pili ambacho husaidia kuendeleza kile ulichonacho. Huko nyuma kulikuwa na wachezaji wengi wenye vipaji vya soka kama kina Edibily Lunyamila, Salvatory Edward, Nteze John Lungu na wengineo, ila walikuwa na mwendelezo mkubwa sana wa kufanya mazoezi na kuyafanya yale wayafanyayo nje ya mechi kuyaingiza ndani ya mechi halisi.