Pina kama ilivyokuwa kwa Maabad na Hilika
Muktasari:
- Pina aliyefanya vizuri na Mlandege msimu wa 2024-2025, hadi kuibuka mfungaji bora, ameshindwa kuwika katika Ligi Kuu, akifuata nyota wengine waliowika Zanzibar na kushindwa kutamba Bara, wakiwemo, Maabad Maulid na Ibrahim Hamad Hilika.
MSHAMBULIAJI wa Pamba Jiji, Abdallah Idd 'Pina' amekamilisha uhamisho wake wa kujiunga na timu ya Muembe Makumbi City ya Zanzibar baada ya kushindwa kuwika katika Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho cha 'TP Lindanda'.
Pina aliyefanya vizuri na Mlandege msimu wa 2024-2025, hadi kuibuka mfungaji bora, ameshindwa kuwika katika Ligi Kuu, akifuata nyota wengine waliowika Zanzibar na kushindwa kutamba Bara, wakiwemo, Maabad Maulid na Ibrahim Hamad Hilika.
Nyota hao walifanya vizuri na kuweka rekodi mbalimbali katika Ligi Kuu Zanzibar kiasi cha kuzivutia timu za Bara kuzitaka saini zao kwa nguvu na ushindi, japo baada ya kutua mambo yamekuwa tofauti na kujikuta wakionekana wa kawaida.
Baada ya Pina kuitumikia Pamba kwa mkataba wa miezi sita tu na kutolewa kujiunga na Muembe Makumbi City kwa mkopo, nyota huyo ameendeleza yaliyowashinda washambuliaji wengine wa Zanzibar walipotua Bara kama ambavyo Mwanaspoti linaeleza.
ABDALLAH IDD 'PINA'
Nyota huyo aliyejiunga na Pamba msimu huu akitokea Mlandege ya Zanzibar na kusaini mkataba wa miaka miwili, alitabiriwa kufanya mambo makubwa kutokana na alichofanya msimu wa 2024-2025, akiwa na kikosi hicho, ingawa mambo yamekuwa tofauti.
Msimu uliopita wa 2024-2025, katika Ligi Kuu ya Zanzibar, Pina aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21, kwenye mechi 22, alizozicheza, huku akichangia pia mengine 12 (Assisti), japo akiwa na Pamba hajafunga bao lolote la Ligi Kuu.
Uwepo wa washambuliaji wengine wakiwemo, Mkenya Mathew Momanyi aliyefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 na sasa 2025-2026, akifunga mawili, umechangia zaidi kwa nyota huyo kukosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Kiwango cha mshambuliaji, Abdoulaye Camara anayeichezea Pamba kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, aliyefunga mabao manne ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 na sasa 2025-2026, akifunga moja, ni sababu nyingine ya Pina kukosa nafasi.
Ujio pia wa Mganda Peter Lwasa aliyejiunga na kikosi hicho cha Pamba akitokea Kagera Sugar, ambaye msimu huu tayari amefunga mabao matatu ya Ligi Kuu Bara huku akionyesha kiwango kizuri, kumechangia kwa nyota huyo kutolewa kwa mkopo.
Pina aliyeianza safari ya soka mwaka 2015, amezichezea pia timu za, Magomeni, Gulioni, Jang’ombe Boys, Polisi Tanzania, Kipanga, Kundemba, Mlandege na sasa Muembe Makumbi City, huku za nje ni za Alzakhir ya Dubai na Chaux Sport ya DR Congo.
MUDRIK ABDI SHEHE 'GONDA'
Baada ya kuondoka Seleman Mwalimu 'Gomez' katika kikosi cha Fountain Gate, mabosi wa timu hiyo walimsajili Mudrik Abdi Shehe 'Gonda' kutoka JKU ya Zanzibar kwenye dirisha dogo la Januari 2025, kufuatia kufunga mabao manane ya kikosi hicho.
Usajili wa nyota huyo, ulikuwa wa kuziba nafasi ya Gomez, aliyejiunga na Wydad Casablanca ya Morocco kisha kutolewa kwa mkopo msimu huu kujiunga na Simba, ingawa ujio wa Gonda ulimshuhudia akimaliza msimu wa 2024-2025, bila bao la Ligi Kuu.
Msimu huu wa 2025-2026, nyota huyo ametoa gundu baada ya kufunga bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa Fountain Gate wa 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa Babati mkoani Manyara, Oktoba 17, 2025.
MAABAD MAULID
Mshambuliaji Maabad Maulid ni nyota mwingine aliyefanya vizuri Zanzibar, ambapo kiwango bora alichoonyesha kiliwavutia mabosi wa Coastal Union, japo licha ya uwezo wake mzuri wa kufunga imekuwa ni tofauti Ligi Kuu Bara.
Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022 akitokea KVZ ya Zanzibar ambako alikuwa mfungaji bora mara mbili mfululizo akianza na msimu wa 2020-2021 alipofunga mabao 17 kisha na uliofuata wa 2021-2022 akafunga mabao 21.
Licha ya rekodi hiyo bora tangu amejiunga na Coastal Union hajawahi kufikisha hata mabao 10 Ligi Kuu Bara, kwani msimu wake wa kwanza wa 2022-2023 alifunga manne, huku 2023-2024 akifunga matatu.
Msimu wa 2024-2025 nyota huyo alifunga mabao matano, huku bao la mwisho kufunga lilikuwa la ushindi wa kikosi hicho wa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Februari 7, 2025.
Hadi sasa msimu huu mshambuliaji huyo ameshafunga mabao mawili Ligi Kuu Bara akiwa na Wagosi wa Kaya, ambapo yote amefunga katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbeya City, Novemba 26, 2025.
YASSIN MGAZA
Nyota mwingine ni Yassin Mgaza ambaye pia alikuwa mfungaji bora katika Ligi ya Zanzibar akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-2023, ambapo alichangia mabao 25, baada ya kufunga 17 na kuasisti manane kwenye mechi 25 kati ya 30, alizocheza.
Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni ya Arusha ambayo kwa sasa inashiriki Ligi ya Championship, ingawa kwa msimu huo ilikuwa Ligi Daraja la Pili, First League, ambapo alionyesha kiwango kizuri kilichoishawishi KMKM kuihitaji saini yake.
Akiwa na Mbuni, Mgaza alihusika katika jumla ya mabao 22 kwa msimu mzima kwenye mechi 16, alizocheza, baada ya kufunga mabao 16 na kuasisti mengine sita, ingawa kiwango hicho bora kwake alikiendeleza hadi alipojiunga na kikosi cha KMKM.
Baada ya hapo, mabosi wa Dodoma Jiji wakamsajili kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji kwa msimu wa 2023-2024 na kubeba matarajio makubwa ndani ya kikosi hicho, ingawa aliangukia pua baada ya kufunga mabao matatu kwa msimu mzima.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Mgaza alifunga bao moja lililokuwa la kichapo ilichokipata Dodoma Jiji cha mabao 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Liti Singida, Desemba 12, 2024.
Mwenendo wa nyota huyo bado sio wa kuridhisha tofauti na mambo makubwa aliyoyafanya akiwa Ligi ya Zanzibar, kwani hadi sasa pia amefunga bao moja la Ligi Kuu, katika ushindi wa Dodoma Jiji wa 2-0, dhidi ya Coastal Union, Septemba 27, 2025.
IBRAHIM HAMAD HILIKA
Hilika ni miongoni mwa washambuliaji bora waliofanya makubwa katika Ligi ya Zanzibar, japo kwa upande wa Ligi Kuu Bara, nyota huyo ameshindwa kuonyesha makali yake, licha ya kuzichezea timu mbalimbali za, Polisi Tanzania na Mtibwa Sugar.
Mshambuliaji huyo, alijizoelea umaarufu mkubwa wakati akiichezea Zimamoto ya visiwani Zanzibar, ambapo alikuwa mfungaji bora mara mbili, akianza msimu wa 2016-2017 alipofunga jumla ya mabao 33, kuanzia Ligi ya Kanda hadi hatua ya nane bora.
Katika Kanda ya Unguja, Hilika alifunga mabao 19 msimu huo, huku kwenye hatua ya nane bora nyota huyo alifunga jumla ya mabao 14, hivyo kuhitimisha msimu kibabe kwa kufunga 33, hali iliyovutia timu mbalimbali zilizohitaji kupata saini yake.
Msimu mwingine wa 2019-2020, nyota huyo akaendeleza balaa akiwa na kikosi hicho cha Zimamoto, ambapo alifunga jumla ya mabao 20, akimpita bao moja tu mshambuliaji wa kikosi cha JKU, Shehuu Magaji Buwa aliyehitimisha msimu huo na mabao 19.
Kabla ya Hilika kuibuka mfungaji bora, msimu uliopita wa 2018-2019, nyota wa Zimamoto, Abubakar Khamis Sufiani 'Kabela Kanu' na Mussa Ali Mbarouk wa KMKM, wote walikuwa wafungaji bora wa Ligi hiyo baada ya kufunga mabao 23, kila mmoja wao.
Licha ya rekodi tamu kwa Hilika, ila nyota huyo ameshindwa kuonyesha makali yake katika Ligi Kuu, baada ya kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Mtibwa Sugar, maafande wa Polisi Tanzania na hadi sasa pia TRA United zamani Tabora United.
Hilika hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho cha TRA United, huku pia hata nafasi ya kucheza mara kwa mara ikiwa ni finyu, kutokana na ushindani wa eneo hilo linaloongozwa na nyota, Mzambia Chanda Chewe.
MSIKIE PINA
Katika mahojiano aliyoyafanya na Mwanaspoti, Pina anasema Ligi Kuu Zanzibar haina presha kubwa kama ilivyo Bara, japo sababu iliyochangia kushindwa kuonyesha ubora ni kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya goti.
"Ukweli ni kwamba nimeenda Muembe Makumbi City kwa mkopo wa miezi sita ili kutafuta utimamu wa mwili baada ya kukaa nje kwa muda mrefu, kwa sababu tangu nimejiunga pia na Pamba sijacheza mechi nyingi kutokana na kuumia goti," anasema Pina.