Amunike: Tanzania tutakwenda Afcon mwaka huu
Muktasari:
Ndoto ya Taifa Stars kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1980, zitafutika rasmi hata kama itaifunga Uganda iwapo Lesotho itaibuka na ushindi ugenini kwa kuwa zitakuwa na idadi sawa ya pointi lakini Taifa Stars itaondoshwa kwa sheria ya kutokuwa na matokeo mazuri mbele ya Lesotho pindi timu hizo zilipokutana katika mechi mbili baina yao.
Dar es Salaam. Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amewataka Watanzania kuamini kuwa timu hiyo itaibuka na ushindi dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Jumapili na kukata tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Misri mwezi Juni.
Taifa Stars inalazimika kushinda dhidi ya Uganda huku ikiomba dua kwa kuombea Cape Verde iibuke na ushindi ama kutoka sare na Lesotho ili kuungana na Uganda kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980.
Amunike alisema Taifa Stars ina uwezo wa kuibuka na ushindi dhidi ya Uganda kwa kuw ana kikosi imara, inafanya maandalizi ya kutosha na pia itabebwa na faida ya kucheza nyumbani.
"Tunapaswa kuamini kwamba ndoto zetu ziko hai na zinaweza kutimia. Maandalizi ambayo tunaendelea kuyafanya yananipa matumaini kuwa timu inaweza kufanya kile ambacho tunahitaji na nimewaambia wachezaji wangu kuwa wasahau kile kilichotokea nyuma na kurekebisha makosa tuliyofanya yasijirudie kwenye mchezo huu.
Nawafahamu Uganda ni timu ngumu ina wachezaji wazuri lakini hatuwaogopi. Hautakuwa mchezo rahisi kwetu na kutakuwa na nyakati ambazo tutakuwa juu na zile ambazo tutakuwa chini ingawa kwetu tutakuwa na faida ya kucheza nyumbani," alisema Amunike.
Amunike alisema kutokana na ubora wa wapinzani wao, Taifa Stars haitacheza kwa kujilipua japo ina ulazima wa kuibuka na ushindi katika mchezo huo.
"Tunatakiwa kuwa na uwiano mzuri wa kujilinda na kushambulia ndio maana hata wachezaji ambao nimewaita kikosini, nimeangalia wale ambao wataweza kufanya kitu pindi tunapokuwa na mpira lakini pale tutakapopokonywa wahusike katika kuusaka," alisema Amunike.
Amunike alisema uwepo wa nyota 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayechezea KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji.
"Kwa wachezaji morali ipo juu na ukizingatia nyota wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamefika kwa wakati na kuwa na mwitikio chanya naamini watakuwa chachu kwa wengine kikosini," alisema Amunike.
Ukiondoa Samatta, nyota wengine wanaocheza soka la kulipwa waliopo kikosini ni pamoja na ni Rashid Mandawa (BDF XI), Hassan Kessy (Nkana), Saimon Msuva (Difaa el Jadida), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), Farid Musa (CD Tenerife), Shaban Chilunda (CD Izarra), Himid Mao (Petrojet), Shiza Kichuya (ENPPI) na Yahya Zayd (Ismaily)
Taifa Stars inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo, iwapo itaibuka na ushindi dhidi ya Uganda itafikisha pointi nane ambazo zinaweza kuivusha ikiwa Lesotho yenye pointi tano itapoteza au kutoka sare na Cape Verde yenye pointi nne.
Lakini, ndoto ya Taifa Stars kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 tangu ilipofanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1980, zitafutika rasmi hata kama itaifunga Uganda iwapo Lesotho itaibuka na ushindi ugenini kwa kuwa zitakuwa na idadi sawa ya pointi lakini Taifa Stars itaondoshwa kwa sheria ya kutokuwa na matokeo mazuri mbele ya Lesotho pindi timu hizo zilipokutana katika mechi mbili baina yao.