Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, Yanga tembeeni na hasira caf mashabiki

WAKONGWE Pict

Muktasari:

  • Hamasa ya mashabiki ndani na nje ya viwanja ilitoa picha halisi kwamba Simba na Yanga siyo klabu za kawaida, bali ni taasisi kubwa ambazo zinabeba hisia, furaha na majonzi ya mamilioni ya Watanzania.

SIMBA na Yanga zimeshamalizana katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Jumanne, wiki hii ukithibitisha kwa mara nyingine ukubwa na heshima ya klabu hizo mbili kongwe Afrika.

Hamasa ya mashabiki ndani na nje ya viwanja ilitoa picha halisi kwamba Simba na Yanga siyo klabu za kawaida, bali ni taasisi kubwa ambazo zinabeba hisia, furaha na majonzi ya mamilioni ya Watanzania.

Umati wa mashabiki, nyimbo, mabango na ari ya mapenzi yasiyo na kifani vilionyesha wazi thamani ya jezi za timu hizo mbili. Hivyo basi, wachezaji wanaozivaa msimu huu ni lazima watambue kwamba wanabeba mzigo mkubwa wa historia na matarajio, na hawana budi kujipanga ipasavyo kuzipigania kwa nguvu na heshima kubwa.

Ni ukweli usiopingika kuwa msimu huu macho yote ya mashabiki na viongozi wa timu hizo yanaelekezwa kwenye mashindano ya kimataifa yaani Ligi ya Mabingwa Afrika. Hapo ndipo kipimo halisi cha ukubwa wa Simba na Yanga kinapopimwa. Ndiyo maana wachezaji wanapaswa kuongeza ari ya kupambana mara tu baada ya pazia la kufunguliwa kwa ajili ya mashindano hayo.

Ni lazima waelewe kwamba kila mechi ya kimataifa siyo mchezo wa kawaida, bali ni vita ya heshima kwa klabu, mashabiki na taifa kwa ujumla.

Mashabiki nao wanajua fika uzito wa msimu huu. Yanga imetimiza miaka 90 tangu kuanzishwa kwake, na Simba ikiwa na miaka 89. Huu ni umri mkubwa mno, lakini ni historia yenye mapengo makubwa kwa sababu hazina mataji makubwa ya Afrika. Ni aibu na changamoto kubwa kwamba klabu zenye umri huo, zenye wafuasi lukuki na uwekezaji mkubwa bado hazijashinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hivyo basi, wachezaji na viongozi wanapaswa kujitazama kwenye kioo cha historia na kujiuliza; je, timu hizo zitaendelea kubaki na simulizi au wataandika historia mpya kwa kutwaa taji au angalau kufika nusu au fainali msimu huu?

Uchungu na mapenzi ya mashabiki ni wa dhati na kipekee. Kila mara wanajitokeza kwa wingi viwanjani wakiwekeza muda na fedha wakiamini kwamba kila mechi ni fursa ya kuona ndoto zikitimia.

Pia wachezaji na viongozi wanapaswa kujua kwamba mashabiki na wanachama hawatakubali kuona mizaha, uzembe au dharau zikijitokeza ndani ya viwanja hasa katika mashindano ya kimataifa. Ni wajibu wa wachezaji na mabenchi ya ufundi kuhakikisha wanajitoa kwa mioyo ya dhati, nidhamu ya hali ya juu na kupambana kwa viwango vya juu kama ilivyo timu za Kiarabu za Afrika Kaskazini.

Timu za Kiarabu hazirembi linapokuja suala la ubingwa; zinapambana, hupiga hesabu na kuwekeza nguvu zote. Huo ndiyo mfano wa kuigwa. Historia ya Tanzania na Afrika inasubiri Simba na Yanga kuandika ukurasa mpya. Mashindano hayo ni zaidi ya michezo ya dakika 90.

Ni fursa ya kuonyesha ukubwa wa soka la Tanzania na nafasi ya kuacha alama itakayodumu vizazi na vizazi.  Wachezaji wakipambana kwa dhati, wakishirikiana na mashabiki hakuna kinachoshindikana. Wakifanya vyema, hakika majina yao yataandikwa kwenye mioyo ya mashabiki wa soka wa Tanzania na historia ya Afrika itawahesabu kama mashujaa wa kweli wa mchezo huu pendwa kupitia timu hizo za Tanzania.