Azam: Simba wanapigwa na ubingwa wao
LICHA ya Simba kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini uongozi wa Azam FC umesema wasitegemee mteremko pindi watakapokutana kwenye mechi yao ya ligi.
Timu hizo zinatarajia kukutana keshokutwa, Alhamis kwenye Uwanja wa Mkapa, huku Azam nayo ikiwa na uhakika wa kushiriki michuano ya kimataifa baada ya kujihakikishia kuwa ndani ya nne bora zilizofuzu hatua hiyo msimu ujao.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Zakaria Thabith ‘Zaka Zakazi’ alisema kuwa wamejipanga vizuri kuelekea mechi hiyo licha ya kutambua ugumu wa mchezo kutokana na ubora wa timu wanayokutana nayo.
“Tunaenda kwenye mechi muhimu kwetu, tunatambua Simba ni mabingwa, ila hii haitutishi kwani ni nafasi ya kuendelea kuonyesha ubora na thamani ya kikosi chetu, kwa kuonyesha ushindani mkubwa tofauti na watu wanavyodhani pindi tunapokutana na Simba. Hata mzunguko wa kwanza mechi ilikuwa ya ushindani,” alisema
Hivi sasa timu hiyo inaendelea kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao, lakini bado wanasubiri ripoti zaidi ya kocha wao mkuu, George Lwandamina kwa ajili ya maboresho ya kikosi.
“Watu wengi wanadhani kuwa usajili tunaoufanya sasa unatokana na ripoti ya msimu huu ya Lwandamina, hapana, nyota wote waliosajiliwa hadi sasa ni wale waliopendekezwa kabla ya dirisha dogo.
“Kuhusu ripoti mpya ya usajili bado tunaisubiri kutoka kwa kocha na hii ataitoa mara baada ya kumalizika kwa ratiba ya michezo ya msimu huu.” alisema.
Hadi sasa usajili uliofanywa na timu hiyo ni wa Charles Zulu kutoka Cape Town City ya Afrika Kusini aliyetua kikosini kwa mkataba wa miaka miwili utakaoanza kutumika rasmi kuanzia msimu ujao wa 2021/22.
Pia, wamewaongeza mikataba nyota wao Prince Dube, Idd Nado, Ayoub Lyanga na Bryson David.