Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZAKARIA: Kitasa kipya Singida BS kisichoisahau Simba

ZAKARIA Pict

Muktasari:

  • Beki huyo ambaye tayari amewaaga viongozi, wachezaji na benchi la ufundi la Mashujaa FC aliyokuwa anaitumikia akitokea Namungo, inaelezwa tayari amemalizana na Singida Black Stars ambapo atakuwa akipambania namba na Anthony Tra Bi Tra pamoja na Morice Chukwu.

NI suala la muda tu kwa beki wa kati Abdulmalik Zakaria kuvaa uzi wa njano na nyeusi baada ya jina lake kutajwa kujiunga na Singida Black Stars kwenye dirisha dogo la usajili la Januari.

Beki huyo ambaye tayari amewaaga viongozi, wachezaji na benchi la ufundi la Mashujaa FC aliyokuwa anaitumikia akitokea Namungo, inaelezwa tayari amemalizana na Singida Black Stars ambapo atakuwa akipambania namba na Anthony Tra Bi Tra pamoja na Morice Chukwu.

Zakaria ambaye ni miongoni mwa mabeki wazawa wanaofanya vizuri Ligi Kuu Bara, ameendelea kuvutia macho ya wadau wa soka kutokana na uimara, uwezo wa kusoma mchezo na kuongoza safu ya ulinzo licha ya ushindani mkubwa uliopo nafasi hiyo.

Ubora huo ndio uliomfanya kuitwa katika timu ya taifa ya Tanzania, hatua inayoonyesha namna anavyoaminiwa na benchi la ufundi, ingawa hadi sasa hajapata nafasi ya kushuka uwanjani. Hata hivyo, uwepo wake kambini unaelezwa kuwa sehemu ya mchakato wa kumjenga na kumpa uzoefu wa kimataifa chini ya kocha Miguel Gamondi ambaye pia ni kocha wa Singida Black Stars.

Mwanaspoti limezungumza mambo mbalimbali na beki huyo ikiwa ni pamoja na kuwataja nyota wa Yanga wanaocheza safu ya ulinzi kuwa wamejitengenezea ufalme katika ligi na Taifa Stars.

ZAKA 05

BACCA, JOB UKUTA WA CHUMA

Kuna mabeki wengi wa kati wazawa wanaofanya vizuri licha ya uwepo wa nyota wa kigeni katika nafasi hiyo, lakini Zakaria anawataja Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ kuwa wana ufalme wao katika eneo hilo.

“Kuna mabeki wengi wanafanya vizuri hasa wa ndani. Kwa upande wa nyota wa kigeni sioni tishio lolote kwani wana uwezo wa kawaida tofauti na nyota wa ndani. Sababu (wa ndani)ni kutoaminiwa tu.

“Bacca na Job wamepewa nafasi na kuaminiwa, wameonyesha uwezo mkubwa na hakuna anayewatilia shaka kuanzia Ligi Kuu hadi timu ya taifa. Wao ndio viongozi imara wa kikosi cha kwanza cha ligi na taifa.”

Zakaria anasema ukiondoa mabeki hao ambao tayari wamethibitisha uwezo wakicheza timu kubwa, anavutiwa pia na uwezo wa Ibrahim Ame, Abdallah Kher ‘Sebo’ na Laurian Omar Makame kuwa ni mabeki wazuri wenye uwezo mkubwa wa kiaminiwa na kupewa nafasi ya kuonyesha walicho nacho.

“Tanzania ukiondoa nafasi ya viungo, basi hata eneo la mabeki kuna wachezaji wengi bora wenye uwezo mkubwa wa kufanya kitu kikubwa eneo hilo tofauti na nyota wengi wa kigeni wanaoletwa kwenye nafasi hii.”


ZAKA 04

MORRIS ALIMVUTA

Kila mchezaji ana mtu aliyemvutia alipokuwa anaanza kucheza soka hasa la ushindani, aliyekuwa akimtazama kama kiongozi wake kutokana na kumtangulia kuanza kucheza, kama anavyosema Zakaria kuwa alivutwa kwenye soka na aliyekuwa staa wa Azam, Aggrey Morris.

“Mpira ni mchezo ambao nilikuwa naupenda tangu nikiwa na umri mdogo. Nafikiri nimezaliwa ili nicheze na katika kujifunza kwangu nilikuwa nikimtazama zaidi Morris. Nakiri kuwa ndiye aliyenifanya nipambane zaidi,” anasema.

“Ni sehemu ya mabeki wengi bora waliocheza vyema na kutupa darasa kwenye eneo hili kipindi hicho wanacheza mpira, nilikuwa nikimtazama kwa kujifunza mengi kutoka kwake, najivunia ubora wake umenifikisha hapa.”

Zakaria anasema aliwahi kuzungumza na Morris na kumuambia kuwa anavutiwa na ubora wake, jambo ambalo lilikuwa mwanzo wao kuzungumza zaidi ambapo mkongwe huyo alianza kumfuatilia na kumpa njia za kupita awe bora kama yeye.


ZAKA 03

HAKUNA KAMA MAYELE

Mabeki wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi kutoka kwa washambuliaji wa timu pinzani katika harakati za kulinda ukuta wa timu zao kwa kushirikiana na makipa wao, kama anavyofunguka Zakaria akimtaja Fiston Mayele kuwa ni miongoni mwa washambuliaji bora na wagumu aliowahi kukutana nao.

“Kazi yangu ni kuzuia mashambulizi yanayoelekezwa langoni kwetu, ni kweli ligi ina washambuliaji wengi bora na washindani, nimefanikiwa kuwazuia na kumudu mbinu zao, lakini kulikuwa na mwamba, Mayele ni mshambuliaji tishio kuwahi kutokea.

“Ni mshambuliaji ambaye haikuwa rahisi kukabana naye tulipokuwa tunakutana, nakiri kuwa ni mshambuliaji aliyekuwa akinipa wakati mgumu sana uwanjani, ni daraja kubwa lililowahi kucheza ligi yetu.”

Zakaria anasema washambuliaji wengi wa kigeni wamepita katika Ligi Kuu Bara, lakini upande wake anamtaja Mayele kuwa mshambuliaji aliyekamilika kwa kasi, nguvu na akili ya mpira.


ZAKA 02

AITAJA SIMBA

Beki huyo ambaye hadi sasa amecheza timu nane tangu aanze kujihusisha na soka la ushindani, anasema amecheza mechi nyingi za ushindani, lakini hataweza kusahau mechi dhidi ya Simba iliyomalizika kwa Mashujaa kuchapwa mabao 2-1.

“Nimecheza mechi nyingi ngumu na za ushindani, lakini mechi yangu bora ilikuwa dhidi ya Simba msimu huu. Ilikuwa mechi bora sana. Upinzani ulikuwa mkubwa kila timu ilitaka matokeo. Simba walitumia makosa yetu kutuadhibu lakini haikuwa rahisi,” anasema.

“Hatukuwa wanyonge kwenye mchezo huo tulipambana kuhakikisha tunapata matokeo lakini bahati haikuwa upande wetu, tulikosa matokeo lakini tulikuwa na mchezo bora.”


ZAKA 01

MTUWI NI SOKA, UONGOZI

Unahodha ni wito na ni uongozi kama anavyodai Zakaria akimtaja aliyekuwa nahodha wake Mashujaa, Baraka Mtuwi kuwa ni mchezaji kiongozi anayestahili kuvaa kitambaa.

“Nimecheza na wachezaji wengi bora nikiwa kwenye timu mbalimbali nilizozitumikia ikiwa ni pamoja na Mafunzo, Polisi Tanzania, Namungo na Mashujaa ninaukubali uwezo wa Mtuwi. Ni mchezaji mzuri anayejiamini na ni kiongozi uwanjani.” anasema.

“Ukicheza na mchezaji kiongozi uwanjani mnaelekezana na mnakuwa na nafasi kubwa ya kupata matokeo au kuambulia hata sare, kwani kuzungumza kunasaidia kupunguza makosa na kujipanga kuzuia mashambulizi, ndio kitu anachokifanya Mtuwi uwanjani.” 

Zakaria anasema Mtuwi anastahili kuvaa kitambaa cha unahodha kwani mbali na maelekezo uwanjani ni mchezaji anayetoa ushirikiano mzuri kwa wenzake kunapokuwa na changamoto.