Mrisho Ngassa awatuliza mashabiki huko Jangwani
Muktasari:
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema tangu amejiunga tena na kikosi hicho alikuwa akifanya mazoezi na wachezaji wachache, lakini tangu aingie kambini amegundua Yanga ina kikosi kizuri kitakacholeta ushindani kwa wapinzani wao.
WINGA wa Yanga, Mrisho Ngassa ameupongeza uongozi wake kwa kufanya usajili wa maana, huku akiwatuliza mashabiki wa klabu hjiyo kuwa pamoja na ukata unaowakabili timu hiyo bado itafanya maajabu katika Ligi Kuu Bara 2018-2019.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ngassa alisema tangu amejiunga tena na kikosi hicho alikuwa akifanya mazoezi na wachezaji wachache, lakini tangu aingie kambini amegundua Yanga ina kikosi kizuri kitakacholeta ushindani kwa wapinzani wao.
“Kumekuwa na maneno mengi, eti Yanga haiwezi kufanya vizuri kwa usajili wa kawaida iliyofanya, wacha waendelee kujidanganya ila tupo vizuri na mashabiki wasubiri waone mambo wasitishwe na majina ya timu nyingine,” alisema Ngassa.
Ngassa aliyeichezea Yanga kwa mafanikio kabla ya kutimka mwaka 2015 kwenda Afrika Kusini, alisema timu yao imetawala chipukizi wengi wenye uchu wa mafanikio, hivyo naamini wakishirikiana na wazoefu wataifanya timu iwe tishio.
Aliongeza mpira unachezwa hadharani sio wa kujificha, hivyo hawezi kutumia maneno sana kufikisha ujumbe kwa mashabiki kubwa aliwaomba waachane na matokeo mabaya ya timu yao katika mashindano ya kimataifa huku akiwataka kuwaombea waweze kuwa fiti zaidi kuelekea msimu mpya.
“Mashindano ya kimataifa kwa sasa ni ukamilikaji wa ratiba kwa upande wa timu yangu kwani hata wakishinda michezo yote iliyosalia haifiki popote. wanatakiwa kusahau matokeo ya nyuma tuangalie tunajipangaje kwa msimu mpya,” alisema.