Prime
Shikamoo Wananchi

Muktasari:
- Masharti yote waliyoyatoa ili wacheze mechi ya marudio ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba yametimizwa. Walitaka mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi aondoke...kaondoka. Walitaka mwenyekiti wa Bodi ya Ligi aondoke...kaondoka.
YANGA imefanikiwa kuzishinda mamlaka za mpira wa Tanzania...kuushinda mpira wa Tanzania. Kitendo cha kuwaangusha viongozi wa juu kabisa wa Bodi ya Ligi na TFF kina maana kwamba Yanga wamekuwa wakubwa kuliko mpira wa Tanzania.
Masharti yote waliyoyatoa ili wacheze mechi ya marudio ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba yametimizwa. Walitaka mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi aondoke...kaondoka. Walitaka mwenyekiti wa Bodi ya Ligi aondoke...kaondoka.
Walitaka katibu mkuu wa TFF aondoke hadi inaandikwa makala hii alikuwa hajaondoka, lakini taarifa za uhakika kutoka vyanzo vya kuaminika zinasema naye ataondoka. Walitaka mechi ibadilishwe tarehe...imebadilishwa. Kwa kifupi Yanga wamepata kila walichotaka.
Labda kuvunjwa kwa Bodi ya Ligi ambako hakuwezi kufanyika ghafla...ila nako kunakuja, kwa mujibu wa taarifa. Kwa hiyo, Yanga wamepata kila kitu...wameshinda hii vita, wameushinda mpira. Kwa sasa Yanga ndio mpira wa Tanzania...Yanga ndio sheria ya mpira.

Viongozi watakaokuja baada ya hawa wanaoondoka, lazima watakuwa waoga kupitiliza kwa Yanga yasije yakawakuta kama ya hawa. Watacheza muziki ambao Yanga wataupiga maana yake Yanga ndio watakuwa wanaongoza mpira wa Tanzania. Hii ni bahati mbaya sana, lakini ndivyo Yanga walivyozaliwa. Ndio asili yao.
Yanga wamekuwa na tabia hii tangu wakiwa wadogo...tangu wanazaliwa. Yanga wamezaliwa kushinda mapambano ya aina hii kuliko hata mechi za mpira. Hakuna kupindi ambacho Yanga huwa wamoja kama cha mapambano ya aina hii. Yanga wanafurahia zaidi kupigana vita hizi ili washinde na kujitanua kimamlaka kuliko kushinda mechi ya mpira ambayo ushindi wake huchuja baada ya siku chache.
Kupitia mkasa huu, leo nataka nikuletee vita vya kwanza vya aina hii ambavyo Yanga walishinda wakiwa wadogo kabisa.

Ushindi huo ndio uliowapa kiburi kinachoendelea kuonekana hadi leo. Mpira uliingia nchini miaka ya 1920 baada ya ujio wa utawala wa Waingereza kufuatia kuondoka kwa Wajerumani.
Timu mbalimbali zilianzishwa kwa misingi ya kibaguzi. Kulikuwa na timu za Wazungu, Wahindi, Waarabu na Waafrika. Timu kubwa zaidi ya Waafrika iliitwa Jangwani Sports Club iliyoanzishwa 1926. Hakukuwa na chama cha kusimamia mpira wala mashindino rasmi hadi 1929. Huo ndio mwaka ambao chama cha kwanza cha kusimamia soka kilianzishwa nchini.
Chama hicho hakikuwa cha kitaifa, bali cha wilaya ya Dar es Salaam na kiliitwa Dar es Salaam Football Association (DFA).
Baada ya kuanzishwa, chama hiki kikapewa jukumu la kuanzisha ligi rasmi, na mwaka huo huo ligi hiyo ikaanzishwa. Mtendaji Mkuu wa chama hicho, A.B Humphrey, alitoa tangazo kwenye gazeti kubwa zaidi la wakati huo la Tanganyika Times kama ifuatavyo;

As all soccer enthusiasts know, the above league has now been formed and a cup and medals will be presented to the champions.
Therefore, non-players should officiate at league matches.
If any of your leaders who are old soccer players would care to officiate at some of the matches, I would be glad if they let me have their names, as soon as possible.
The league matches begin on June 1st, 1929.
Tangazo hili lilitoka miezi miwili kabla ya ligi kuanza, Juni Mosi, 1929. Ligi hii ilianza kwa kuwa na daraja moja tu; la kwanza hadi 1932 lilipoanzishwa daraja la pili. Ligi Daraja la Kwanza lilidhaminiwa na kamishna wa Polisi aliyeitwa Percy F. Browne, na ligi hiyo ikaitwa Browne Cup.
Msimu wa kwanza ulikuwa na timu 6; King’s African Rifles Club (K.A.R), Government School, Police, Railways, Gymkhana
Government Service. K.A.R ambayo ilikuwa timu ya jeshi, ikawa mabingwa kwa mwaka wa kwanza. Ligi Daraja la Pili iliyoanza 1932 lilidhaminiwa na tajiri mmoja aliyeitwa Kassum Sunderji Samji na mashindano yake yakaitwa Kassum Cup.

Hata hivyo, ligi hii ilikuwa ya wageni watupu yaani Wazungu, Wahindi na Waarabu wazawa yaani Waafrika hawakuruhusiwa kuingiza timu yao. Kitu pekee walichoruhusiwa ni kuchagua timu za kushangilia miongoni mwa zile za wageni. Watu wengi wakiichagua timu iliyoitwa New Strong SC ambayo angalau ilikuwa na wachezaji wazawa.
Timu hiyo iliyoanzishwa 1921, ilishiriki Ligi Daraja la Pili mwaka 1932 na kupanda la kwanza. Ikacheza la kwanza 1933 na 1934, lakini ikashuka na baadaye ikapasuka vipande viwili; New Strong A na New Strong B. Nahodha wa timu hiyo, A. E. Selemani alisema timu yao iliathirika na vitisho vya kibaguzi kwa kutumia wachezaji wazawa.
Hii iliwaumiza sana Waafrika na kurudisha tena tamanio la kuwa na timu zao wenyewe. Waafrika walitamani sana timu zao zishiriki hasa Jangwani Sports Club ambayo ndio ilikuwa na mashabiki wengi. Jambo hilo lilileta mpasuko mkubwa kiasi cha kuathiri uchaguzi wa DFA ambao ulikuwa ufanyike mwaka huo.
Uchaguzi ulipofanyika, DFA ikapata viongozi wapya; Bwana J.R.Harvey akawa rais, Bwana H. Mcleven akawa makamu wa rais na Bwana Hall akawa katibu mkuu (mtendaji mkuu). Uongozi mpya ukaleta mabadiliko na kuruhusu timu za wazawa kushiriki ligi.
Hapo sasa harakati za wazawa kuwa na timu zao kwenye ligi zikalipa, na mwaka 1935, zikaruhusiwa.
Bahati mbaya mwaka huo timu kubwa ya wazawa, Jangwani Boys, ikafa. Ili kuitumia nafasi ya vizuri baadhi ya mashabiki wake wakaamua kuanzisha timu mpya iliyoitwa New Young. Timu hiyo ikajiandikisha kushiriki Ligi Daraja la Pili yaani Kassum Cup. New Young ikawa timu ya kwanza ya wazawa kushiriki ligi na hapo ndipo jina la Wananchi lilipoanzia. Yaani timu ya kwanza ya wananchi zingine zote hazikuwa za wananchi, bali wageni.

Mambo yakawaendea vizuri na kushinda ubingwa, hivyo kupanda daraja. Mwaka 1936 wakashiriki Ligi Daraja la Kwanza, lakini mambo hayakuwa mazuri. Hadi inafika Novemba, New Young ilishinda mechi mbili na sare tatu ikijipatia alama saba pekee. Mwisho wa msimu ikashuka daraja.
Kushuka kwao pia kukageuka balaa kama ilivyokuwa kwa New Strong nao wakagawanyika, kwa wengine kujitenga. Waliojitenga waliulalamikia uongozi kutowajibika. Waliobaki walilalamikia ubaguzi wa rangi kwenye ligi kwamba hata waamuzi ambao walikuwa wageni pia walikuwa wanawaonea dhidi ya timu zao.
Waliojitenga wakaanzisha klabu yao mpya iliyoitwa Stanley Football Club. Klabu hiyo iliitwa hivyo kwa sababu ilianzishiwa mtaa wa Stanley ambao sasa ni Aggrey. Wale waliobaki wakaibadilisha jina timu na kuiita Young Africans, huku lile jina la Wananchi wakiendelea nalo.
Hawa Young Africans wakasema hawatashiriki Ligi Daraja la Pili mwaka 1937 hadi mfumo wa waamuzi ubadilike na kama hautabadilika, basi watajitoa kwenye ligi na kuanzisha ligi yao wenyewe itakayochezwa na timu za wazawa watupu - Africans Football League chini ya Chama cha Africans Football Association.
Hilo lilikuwa tamko zito kutolewa na hata serikali ya kikoloni ilitikisika. Hofu ikawa endapo ligi ya Waafrika ikianzishwa ile iliyokuwepo yaani Ligi ya Dar es Salaam ingepooza na hatimaye kufa kabisa. Hadi hapo DFA ilitambuliwa na Fifa na ikachukuliwa kama mfano kwa kusimamia ligi zenye mafanikio.
Ukiacha zile ligi mbili yaani daraja la kwanza (Browne Cup) na la pili (Kassum Cup), pia DFA ilianzisha mashindano ya majimbo yaliyodhaminiwa na Meja Jenerali J.E.Higgins na kuitwa Higginson Cup. Majimbo ya wakati huo ni sawa na mikoa kwa sasa. Kwa hiyo serikali ilihofia sifa kubwa ya DFA ingeingia dosari, na pia ligi ya wazawa peke yao ingegeuka kuwa chombo cha harakati za uhuru.
Ilibidi mkutano mkubwa ufanyike Splendid Hotel Dar es Salaam, Julai 7, 1937. Mkutano huo ukaanzisha Chama cha Waamuzi kilichoitwa Association of Football Referees (AFR). Young Africans wakawa wameshinda vita dhidi ya ubaguzi. Chama kipya cha waamuzi kikatenda haki na timu ya Wananchi ikapanda tena daraja 1938 kurudi Daraja la Kwanza.
Wale waliojitenga yaani Stanley FC wakajibadili jina mwaka 1939 na kuwa Sunderland ambao sasa ni Simba SC. Mwaka 1936 wakiwa na miaka miwili ya kuzaliwa, Wananchi waliitingisha serikali ya wakoloni ikatikisika. Mwaka 2025 wakiwa na miaka 90 wamezitingisha mamlaka za mpira na zimetingishika. Shikamoo Wananchi.