Aliyekuwa kocha Simba ajiunga Yanga
Muktasari:
- Uongozi Yanga uliamua kuvunja mkataba na Edna Lema aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Princess na msaidizi wake Mohamed Hussein 'Mmachinga' baada ya timu hiyo kufungwa na Fountain Gate Princess bao 1-0 kwenye Ligi Kuu Bara ya Wanawake.
BAADA ya siku mbili tu uongozi ya Yanga kumuondoa Kocha Edna Lema, leo wamemtangaza kocha wa zamani wa Simba Queens, Sebastian Nkoma kuchukua mikoba Yanga Princess.
Nkoma alikuwa kocha wa Simba Queens na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara mara mbili mfululizo.
Kocha huyo aliondolewa Simba Septemba mwaka huu baada tu ya kuipa ubingwa wa Cecafa kwa kuifunga She Corparate ya Uganda bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Agosti 27.
Ilidaiwa Simba iliamua kuachana na Nkoma kutokana na kutokuwa na leseni A ya ukocha ambayo ingemfanya kukaa benchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Simba ilifuzu na kuishia hatua ya nusu fainali.
Kutokana na kutokuwa na vigezo hivyo, Simba ilimleta kocha wa She Coorparate ya Uganda, Charles Lukula ambaye ndio kocha wa timu hiyo hadi sasa.
Ilidaiwa kuwa Simba ilitaka kuendelea na Nkoma ili awe msaidizi chini ya Lukula lakini kocha huyo wa zamani wa Majimaji ya Songea aligoma.
Hivi karibuni ilidaiwa Nkoma amejiunga na The Tigers Queens ya Arusha inayoshiriki Ligi Kuu Bara ya Wanawake lakini hata hivyo mwenyewe alikanusha kumalizana na timu hiyo.
Ujio wa Nkoma ndani ya Yanga Princess unaweza kuibadilisha timu hiyo kiuchezaji kwani ni kocha ambaye anapenda soka la pasi, kasi na nguvu.
Pia ni kocha ambaye hana masihara hata kidogo na wachezaji wavivu na huwa ni mwenye misimamo mikali.