Masihara ya kina Bocco yamchefua Zahera
Muktasari:
- Zahera alisema kilichiofanywa na wachezaji hao hata kama wamesamehewa ni dalili za wazi za kutojitambua kwa wachezaji wengi wa Tanzania na kufichua taratibu wanazofanya kwao mchezaji akichelewa mazoezi ya timu yao ya taifa.
KOCHA Mkuu wa Yanga na msaidizi wa timu ya taifa ya DR Congo, Mwinyi Zahera amesikia taarifa za nyota sita wa Simba na mmoja wa Yanga kuchelewa kambi ya Taifa Stars na kuenguliwa kabla ya kurejeshwa tena na kucheka akidai ni masihara.
Zahera alisema kilichiofanywa na wachezaji hao hata kama wamesamehewa ni dalili za wazi za kutojitambua kwa wachezaji wengi wa Tanzania na kufichua taratibu wanazofanya kwao mchezaji akichelewa mazoezi ya timu yao ya taifa.
Alisema katika timu ya taifa ya Congo mchezaji akichelewa dakika tano ya mazoezi anakatwa Dola 500 na wakizingua klabu zao za Ligi Kuu kwa dakika 10 tu wanakatwa Dola 150 kama njia ya kuwanyoosha.
“Congo wamejiwekea misingi imara ya ushirikiano unaonzia kwa makocha wa klabu na viongozi wao kuhakikisha mchezaji anapotoka kwenye timu yao anakuwa mfano wa kuigwa kwa nidhamu na kiwango chake hasa kwa kupata namba ndani ya kikosi cha kwanza.
“Hivyo mchezaji anapochelewa mazoezini ama anaonyesha utovu wa nidhamu, mimi kocha wa timu ya taifa naandika ripoti yake kwenda kwa viongozi wake wa klabu ambao ndio wanachukua hatua ya kumwajibisha kwa makosa yake, hilo nimeliona limesaidia kwa hali ya juu sana na kila mchezaji anakuwa na hamu ya kuitwa kulitumikia taifa lake, tofauti na Tanzania wanaojivutavuta na kuona wao wapo juu ya taifa, hii ni mbaya.”
Alistajabishwa na kile kilichotokea kwa wachezaji ambao wameanguliwa kwenye mpango wa kikosi cha Kocha Emanuel Amunike, kama wanashindwa kuwa na moyo wa uzalendo na taifa lao ni dhahiri hawaangalii mbali na kujiona wamemaliza kila kitu.
“Asilimia kubwa ya wachezaji wa Tanzania wameshindwa kuishi kwa kuzingatia taaluma yao ya kazi, hasa nimeona kama wanapenda sifa kuliko kuwajibika, Kocha Amunike ni mtu anayejua mpira kwani amecheza katika mataifa yalioendelea, analolifanya liwafunze na wengine, la sivyo wataishia kucheza ligi hiyo hiyo,” alisema.
Pamoja na kuenguliwa kwenye mpango wa Amunike, Zahera aliwashauri wachezaji hao kuiomba radhi nchini yao na kujutia kile ambacho wamekifanya, akisisitiza kinakinzana na kanuni za soka.