Amir Njeru ala shavu Comoro
Muktasari:
- Mbali na KenGold FC na Biashara United, Njeru aliwahi kupitia akademi ya Azam FC ya Dar es Salaam na kuitumikia timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys mwaka 2019.
BEKI wa kati wa zamani wa KenGold FC ya Mbeya, Amir Njeru, amekamilisha uhamisho wa kujiunga na FC Hantsindzi inayoshiriki Ligi Kuu ya Comoro, akisaini mkataba wa mwaka mmoja.
Njeru, ambaye ana uwezo pia wa kucheza kiungo mkabaji, amejiunga na klabu hiyo baada ya kukaa bila timu tangu alipoachana na KenGold FC katika dirisha dogo la usajili la Desemba 2024.
Akizungumza baada ya kukamilisha uhamisho huo, Njeru amesema amefurahi kupata nafasi ya kucheza soka nje ya Tanzania, akieleza kuwa fursa hiyo imempa motisha mpya ya kuendelea kupambana baada ya kipindi cha kukosa timu.
Alijiunga na KenGold FC Agosti 15, 2024, akitokea Biashara United ya Mara, ambako alikuwa akicheza kabla ya kuhamia Mbeya kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Hata hivyo, aliondoka KenGold Desemba 18, 2024, kabla ya kumalizika kwa mkataba wake, baada ya kupata ushindani mkubwa wa nafasi kufuatia kuongezwa kwa wachezaji wenye uzoefu katika dirisha dogo la usajili.
Hali hiyo ilimfanya akose nafasi ya kucheza mara kwa mara na hatimaye kusitisha mkataba wake wa miezi sita uliokuwa umebaki.
Mbali na KenGold FC na Biashara United, Njeru aliwahi kupitia akademi ya Azam FC ya Dar es Salaam na kuitumikia timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys mwaka 2019.