Tuwe na msimu bora wa Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Mchezo huo ndiyo unaodhihirisha msimu mpya umeanza na leo katika viwanja viwili vya soka, kuna mechi zinapigwa za mzunguko wa kwanza na KMC itaikaribisha Dodoma, huku Coastal ikianza na Tanzania Prisons, Mkwakwani.
Pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2025/26 lilifunguliwa jana kwa mchezo wa Ngao ya Jamii uliozikutanisha miamba ya soka Yanga na Simba.
Mchezo huo ndiyo unaodhihirisha msimu mpya umeanza na leo katika viwanja viwili vya soka, kuna mechi zinapigwa za mzunguko wa kwanza na KMC itaikaribisha Dodoma, huku Coastal ikianza na Tanzania Prisons, Mkwakwani.
Jumla ya timu 16 inashiriki ligi hii ambayo bingwa mtetezi ni Yanga na msimu huu ina kazi kubwa ya kutetea kwani timu zimejipanga kuipokonya taji hilo inalolishikilia kwa mara ya nne mfululizo.
Ni wazi mashabiki wa soka wamejaa hamasa, matarajio na matumaini ya kushuhudia soka safi, lenye ushindani, nidhamu na burudani ya kweli tofauti na msimu uliopita wa 2024/25 ambao licha ya mafanikio, pia ulikuwa na changamoto kadhaa.
Tunaamini kila timu imejipanga kwa ajili ya msimu huu mpya na hivyo kutakuwa na burudani na usajili zilizofanya zitaifanya kuwa na ligi bora.
Moja ya mambo yaliyolalamikiwa sana msimu uliopita ni kukosekana kwa ushindani wa kweli hasa kwa baadhi ya mechi kuonekana kuwa na viashiria vya upangaji matokeo.
Hili linapaswa kushughulikiwa haraka. Mamlaka husika zihakikishe zinadhibiti upangaji wa mechi, rushwa na aina yoyote ya vitendo vya kihuni vinavyoharibu sura ya mpira wetu.
Timu zinapaswa kujipanga vizuri kiufundi, kifedha na kiusimamizi ili kuwa na vikosi bora vitakavyoshindana kwa haki. Msimu huu uoneshe mabadiliko ya kweli kutoka soka la mazoea hadi kuwa soka la ushindani wa hadhi ya juu.
Waamuzi pia ni sehemu muhimu ya mchezo na msimu uliopita kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu maamuzi yasiyo sahihi ambayo yaliathiri baadhi ya matokeo ya mechi.
TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kuhakikisha waamuzi wote walioteuliwa kusimamia mechi msimu huu wanakuwa katika viwango vya juu vya ufundi, nidhamu na uadilifu.
Maamuzi mabovu yanaua morali ya timu, mashabiki na hata wachezaji, hivyo, waamuzi waendelee kupewa mafunzo ya mara kwa mara na kufanyiwa tathmini kila baada ya mechi.
Ni wazi pia msimu wa 2024/25 ulikumbwa na changamoto za viwanja visivyo na ubora, hali mbaya ya nyasi na miundombinu hafifu.
Ili ligi hii iwe na heshima na kuvutia zaidi, viwanja vinapaswa kuboreshwa kabla ya kila mechi. Pia, ratiba iwe shirikishi na ya wazi, bila upendeleo.
Tunaamini kasoro zilizojitokeza misimu ya nyuma na kuifanya liku kuonekana ina upungufu, hayatajirudia na hivyo msimu huu mpya mipango itaenda kama ilivyowekwa ikiwamo ratiba yenyewe na inapotokea mechi za viporo pia ziangaliwe ili zisisababishe lawama za baadhi ya timu kuchelewa kucheza.