Zilizobamba 2025… Ulikuwa mwaka wa Yanga SC
Muktasari:
- Yanga ambayo ni bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara ikibeba taji hilo mara 31, imekuwa na wakati mzuri zaidi kwa mwaka 2025 uliobakisha siku chache kabla ya kumalizika.
MWAKA 2025, utaendelea kuwa wa kukumbukwa na mashabiki wa Yanga SC kutokana na timu hiyo kufanya vizuri zaidi kuliko timu yoyote ya Tanzania.
Yanga ambayo ni bingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara ikibeba taji hilo mara 31, imekuwa na wakati mzuri zaidi kwa mwaka 2025 uliobakisha siku chache kabla ya kumalizika.
Wakati tukihesabu siku kuumaliza mwaka 2025, Yanga imefunga hesabu tayari kwa rekodi mbalimbali kuanzia kwa wachezaji, klabu na uongozi.
HAIJAPOTEZA MECHI ZA NDANI
Kuanzia Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, Kombe la Muungano na Ngao ya Jamii, Yanga imebakia kuwa timu pekee ya Tanzania isiyopoteza mechi yotote katika mashindano hayo kwa mwaka 2025.
Katika Ligi Kuu Bara, Yanga imecheza mechi 21, imeshinda 19 na sare mbili. Haijapoteza ndani ya mwaka 2025.
Matokeo ya mechi hizo ni; Yanga 4-0 Kagera (Februari 1), Yanga 6-1 KenGold (Februari 5), JKT Tanzania 0-0 Yanga (Februari 10), KMC 1-6 Yanga (Februari 14), Yanga 2-1 Singida Black Stars (Februari 17), Mashujaa 0-5 Yanga (Februari 23), Pamba Jiji 0-3 Yanga (Februari 28), Tabora United 0-3 Yanga (Aprili 2), Yanga 1-0 Coastal (Aprili 7), Azam 1-2 Yanga (Aprili 10), Fountain Gate 0-4 Yanga (Aprili 21), Yanga 3-0 Namungo (Mei 13), Tanzania Prisons 0-5 Yanga (Juni 18), Yanga 5-0 Dodoma Jiji (Juni 22), Yanga 2-0 Simba (Juni 25), Yanga 3-0 Pamba Jiji (Septemba 24), Mbeya City 0-0 Yanga (Septemba 30), Yanga 2-0 Mtibwa (Oktoba 28), Yanga 4-1 KMC (Novemba 9), Yanga 2-0 Fountain Gate (Desemba 4) na Coastal 0-1 Yanga (Desemba 7).
Kwa upande wa Kombe la Muungano lililofanyika kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba kuanzia Aprili 24 hadi Mei Mosi, Yanga ilicheza mechi tatu, ikianzia robo fainali na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ, ikatoka 1-1 na Zimamoto na kushinda kwa penalti 3-1 hatua ya nusu fainali, kisha fainali ikaichapa JKU 1-0.
Katika Kombe la FA, Yanga ilianzia hatua ya 64 bora, ikatembeza vichapo hadi fainali na kubeba ubingwa kwa msimu wa nne mfululizo ikicheza mechi sita na kushinda zote ndani ya muda wa kawaida.
Yanga ilianza kwa kuichapa Copco mabao 5-0 (Januari 25), kisha Coastal Union ikalambwa 3-1 (Machi 12), Songea United ilifungwa 2-0 (Machi 29), Stand United ilipigwa 8-1 (Aprili 15), JKT Tanzania ilifungwa 2-0 (Mei 18) na Singida Black Stars ikapigika 2-0 (Juni 29).
Ukija upande wa Ngao ya Jamii, Yanga ikaichapa Simba bao 1-0, ilikuwa Septemba 16.
Kwa ujumla, katika mashindano yote ya ndani, kwa mwaka 2025, Yanga imecheza mechi 30, imeshinda 28 na sare mbili. Haijaonja ladha ya kipigo.
YABEBA MATAJI YOTE
Kutokana na mwenendo mzuri, Yanga imeufunga mwaka 2025 kwa kuweka kabatini mataji manne ya ndani iliyoshiriki.
Taji la kwanza Yanga kubeba mwaka 2025 ni Kombe la Muungano ilipoichapa JKU bao 1-0 katika fainali iliyochezwa Mei Mosi kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
Taji la pili lilikuwa Ligi Kuu Bara ikimaliza ligi kwa kukusanya pointi 82 baada ya kucheza jumla ya mechi 30. Kumbuka ligi msimu wa 2024-2025 ilitamatika Juni 25 ambapo Yanga iliichapa Simba mabao 2-0 katika mechi ya mwisho iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar na kukabidhiwa kombe ikiwa ni msimu wa nne mfululizo inabeba taji hilo ambalo ni la 31 kwa jumla tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965. Inafuatiwa na Simba iliyolitwaa mara 22.
Kisha Yanga ikaenda kubeba Kombe la FA, ikiichapa Singida Black Stars mabao 2-0, fainali iliyochezwa Juni 29, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja.
Taji la nne ni Ngao ya Jamii katika kufungua msimu huu wa 2025-2026, mechi ikichezwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga ikaifunga Simba bao 1-0.
Katika mataji hayo manne ya Yanga, mawili ambayo ni Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii imekabidhiwa mbele ya watani wao wa jadi, Simba.
MAKUNDI CAF MARA NNE MFULULIZO
Yanga imeendelea kuweka mizizi katika mashindano ya CAF ambapo sasa ipo hatua ya makundi upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kufuzu kwa Yanga hatua ya makundi msimu huu, imekuwa ni mara ya nne mfululizo baada ya 2022-2023 (Kombe la Shirikisho), kisha 2023-2024, 2024-2025 na 2025-2026 zote ikiwa Ligi ya Mabingwa.
Kabla ya hapo, Yanga haikuwahi kufanya hivyo mfululizo, imeweka rekodi mpya inayoweza kudumu kwa muda mrefu.
MAKOCHA WATANO WAMEPITA
Wakati Yanga ikipata mafanikio hayo kwa mwaka 2025, makocha watano tofauti wameifundisha timu hiyo kwa nyakati tofauti.
Alianza Sead Ramovic ambaye alitoka na timu mwishoni mwa mwaka 2024, aliposepa Februari, timu ikaongozwa na Abdihamid Moalin kwa mechi moja, kisha Miloud Hamdi akaja kumalizia msimu.
Ulipoanza msimu wa 2025-2026, Romain Folz akaiongoza Yanga, hata hivyo hakudumu sana, akaja Pedro Goncalves ambaye yupo hadi sasa akielekea kuufunga mwaka huku timu hiyo ikiwa haina tena mechi nyingine ya mashindano hadi Januari 23, 2026.
Kati ya makocha hao, Hamdi ndiye amefanikiwa zaidi akibeba mataji matatu ambayo ni Kombe la Muungano, Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Folz amebeba Ngao ya Jamii.
MZIZE NA TUZO YA BAO LA CAF
Novemba 19, 2025, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize alitwaa Tuzo ya Bao Bora la Mwaka la CAF 2025 katika hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) iliyofanyika Rabat, Morocco.
Mzize alitwaa tuzo hiyo kutokana na bao alilofunga msimu wa 2024-2025 hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe wakati Yanga ikishinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Januari 4, 2025.
Katika kinyang'anyiro hicho, Mzize alikuwa anashindana na wenzake 12, lakini kura zilizopigwa na mashabiki, zikampa ushindi huo.
Katika mchakato wa kulisaka bao bora, CAF ilitangaza wachezaji 13 walioteuliwa kuwania tuzo hiyo ambapo mashabiki wakapewa nafasi ya kuchagua mshindi.
Orodha hiyo iliandaliwa na Kamati Maalum ya Ufundi ya CAF ambapo kura zilianza kupigwa Alhamisi, Novemba 6, 2025 na kufungwa Jumatano, Novemba 12, 2025.
Kwa mujibu wa CAF, kura za mashabiki zinachangia asilimia 100 ya matokeo ya mwisho.
Mzize aliibuka mshindi mbele ya Abdellah Ouazane (Morocco vs Tanzania-AFCONU17), Anas Roshdy (Misri vs Afrika Kusini -AFCONU17), Asharaf Tapsoba (Burkina Faso vs Cameroon-AFCONU17), Barbra Banda (Zambia vs Morocco-WAFCON2024).
Wengine ni Calvin Fely (Madagascar vs Morocco-CHAN2024), Ghizlane Chebbak (Morocco vs Nigeria-WAFCON2024), Ibrahim Adel (Pyramids vs ES Tunis-Ligi ya Mabingwa), Jean-Claude Girumugisha (Al Hilal SC vs MC Alger-Ligi ya Mabingwa).
Pia kuna Ndabayithethwa Ndlondlo (Afrika Kusini vs Uganda-CHAN2024), Oussama Lamlioui (Morocco vs Madagascar-CHAN2024), Refiloe Jane (Afrika Kusini vs Mali-WAFCON2024) na Soufiane Bayazid (Algeria vs Uganda-CHAN2024).
REKODI YA MAUZO YA AZIZ KI
Katika vitabu vya kumbukumbu, nyota kutoka Ligi Kuu Tanzania Bara aliyeuzwa kwa fedha nyingi zaidi hadi sasa anabaki kuwa Stephane Aziz KI ambaye amejiunga na Wydad Athletic mwisho mwa msimu wa 2024-2025 akitokea Yanga ikielezwa dau lilifika Sh2.9 bilioni.
Kiasi hicho cha fedha kimetokana na Sh2 bilioni za kununua mkataba wa mwaka mmoja uliobaki na Sh965 milioni za dau la usajili, ukijumlisha unapata jumla mauzo ya Aziz KI yanafika Sh2.9 bilioni.
Mauzo hayo yameweka rekodi katika soka la Tanzania ambapo nyota huyo ametokea Yanga.
Kabla ya Aziz KI, Yanga pia ilimuuza straika wake raia wa DR Congo, Fiston Mayele aliyekwenda Pyramids ya Misri mwaka 2023 kwa ada ya uhamisho ambayo haikutajwa hadharani lakini inasemekana kuwa ni dola 900,000 (sawa na Sh2.3 bilioni).
HERSI AULA FIFA
Oktoba 2025, Rais wa Yanga, Hersi Said aliteuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Klabu za Soka za Wanaume Duniani.
Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Klabu za Soka Afrika (ACA), uteuzi huo ndani ya FIFA utadumu kwa muda wa miaka minne kuanzia 2025 hadi 2029.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa FIFA, Gianni Infantino na kupitishwa na Baraza la Shirikisho hilo.