Prime
Tshabalala alivyojitofautisha na mastaa wengine Yanga
YANGA imefunika kwa misimu minne mfululizo ikiwa na kikosi bora cha ushindani kilichowapa wapinzani shida ya kupenya kubeba ubingwa wa michuano ya ndani, kwani katika muda wote imebeba taji la Ligi Kuu na Kombe la Kombe la Shirikisho (FA).
Ubora wa kikosi chao ulikuwa mwiba kwa wapinzani ikiwaweka matatani hadi watani wao Simba waliowafumua mara sita mfululizo katika michuano mbalimbali ikiwamo ya Ligi Kuu na Ngao ya Jamii.
Ubora wa misimu minne umeonekana kutingishika msimu huu baada ya nyota kadhaa kuondoka na maingizo mapya kushindwa kupenya katika kikosi cha kwanza.
Jambo hilo limei- sukuma Yanga kutaka kulitumia vyema dirisha dogo la usajili lililo wazi hadi Januari 30, kujaribu kuipa uthabiti timu.
Klabu nyingi hutumia dirisha dogo kama sehemu ya marekebisho ya haraka, lakini safari hii linaonekana kuwa zaidi ya hilo upande wa Yanga. Ni dirisha la kuokoa msimu, kurejesha ushindani wa ndani na kulinda malengo ya mataji ya ndani pamoja na heshima ya klabu katika michuano ya kimataifa.
Dirisha kubwa la usajili lilianza kwa matumaini makubwa baada ya Yanga kuachana na baadhi ya wachezaji na kuleta sura mpya zilizobebwa na wasifu mzito na bora kuzidi waliotoka.
Mashabiki walitarajia kuona kikosi kipya chenye nguvu zaidi, kasi zaidi na ubora wa juu unaolingana na changamoto za Ligi Kuu na michuano ya CAF. Hata hivyo, uhalisia wa uwanjani umekuwa tofauti na matarajio ya awali.
Yanga ilimalizana na Khalid Aucho ambaye alikuwa mhimili mkubwa katika eneo la kiungo kwa misimu minne mfululizo na kumshusha Moussa Bala Conte kutoka CS Sfaxien ya Tunisia ambaye, hata hivyo, hajaonyesha makali yopyote na kujikuta akisugua benchi kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo.
Licha ya kusajili wachezaji kadhaa wa kigeni na wa ndani, mchango wa papo kwa papo umekuwa mdogo. Katika tathmini ya wazi, usajili pekee uliotoa thamani ya moja kwa moja ni wa Mohammed Hussein “Tshabalala” kutoka Simba.
Tshabalala aliingia kikosini bila kelele, lakini akajenga heshima yake kupitia kiwango cha juu, nidhamu ya kazi na uelewa wa mechi kubwa.
Tshabalala anaonyesha kile ambacho Yanga ilikikosa kwa usajili mwingine, yaani mchezaji aliyekomaa, anayeijua ligi, anayefahamu presha ya klabu kubwa na asiyehitaji muda mrefu kuzoea. Hilo lilimfanya awe chaguo la uhakika kwa benchi la ufundi tangu mwanzo.
Kinyume chake, wachezaji waliokuja na majina makubwa na wasifu wa kuvutia wameshindwa kuakisi thamani hiyo uwanjani.
Mohammed Dombia, aliyesajiliwa kama kiungo mwenye uwezo wa kukaa na mali mguuni na kuunganisha timu, ameshindwa kuleta uthabiti unaotarajiwa kwenye eneo la kiungo tofauti na ilivyokuwa kwa Stephane Aziz Ki ambaye aliuzwa Wyadad. Kasi ya mchezo wa Ligi Kuu na presha ya ushindani imemzidi mara kadhaa.
Conte aliyeletwa kama suluhisho kwenye eneo la ukabaji, akiwa na sifa za kasi na uwezo wa kushambulia, ameshindwa kuendana na mfumo wa timu, akipata nafasi chache na pale anapocheza kushindwa kuacha alama ya kudumu.
Celestin Ecua, ambaye usajili wake ulisifiwa kama uwekezaji mkubwa kwenye safu ya ushambuliaji akitoka kushinda tuzo ya MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, naye ameshindwa kuonyesha tofauti kubwa inayotarajiwa kwa mchezaji wa kigeni katika klabu inayolenga ubingwa. Kukosa mabao ya uhakika na mchango mdogo kwenye kupandisha mashambulizi vimemfanya apoteze nafasi ya kuaminika.
Mbali na hao, kuna kundi la wachezaji wengine waliotambulishwa kwa mbwembwe, lakini wamejikuta wakikaa benchini kwa muda mrefu au kutopata nafasi kabisa.
Hali hii imezua maswali kuhusu usajili wao na kama waliletwa kwa kuzingatia mahitaji ya kiufundi au kwa uamuzi ya nje ya benchi la ufundi.
Changamoto nyingine kubwa iliyochangia kuyumba kwa usajili ni mabadiliko ya makocha. Yanga ilianza msimu ikiwa na kocha Romain Folz aliyekuwa na falsafa na mfumo wake, lakini mabadiliko ya benchi la ufundi yaliyoshuhudiwa Mfaransa huyo akiondoka baada ya kuwa madarakani kwa miwezi miwili tu na nafasi yake kuchukuliwa na Pedro Goncalves, raia wa Ureno, yamebadilisha kabisa mwelekeo wa matumizi ya wachezaji.
Baadhi ya wachezaji waliosajiliwa walikuwa wanaendana na mfumo wa kocha wa awali, lakini walijikuta hawana nafasi chini ya kocha mpya. Hili liliathiri moja kwa moja matumizi ya kikosi, uthabiti wa timu na kuua morali ya baadhi ya wachezaji.
Mipishano ya kiufundi ilionekana wazi pale wachezaji walipoanza kutumika nje ya nafasi zao au kubadilishwa mara kwa mara bila kupata mwendelezo. Kikosi kilionekana kana kwamba bado kinatafuta utambulisho wake katikati ya msimu.
Matokeo yake, Yanga imeendelea kubebwa zaidi na wachezaji wa msimu uliopita badala ya usajili mpya. Ushindani wa ndani umepungua, benchi limekuwa dhaifu na chaguo mbadala kwenye mechi ngumu limekuwa finyu.
Hali hii imeathiri pia uimara wa timu kwenye mechi kubwa, ambapo tofauti ndogo tu ya ubora imekuwa ikiamua matokeo. Yanga imeonekana kukosa wachezaji wa “kubadilisha mchezo” wanapoingia kutoka benchini.
Ndio maana dirisha dogo la usajili linakuja kama fursa ya mwisho ya kusahihisha makosa. Hili si dirisha la kuongeza idadi ya wachezaji, bali ni dirisha la kuongeza ubora.
Kutokana na hali hiyo hivi karibuni yameibuka maneno mengi kwamba Yanga kwa asilimia kubwa inatarajia kuachana na nyota wao waliosajiliwa dirisha kubwa kwa kuwatoa kwa mkopo na kufanya maingizo mapya ili kuirudisha timu hiyo kwenye ushindani.
Conte, Doumbia wanatajwa kuwa huenda wakapelekwa kwa mkopo Singida Big Stars. Hii inajenga picha kwamba pengine hawakufanya usajili sahihi wa kuendeleza ushindani wao kwa miaka minne mfululizo, lakini pia Ecua inatajwa kuwa pia anatafutiwa timu ya kupelekwa kwa mkopo.
Yanga inapaswa kuanza kwa kufanya tathmini ya kweli ya nani anaendana na mfumo wa kocha wa sasa na nani hapaswi kuendelea. Kuendelea kubeba wachezaji wasiotumika ni mzigo wa kifedha na wa kiufundi.
Pili, usajili wa dirisha dogo unapaswa kulenga wachezaji waliokomaa, wanaoijua ligi au mazingira ya Afrika, hata kama ni wachache. Wachezaji wawili au watatu bora wanaweza kuleta tofauti kubwa kuliko wachezaji sita wa majaribio.
Tatu, klabu inahitaji kuimarisha maeneo yenye upungufu wa wazi, hasa kiungo mshambuliaji mwenye ubunifu na mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumia nafasi chache kufunga mabao tofauti na sasa ambapo waliamua kumalizana na Keneddy Musonda na kumsajili kwa mkopo Andy Boyeli ambaye hata hivyo hajaonyesha maajabu yoyote akifunga mabao mawili tu.
Nne, lazima kuwe na maelewano ya wazi kati ya uongozi na benchi la ufundi ili kuepuka kusajili wachezaji wasiokuwa kwenye mpango wa kocha. Dirisha hili linahitaji uamuzi wa pamoja, si wa upande mmoja.
Kadri dirisha dogo lilivyofunguliwa hadi Januari 30, Yanga inapaswa kukumbuka kuwa mashabiki hawataangalia majina bali matokeo. Uvumilivu umeanza kupungua na presha inaongezeka kila mchezo unapopita.
Kwa klabu yenye historia na matarajio makubwa kama Yanga, dirisha hili dogo linaweza kuwa mwanzo wa kurekebisha msimu au uthibitisho wa makosa ya dirisha kubwa. Uamuzi uko mikononi mwa viongozi.
Mwisho wa siku, usajili bora haupimwi kwa kelele, bali kwa mchango wa haraka uwanjani.