Prime
The Gunners, miaka 22 ya machozi, jasho na damu
IMESEMWA mara nyingi. Mara ya mwisho kufanya walichokifanya mtandao wa Instagram ulikuwa haujaanzishwa. Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa bado hajawa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Max Dowman alikuwa bado hajazaliwa wakati Gavi wa Barcelona alikuwa na miezi mitatu.
Haishangazi kuona dunia imezimama baada ya Arsenal kutwaa ubingwa. Wahuni wenyewe waliosukuma gurudumu hili walikuwa wamekusanyika katika ukumbi fulani wa uwanja wa mazoezi wa Arsenal uitwao Sobha wakitazama pambano la Bournemouth dhidi ya Manchester City. Kuna kitu kilikuwa kinaweza kutokea. Na kweli kilitokea.
Bournemouth waliisaidia Arsenal kutwaa ubingwa wa England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22. Mashabiki wao, duniani kote walipaswa kukaa katika makochi kusubiri dakika za mwisho za pambano hilo lakini hawakuweza kukaa. Walikuwa wamesimama kama wachezaji wao walivyokuwa wamesimama pale Sobha. Walikuwa wamesimamia kucha wakisubiri filimbi ya mwisho ya mwamuzi, Anthony Taylor.
Naam, baada ya miaka 22 ubingwa wa England umerudi Arsenal. Nahodha wa mwisho kunyanyua kombe lao alikuwa Patrick Vieira. Msimu huo walicheza msimu mzima bila ya kupoteza mechi.
Keshokutwa nahodha ambaye atanyanyua kombe katika dimba la Selhust Park atakuwa Martin Odegaard. Kutoka kwa Mfaransa hadi Mnorway Arsenal wamepitia tanuri la moto kupata ubingwa huu.
Kwa nini? Ilianzia pale mpira ulipoingia pesa. Halafu hapo hapo Arsene Wenger akapoteza maarifa. Roman Abramovich alitua England akaweka noti nyingi Chelsea. Sir Alex Ferguson akaendelea kupambana lakini Arsene alionekana kuishiwa maarifa kwa sababu za ndani na nje ya uwanja. Nje ya uwanja inasemekana Arsenal walikuwa wana bajeti ndogo kwa sababu walikuwa wametoka kujenga Uwanja wa Emirates.
Hata hivyo, bado kuna utata. Mara nyingi matajiri wa Arsenal walidai pesa ya usajili ilikuwepo. Ilionekana tu vile Arsene Wenger alikuwa anataka kuendelea kuonyesha maajabu yake ya kuwageuza wachezaji wa kawaida kuwa wachezaji wa daraja la dunia maarufu kama World Class players.
Alishafanya hivyo kwa kina Patrick Vieira na Thierry Henry. Alimchukua Henry akiwa benchi pale Juventus akamgeuza kuwa mchezaji wa ajabu. Alimtoa Patrick Vieira akisota benchi AC Milan akamgeuza kuwa kiungo bora wa ulinzi duniani.
Ilionekana alikuwa anataka kufanya hivyo kwa kumchukua mchezaji wa daraja la pili Ufaransa kama Yaya Sanogo na kumgeuza kuwa Thierry Henry. Haikuwezekana. Na hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa mwisho wa Arsenal.
Wakati yeye akifanya hivyo, kina Chelsea walikuwa wakitia pesa. Halafu wakaibuka Waarabu wakatia pesa Manchester City. Kuanzia hapo kazi ya Wenger ikawa kugombea kuingia Top Four. Kazi ya ubingwa akawaachia Manchester United, Manchester City na Chelsea.
Ndani ya uwanja kulikuwa na shida. Wenger aliendelea kuwa yule yule ambaye alikuwa anacheza mpira mzuri wa kuvutia usio na mbinu zozote katika ulinzi. Alikuwa anacheza kwa kadri anavyotaka timu yake icheze na sio kupambana na mbinu za maadui. Ikawa rahisi tu kwa Arsenal kufungwa 8-2 na Manchester United. Vipigo vya 6-1 vilikuwa kawaida tu kutoka kwa ndugu zetu Chelsea na Manchester City.
Baadae Liverpool nao wakaunda timu nzuri na wakaanza kupitia humo kumchapa Arsenal 4-1 au 4-0. Kuna ile siku ambayo ndani ya dakika 18 tu Arsenal alikuwa ashachapwa mabao manne pale Anfield.
Mwishowe kabisa mabosi wa Arsenal wakachoka. Wakamtimua kijanja na kuanza mwanzo mpya. Awali walienda kwa Unai Emery lakini ikaonekana Arsenal ni maji mazito kwake. Wakamfukuza.
Mwanzo wa mwisho wa karaha ukaenda kwa Mikel Arteta. Kijana wa nyumbani ambaye alikuwa ameenda kuchota akili kwa kaka yake wa Kihispaniola, Pep Guardiola pale Manchester City akiwa kama kocha msaidizi. Arteta alionekana kuwa na majibu mengi ambayo Wenger aliyakosa katika kipindi kirefu baada ya kutwaa ubingwa bila ya kufungwa.
Tuanzie wapi? Namna alivyoipeleka Arsenal katika mpira wa kisasa. Kwanza kabisa alipangua kikosi kizima na kubakia na wachezaji aliowataka ambao wangecheza aina yake ya mpira.
Pasi fupi na kukaba kwa pamoja kuanzia maeneo yote ya uwanja. Mpira mgumu lakini ndio wa kisasa. Unahitaji wachezaji wanaojituma hasa. Haishangazi kuona kina Pierre-Emerick Aubameyang na Mesut Ozil waliondoka walipoonekana wavivu.
Kitu cha kwanza kabisa aliirudisha Arsenal katika ushindani. Wameshindana hasa hapa katikati. Kilichokosekana kwa Arteta kitu kimoja tu. Namna ya kumalizia msimu. Kuna wakati alikumbana na bahati mbaya ya majeraha pamoja na kadi za ajabu ajabu.
Katika msimu wake wa kwanza wa ushindani ambao alikimbizana na Guardiola akakosa ubingwa kwa pointi chache baada ya kuongoza kwa muda mrefu Arteta alionekana ana tatizo la kukosa kikosi kipana.
Baada ya hapo matajiri wakaanza kutia pesa zaidi na zaidi. Waliwahi kuvunja hata rekodi ya uhamisho ya England kwa kumchukua Declan Rice kwa dau la pauni 105 milioni. Haikuwa tabia ya Arsenal wala Arsene Wenger kufanya mambo haya. Hata hivyo matajiri wa Arsenal walibadilika kitabia wakaanza kutia pesa zaidi na zaidi. Nadhani ni kwa sababu walimuamini Arteta na mipango yake.
Msimu uliopita walipoteza kizembe zaidi kwa kocha anayeitwa Arne Slot. Liverpool ile ya kawaida ikachukua ubingwa mbele ya Arsenal. Mashabiki wa Arsenal walianza kutoa machozi wakiamini Arteta hakuwa kocha sahihi.
Hata hivyo kulikuwa na mgawanyiko wa mawazo. Mtu ambaye aliwatoa jalalani akawapeleka katika kushindania ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo inawezekana vipi asiwe mtu sahihi?
Msimu huu pia ilikuwa inaonekana kama vile ungeweza kumalizika kama msimu uliopita. Alipopoteza fainali ya Carabao na kisha kutolewa nje ya FA na Southampton kabla ya kuchapwa ugenini na Bournemouth, Arteta alianza kuhitimisha fikra za mashabiki wa Arsenal hakuwa mtu sahihi kwao. Lakini ghafla kila kitu kimebadilika baada ya Arsenal kujikuta wametwaa ubingwa wakiwa sebuleni huku wakiwa na mechi moja mkononi.
Mechi ya kesho dhidi ya Crystal Palace wanaweza kumpanga hata Gabriel Jesus katika lango huku wakisubiri fainali ya Ligi ya mabingwa wiki ijayo dhidi ya PSG. Hawana kitu kikubwa cha kujali kwa sasa. Wameshusha pumzi. Wanaruhusiwa kunywa mvinyo kwa raha zao. Ilikuwa miaka 22 yenye machozi, jasho na damu. Miaka ya masimango.
Kwa mtazamo wangu wamechukua ubingwa na kikosi ambacho sio bora sana kama cha misimu mitatu iliyopita. Kuna ubora umepungua kikosini na wamesaidiwa sana na kushuka kwa Manchester City. Hata hivyo sidhani kama watajali sana. Walichohitajika kuwa nacho ni kombe tu. Kombe ni kitu walichokihitaji zaidi.
Hofu yangu kwa wapinzani wa Arsenal ni wajipange. Msimu ujao Arsenal watacheza kwa kujiamini sana huku wakijiona wao ni washindi na wababe. Kitu kizuri zaidi kwao ni Pep Guardiola anaondoka.
Sijui ni nani atamfunga kengele kiurahisi Mikel Arteta. Kushindana na Guardiola huwa ni mateso makubwa. Unaweza kumuuliza pia, Jurgen Klopp. Haiwi kazi rahisi. Arsenal inaweza kuserereka tena msimu ujao na kuendelea kula matunda ya uvumilivu wao.