Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yapangwa kundi B AFCON Futsal 2026, kuanza Misri

Muktasari:

  • Katika michuano hiyo, Tanzania itazindua kampeni zake kwa kuumana na Misri, mchezo utakaopigwa Oktoba 13 kuanzia saa 1:00 usiku.

Tanzania imepangwa Kundi B pamoja na Misri, Angola na Msumbiji katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika la Futsal 2026, ambazo zimepangwa kufanyika Morocco kuanzia Oktoba 12 hadi 23 mwaka huu.

Katika michuano hiyo, Tanzania itazindua kampeni zake kwa kuumana na Misri, mchezo utakaopigwa Oktoba 13 kuanzia saa 1:00 usiku.

Oktoba 15, Tanzania itacheza mchezo wake wa pili dhidi ya Angola, utakaopigwa saa 4 usiku na kumaliza hatua ya makundi dhidi ya Msumbiji Oktoba 17, saa 4 usiku.

Mchezo dhidi ya Misri utakuwa mtihani wa kwanza kwa Tanzania katika fainali hizo, hasa kutokana na uzoefu wa wapinzani hao ambao wamewahi kutwaa ubingwa wa Afrika mara tatu, mwaka 1996, 2000 na 2004.

Timu mbili zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu katika kila kundi zitaingia hatua ya nusu fainali.

Tanzania, ambayo inashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza, ilikata tiketi ya Morocco baada ya kuibwaga Ivory Coast kwa jumla ya mabao 9-7 katika hatua ya mwisho ya mechi za kufuzu.

Akizungumzia ratiba hiyo jana, kocha wa Tanzania, Curtis Reid, alisema anaamini wataenda Morocco kushindana na si kushiriki.

"Nimeiona ratiba, tumepangwa na timu zenye uzoefu mkubwa ukilinganisha na sisi, lakini kwa maandalizi tunayoendelea kuyafanya, sina shaka tutaenda Morocco kama washindani na si washiriki," alisema Reid.

Alisema anaamini michezo ya kirafiki wanayoendelea kucheza itawajenga kiasi cha kutosha na kuwawezesha kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Tanzania tayari imecheza michezo minne ya kirafiki ya kimataifa kujiandaa na michuano ya Futsal AFCON 2026.

Ilianza kwa kukutana na Zambia jijini Lusaka na kufungwa mabao 6-0 kabla ya kurudiana na kuchapwa mabao 5-0.

Baadaye Tanzania ilisafiri kwenda Misri kwa michezo miwili ya kirafiki dhidi ya wenyeji wao.

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya Misri, uliochezwa Agosti 14, 2026, Tanzania ilipoteza kwa mabao 6-0.

Mchezo wa pili dhidi ya Misri, uliochezwa Agosti 16, 2026, Tanzania ilifungwa kwa mabao 5-0, hivyo katika michezo yake minne ya maandalizi dhidi ya Zambia na Misri, Tanzania ilipoteza kwa mabao 22.

Mataifa nane yamefuzu kushiriki michuano hiyo, ambayo ni wenyeji Morocco, Misri, Algeria, Angola, Libya, Msumbiji, Zambia na Tanzania.