Seif na rekodi ya mabao 39
Muktasari:
- Akiwa na wastani wa kufunga mabao tisa kwa msimu mmoja, Seif anaonekana kuwa miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa katika eneo la ushambuliaji kwenye ligi hiyo. Hata hivyo, nyota huyo anayevaa jezi namba 10 hataki kuishia hapo, kwani msimu wa 2026-2027 amejiwekea malengo ya kufunga mabao zaidi ya 10 ili kuvunja rekodi yake mwenyewe.
KIUNGO mshambuliaji wa Muembe Makumbi City FC, Seif Iddi Juma, katika kipindi chake cha misimu minne iliyopita ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), amefunga mabao 39, huku akilenga kuongeza idadi hiyo na hatimaye kutumia mafanikio yake kupata changamoto mpya nje ya Tanzania.
Akiwa na wastani wa kufunga mabao tisa kwa msimu mmoja, Seif anaonekana kuwa miongoni mwa wachezaji wenye mchango mkubwa katika eneo la ushambuliaji kwenye ligi hiyo. Hata hivyo, nyota huyo anayevaa jezi namba 10 hataki kuishia hapo, kwani msimu wa 2026-2027 amejiwekea malengo ya kufunga mabao zaidi ya 10 ili kuvunja rekodi yake mwenyewe.
Uwezo wake wa kumiliki mpira, kutoa pasi sahihi, kutumia kasi na kupiga mashuti makali ni miongoni mwa silaha zinazomtofautisha na wachezaji wengine. Mbali na nafasi yake ya kiungo mshambuliaji, Seif pia ana uwezo wa kucheza pembeni mwa uwanja kama winga wa kulia au kushoto, jambo linalomfanya kuwa mchezaji muhimu kulingana na mahitaji ya mwalimu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Seif anasema baada ya kuitumikia Ligi Kuu Zanzibar kwa misimu minne, anaamini sasa ni wakati mwafaka wa kutafuta changamoto mpya nje ya nchi.
Tofauti na wachezaji wengi wanaotamani kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara, ndoto ya Seif imeelekezwa zaidi katika soka la kimataifa, akitamani kucheza katika ligi bora barani Afrika na nje ya bara hilo.
Anasema tangu aanze kucheza soka la kulipwa, amekuwa na azma ya kujenga jina katika medani ya kimataifa na hatimaye kuwa miongoni mwa wachezaji wakubwa duniani.
“Huu ni msimu wangu wa tano, katika misimu minne iliyopita nimefunga jumla ya mabao 39. Kati ya misimu hiyo, wa kwanza ulikuwa bora kwangu kwani nilifunga mabao 12, huku katika misimu mitatu iliyofuata nikifunga mabao tisa kila mmoja. Kwa msimu huu nahitaji kufunga zaidi ya mabao 10,” anasema.
MWENENDO WA MUEMBE MAKUMBI
Licha ya mafanikio yake binafsi, Seif anakiri kutoridhishwa na mwenendo wa mwanzo wa timu yake msimu huu, baada ya kukusanya pointi 18 katika michezo 12, ikiwa ni tofauti na matarajio yao ikishika nafasi ya saba.
Hata hivyo, kiungo huyo anaamini bado hawajapoteza nafasi ya kupigania ubingwa, akisisitiza kuwa wanahitaji kuongeza juhudi na kuhakikisha wanapata ushindi katika michezo inayofuata ili kupunguza pengo la pointi dhidi ya timu zinazowaongoza.
“Tunaweza kuchukua ubingwa bila shaka, lakini tuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunashinda michezo yetu inayokuja ili kupunguza pengo la pointi dhidi ya timu zilizo juu yetu,” anasema.
Akizungumzia maisha yake ndani ya Muembe Makumbi City, Seif anasema amekuwa na wakati mzuri tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Uhamiaji FC, licha ya kukabiliwa na ushindani mkubwa wa namba kutokana na ubora wa kikosi walichonacho.
Anabainisha kuwa kucheza Ligi Kuu Zanzibar, anayoitaja kuwa miongoni mwa ligi bora, kumemsaidia kukua na kuboresha uwezo wake wa kisoka ukilinganisha na kipindi alipokuwa akicheza katika madaraja ya chini.
Anahusisha maendeleo hayo na nidhamu, kujituma pamoja na kufuata maelekezo ya makocha, akiamini kuwa mafanikio ya mchezaji yanahitaji juhudi binafsi na utayari wa kujifunza kila siku.
ATAJA ANAOWAKUBALI
Katika harakati za kuendelea kuboresha kiwango chake, Seif amewataja winga wa Azam FC na timu ya Taifa ya Tanzania, Iddi Suleiman ‘Nado’, pamoja na mshambuliaji wa Atletico Madrid na timu ya Taifa ya Argentina, Julian Alvarez, kuwa miongoni mwa wachezaji anaowakubali na kujifunza kutoka kwao.
Anasema anavutiwa na kasi na uwezo wao wa kufunga mabao, sifa ambazo zimempa hamasa ya kuendelea kujifunza na kupambana ili kuboresha kiwango chake.
Licha ya kutokuwa miongoni mwa wachezaji wanaozungumziwa sana, Seif amekuwa na uwezo wa kutumika katika nafasi zaidi ya moja, hususan kiungo mshambuliaji na winga wa pande zote mbili. Uwezo huo unampa mwalimu machaguo tofauti ya kumtumia kulingana na mahitaji ya mchezo.
Kwa upande wake, anasisitiza kuwa soka kwake si burudani pekee, bali ni kazi inayomuwezesha kujenga maisha yake na kutimiza ndoto alizojiwekea.
“Mimi kazi yangu ni kufunga na kutengeneza nafasi, wakati huohuo kuiongezea timu morali bila kujali kiwango chake,” anasema.
Anaongeza kuwa maandalizi ya mchezo kwake huanza kabla ya kuingia uwanjani, ambapo hujiwekea mipango, malengo na namna ya kucheza ili kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa timu.