Yanga Princess ikikomaa inabeba!
Muktasari:
- Mafanikio makubwa kwa Yanga ni kubeba Kombe la Samia Cup nje na hapo haikuwahi kunyanyua makwapa zaidi ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2021/22 ikiwa chini ya Kocha Edna Lema ‘Mourinho’.
TANGU Yanga Princess ianze kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (WPL) mwaka 2018 haijawahi kuchukua ubingwa na hilo limewafanya baadhi ya mashabiki wa wananchi hao kuwa na hamu kweli kweli hususani wakiona taji hilo la wanawake likienda kwa wapinzani Simba Queens na JKT Queens ambao wote wamebeba mara nne.
Mafanikio makubwa kwa Yanga ni kubeba Kombe la Samia Cup nje na hapo haikuwahi kunyanyua makwapa zaidi ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2021/22 ikiwa chini ya Kocha Edna Lema ‘Mourinho’.
Lakini licha ya kutobeba kombe hilo, hivi karibuni wamekuwa wakipiga hatua, wakijenga timu imara pamoja na kuongeza ushindani. Hapo awali ilionekana kama timu ya kujifunza, lakini sasa imekua na kuwa miongoni mwa vigogo wanaotajwa kwenye mbio za ubingwa. Swali ni je, msimu huu wataweza kufanikisha hitaji la misimu nane?
IMEANZA FRESHI
Baada ya mzunguko wa kwanza, Yanga Princess ipo nafasi ya pili ikiwa na tofauti ya pointi moja tu dhidi ya vinara Simba Queens yenye 31, lakini wakitofautiana pointi 10 na JKT iliyopo nafasi ya tatu yenye 20.
Tofauti ya pointi moja na Simba katika ligi yenye ushindani mkali siyo pengo kubwa, ni mechi moja tu. Hii ina maana mbio bado ziko wazi.
Yanga imeonyesha kiwango kizuri, hasa kwenye mechi ngumu. Imekuwa ikikusanya pointi tatu hata pale na kiuchezaji haikuwa vizuri, jambo linaloonyesha ukomavu wa kiushindani, mfano mechi na Fountain Gate Princess ugenini, dakika 90 zilimazika kwa ushindi wa mabao 5-4.
Ilionyesha kiwango kikubwa licha ya Fountain kuipa chalenji ambayo iliamuliwa na mshambuliaji Jeaninne Mukandayisenga dakika za jioni na kuwafanya wananchi hao wamalize kifua mbele.
DHIDI YA MTETEZI
Moja ya matokeo yaliyotikisa mzunguko wa kwanza ni ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi JKT Queens. Huu haukuwa ushindi wa kawaida. Uliwapa pointi tatu muhimu na imani yeyote wanaweza kumwangusha.
Katika mechi hiyo, Yanga Princess ilionyesha nidhamu ya hali ya juu ya kukaba, mkakati na ufanisi mbele ya lango. Tofauti na misimu iliyopita ilikuwa ikikosa umakini kwenye mechi kubwa, safari hii ilionekana kuwa tayari kiakili na kimchezo.
Tangu zianze kukutana msimu wa 2018/19 hii ilikuwa mara ya kwanza kwenye ligi Yanga kuifunga JKT, awali iliambulia vichapo na sare tu.
Hivyo kumaliza mzunguko wa kwanza ikichukua pointi tatu mbele ya bingwa mtetezi siyo jambo rahisi lakini imewaongezea kujiamini zaidi.
USAJILI BORA
Moja ya sababu kubwa inayowafanya waonekane tishio ni usajili walioufanya kabla ya msimu kuanza. Iliongeza wachezaji wenye uzoefu na ushindani, wakiwemo watatu kutoka kwa watani zao, Simba. Kwa misimu miwili mfululizo Yanga imekuwa bora kwenye usajili tangu Edna Lema arejeshwe msimu uliopita na sasa ina kikosi kipana kuanzia golini na mbali na kipa namba moja, Ritha Akarekor, Zubeda Mgunda amekuwa akipata nafasi na kuonyesha kiwango cha kuisaidia timu.
Pia eneo la beki, timu hiyo imesajili mabeki wenye viwango vinavyoendana na haitegemei mchezaji mmoja au wawili.
Ikilinganishwa na misimu mitatu nyuma, Yanga Princess inaonekana kuwa na beki imara, kiungo kinachoweza kumiliki mpira na kudhibiti kasi ya mechi na mshambuliaji mwenye ufanisi mbele ya lango.
Hadi sasa mshambuliaji wake, Mukandayisenga anaongoza kwenye upachikaji mabao akiwa na 15, lakini hata msimu uliopita alikuwa na rekodi nzuri alipoingia dirisha dogo na kumaliza na mabao 13.
Tangu mwaka 2018, Yanga Princess imekuwa ikijenga misingi. Lakini mara nyingi ilishindwa kuuendeleza hasa inapocheza mechi za kuamua kwani hupoteza pointi kirahisi dhidi ya vigogo wenzao.
Msimu huu kuna dalili tatu za mabadiliko. Ukomavu wa kiakili wanacheza kwa kujiamini hata wakiwa ugenini, wanapata matokeo hata siku ambazo hawachezi vizuri sana.
Lakini njaa ya mafanikio wachezaji wanaonekana kuwa na hamasa ya kuandika historia na kama wataendeleza inaweza kuwa na manufaa makubwa kwao.
WASIKIE WENYEWE
Mratibu wa Yanga, Kibwana Matokeo anasema “Msimu uliopita tulijiwekea malengo ya kutengeneza timu huku tukileta ushindani lakini huu, malengo ni kupambana na kuhakikisha tunanyakua ubingwa.”