Prime
Azam yafunguka kipengele cha Yanga, Fei Toto kutua Simba

Muktasari:
- Basi neno hilo limerejea tena kwa kishindo likiwahusisha haohao Simba na Yanga, lakini safari hii ni kupitia mkataba wa Feisal Salum maarufu zaidi kama Feitoto, Failasufi au Zanzibar Finest.
Unakumbuka neno kipengele lilivyogonga vichwa vya habari wakati wa sakata la kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi?
Basi neno hilo limerejea tena kwa kishindo likiwahusisha haohao Simba na Yanga, lakini safari hii ni kupitia mkataba wa Feisal Salum maarufu zaidi kama Feitoto, Failasufi au Zanzibar Finest.
Mchezaji huyo wa Azam FC amekuwa akihusishwa kuhamia Simba kwa muda mrefu, lakini kizingiti namba moja kwa Wekundu wa Msimbazi kimekuwa kipengele kilichowekwa na Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa, kuna kipengele kwenye mkataba wa Feitoto kinachoitaka Azam FC kuilipa Yanga Sh1 bilioni endapo Feisal Salum atauzwa kwenda Simba. Inasemekana Yanga waliweka kipengele hicho kwenye mkataba wa Feisal.

Lakini, taarifa hizo hazikuwahi kukanushwa au kuthibitishwa na upande wowote; Azam FC, Yanga au mchezaji, hadi hivi karibuni alipoibuka mwanadada Yasmin Razack ambaye ni msimamizi wa mchezaji huyo.
Mwanadada huyo mzoefu wa usimamizi wa wachezaji kutokana na ukaribu wake na wachezaji wengi wakubwa wa Kiafrika wanaocheza Ulaya, hasa England ndiye aliyemsaidia Saimon Msuva kushinda kesi dhidi ya Wydad Athletic 2022.
Katika mahojiano yake ya hivi karibuni na baadhi ya vyombo vya habari, Yasmin alikanusha kuwepo kwa kipengele hicho kwenye mkataba wa Feisal.
Kukanusha kwa Yasmin kukabadilisha uelekeo wa upepo wa sakata hilo na kuendelea kuvuruga akili za mashabiki wa soka, hasa wa Simba ambao sasa walianza kupata picha mpya.
Kutokana na hilo, gazeti hili likamtafuta Zaka Zakazi, mkuu wa idara ya habari na mawasiliano wa Azam FC ili kupata ufafanuzi kutoka upande wao.
Kupitia mahojiano ya simu, Zaka akasema ameona kwenye mitandao ya kijaminii Yasmin akikanusha uwepo wa kipengele hicho.

"Naweza kusema majibu ya Yasmin yako sahihi kutokana na aina ya swali aliloulizwa," alisema Zaka kisha akaendelea:
"Ukisoma katikati ya mistari kwenye majibu yake utabaini kwamba swali aliloulizwa lilikuwa je kuna kipengele kwenye mkataba wa Feitoto?" alisema Zaka akielezea undani wa taarifa hiyo.
"Yasmin ni msimamizi wa Feisal Salum, na yeye anahusika na mkataba kati ya Feisal Salum na Azam FC, na ndio aliouzungumzia hapo."
Zaka anasema kipengele hicho hakipo kwenye mkataba wa Azam FC na Feisal anaoujua Yasmin.
"Kipengele hiki kipo kwenye mkataba wa mauziano baina ya Azam FC na Yanga, ambako Yasmin hahusiki nao."
Zaka aliongeza kwa kusema ili mtu aelewe vizuri juu ya uwepo wa kipengele hicho anatakiwa kwanza ajue hatua ambazo Azam FC walipitia hadi kufanikisha kumpata Feisal.
"Kabla ya kukutana na Feitoto na wasimamizi wake akiwemo Yasmin, tulikutana kwanza na Yanga na kufanya nao mazungumzo, kama wamiliki wa mchezaji," akasema Zaka.
Anasema taratibu za uhamisho haziruhusu kuanza kuzungumza na mchezaji bila ridhaa ya klabu yake.

"Katika hayo mazungumzo baina yetu na Yanga hadi kufikia makubaliano ya kufanya biashara, ndio wakaweka hayo masharti kwamba kuwepo na kipengele hicho kwenye mkataba wa mauziano."
Gazeti hili likamuuliza Zaka, kwanini walikubali kipengele hicho ambacho ni kigumu?
"Hiki kipengele sio kigumu hata kidogo kwa sababu sisi hatumkununua Feitoto ili tumuuze kwa klabu yoyote, tumlinunua ili aitumikie timu yetu," akasema.
Zaka akasema hata kama Yanga wangeweka kipengele cha Sh500 bilioni bado wangesaini kwa sababu wao hawakuwa na lengo na kumuuza Feitoto kwenda timu yoyote, achilia mbali Simba kwa hiyo hawakuwa na hofu.
"Kwa hiyo baada ya kukubaliana na Yanga na kutupa ruhusa ya kuongea na mchezaji ndio tukawatafuta kina Yasmin. Mazungumzo yetu na Yanga hayakuwahusu wao...kwa hiyo hawezi kujua lolote kuhusu sisi na Yanga."
Kwa majibu hayo ni dhahiri kwamba ni kweli kipengele kipo, lakini ni kati ya Azam FC na Yanga, sio Azam FC na Feisal wala Yanga na Feisal.
Sakata linarudi palepale kwamba ili Feisal auzwe kwenda Simba ni lazima Yanga ipate hicho kiasi cha pesa, hata kama mkataba wa mchezaji huyo na Azam FC hausemi hivyo, lakini mwenye haki ya kuuza mchezaji ni klabu.
Kama Azam FC ikikataa kumuuza Feisal kwenda Simba, Yasmin na watu wake hawawezi kufanya chochote hata kama mkataba walionao hauna hicho kipengele. Wao kama wasimamizi wa mchezaji hawana haki ya kuichagulia klabu inayommiliki mchezaji wao klabu ya kwenda.
Kwa hiyo, Azam FC ndio yenye uamuzi, kumuuza Feitoto kwenda Simba na kuilipa Yanga Sh1 bilioni au vinginevyo.
Na vipengele kama hivyo sio vigeni kwenye mpira, vimekuwepo kwa muda mrefu na hata Simba wenyewe walikiweka kwenye mkataba wa mauziano ya Luís Miquissone kwenda Al Ahly, ili kumzuia asije akarudia Yanga na hata Azam FC walikiweka kwenye mauziano ya Kipre Jr kwenda MC Alger ya Algeria asije akarudi klabu yoyote Tanzania.
Arsenal walikiweka kwa Barcelona kwenye mauziano ya Cesc Fabregas, lakini sharti lao halikuwa kiasi cha pesa, bali haki ya kuulizwa wao kwanza kama wanamhitaji endapo Barcelona itataka kumuuza.

Na kweli, wakati Barcelona ilipoamua kumuuza Fabregas, Arsenal walikuwa wa kwanza kuulizwa kama wanamtaka. Arsene Wenger, kocha wa zamani wa timu hiyo akasema hana mpango naye kwa sababu tayari ana Mesut Ozil, ndipo Fabregas akauzwa kwenda Chelsea.
Makubaliano baina ya klabu na klabu kwenye mauziano ya mchezaji ni kawaida na hayamhusishi mchezaji kwa sababu yeye sio sehemu ya mazungumzo hayo.