Iwe dabi ya heshima, soka na ubora
Muktasari:
- Mchezo huo wa ufunguzi wa msimu ukiwa ni wa Ngao ya Jamii unatarajiwa kuwa na hadhi na mvuto wa ligi.
LEO ndio mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuwa na mvuto wa kipekee kwa wapenzi wa soka nchini.
Mchezo huo wa ufunguzi wa msimu ukiwa ni wa Ngao ya Jamii unatarajiwa kuwa na hadhi na mvuto wa ligi.
Kwa mara nyingine, Simba na Yanga, timu mbili zenye historia ndefu ya ushindani zitakutana kuonyesha soka lenye hadhi, ubora na heshima.
Huo ni wakati wa kuonyesha kuwa soka la Tanzania linaweza kuchezwa kwa kiwango cha juu, huku wachezaji na mashabiki wakizingatia heshima kama msingi wa ushindani.
Ni muhimu kwa pande zote mbili kuzingatia kwamba dabi hii sio tu kuhusu ushindi wa timu, bali ni fursa ya kutoa picha kamili ya namna soka linavyopaswa kuchezwa.
Hapa, hakuna vurugu, kejeli, au misukumo isiyo ya heshima. Wachezaji wa Simba na Yanga wanapaswa kuonyesha kuwa ushindani unaweza kuwa na nidhamu na umahiri huku wapenzi wa soka wakishuhudia ubora na utamu wa soka.
Lengo ni kuonyesha ushindani unaoonekana ambao unavutia, unasisimua na wakati huohuo unaenzi maadili ya mchezo.
Mbali na heshima, mchezo huu ni fursa kwa timu zote mbili kujipanga vyema kwa ajili ya mashindano ya mwaka huu, si tu ya ndani bali pia ya kimataifa.
Simba na Yanga zinapaswa kutumia mchezo huo kama kielelezo cha maandalizi ya kimkakati kujipanga kimbinu, kuimarisha umoja na kuhakikisha wachezaji wanakuwa katika hali bora ya ushindani.
Ubora wa mchezo huo utakaoonyeshwa kupitia uchezaji kiufundi na kasi ndio utakaoonyesha ni kwa namna gani timu zimejipanga vyema kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Mashabiki wanapaswa kuangalia mchezo huo si kwa kuangalia tu timu gani itashinda, bali jinsi timu zinavyocheza soka la ushindani zikionyesha mfano wa kiwango cha soka kinachotarajiwa na mashabiki katika soka la kimataifa.
Ubora wa wachezaji, mbinu za makocha, uelewa wa mchezo na jinsi wanavyoshirikiana katika uwanja ndizo alama zinazopaswa kuzingatiwa kabla ya safari ya mashindano msimu huu.
Hii itawawezesha mashabiki kuanza kuhesabu mafanikio na kuujua ubora wa timu ambazo zitakuwa na kazi ya kupeperusha bendera ya nchi Afrika.
Dabi hii ni zaidi ya ushindi wa mchezo mmoja. Ni onyesho la utamaduni wa soka la Kitanzania, fursa ya kuimarisha hadhi ya ligi na msingi wa mashindano mazuri yanayofuata.
Simba na Yanga zinapaswa kuingia uwanjani zikiwa na lengo la kuonyesha heshima, kushindana kwa kiwango cha juu na kutoa picha halisi ya soka la Tanzania namna linavyokua.
Wachezaji, makocha na mashabiki wanapaswa kushirikiana kuhakikisha kuwa mchezo huo unakuwa mfano wa namna ambavyo Ligi Kuu Bara inavyotakiwa kuendelezwa.
Kwa hiyo, wachezaji wa Simba na Yanga wacheze mchezokwa umakini na nidhamu, wakionyeshana ushindani huku wakijiandalia ubora kuelekea mashindano ya kimataifa.
Ubora wa soka watakaouonyesha katika mchezo huo ndiyo msingi wa mashabiki kuuzingatia, kuhakikisha kuwa safari ya msimu huu inaanza kwa nguvu, nidhamu na heshima inayostahili Ligi Kuu Bara.