Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Msimu Mpya wa 2023/24 uko mikononi mwa waamuzi

KUJIANDAA na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara (Tanzania Mainland Premier League), waamuzi ni wadau wakuu katika kufanikisha au kutofanikisha mashindano hayo. Mpira wa miguu hauwezi kuchezwa bila waamuzi.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), mwamuzi ndio mamlaka ya mwisho katika mchezo wa mpira wa miguu katika dakika zote mchezo unapoendelea.

Mamlaka na umuhimu wa waamuzi katika mchezo wa soka hayapingiki japo hawaimbwi. Mwamuzi ana uwezo wa kuanzisha na kusimamisha au kumaliza mchezo.

Mwamuzi anafanya kazi na waamuzi wasaidizi ambao pamoja na kutokuwa na maamuzi ya mwisho lakini wanawezesha mwamuzi kufanya maamuzi yake kwa usahihi akiwa nao kama jicho la tatu katika kutafsiri sheria 17 za mchezo.

Matumizi ya waamuzi katika mchezo wa mpira wa miguu yalianza takribani miaka 200 iliyopita huko Uingereza.
Kabla ya hapo mchezo huu ulionekana ni wa kiungwana kwa maana ya pande zinazocheza zilikuwa na uwezo wa kukubaliana katika mwenendo wa mchezo.

Ushindani mkubwa katika mchezo huu uliendelea kupandisha hadhi na nafasi ya waamuzi.
Hapa nyumbani hasa katika ligi kuu kumekuwa na malalamiko yasiyokwisha kuhusu uwezo na usahihi wa waamuzi.

Maamuzi yasiyo sawa ya waamuzi yamezikosesha timu pointi, maamuzi yasiyo sahihi yamezishusha timu daraja, maamuzi yasiyo sahihi yamezibakiza timu kwenye ligi, maamuzi yasiyo sahihi yamezipandisha timu daraja.

Makosa ya waamuzi yanatokana na mapungufu katika uelewa, mapungufu katika utimamu wa mwili, upendeleo binafsi na hata rushwa.
Kuna waamuzi wamepandishwa madaraja haraka hata kabla ya kuelewa vizurijinsi ya kutafsiri sheria 17 za mchezo hivyo hujikuta katika wakati mgumu kwenye kufanya maamuzi. Kuna waamuzi hawako timamu kimwili kwa maana ya kuwa na kasi,pumzi na hata uwezo wa kuona vizuri matukio, hawa pia watapata ugumu kusimamia mchezo.

Kuna waamuzi wana mapenzi au mahusiano na timu kiasi cha kushindwa kujizuia kuipendelea timu ya mapenzi ya. Hili ni tatizo la kibinadamu lakini ni tatizo kubwa kwa mchezo wenyewe. Ni vema mwamuzi akawa shujaa na kuomba kutochezesha mchezo anaofikiria una mgongano wa maslahi kwake kuliko kuficha huku akichezesha na kuharibu.

Kumekuwa na tuhuma za rushwa miongoni mwa waamuzi. Mwamuzi anayepokea rushwa hawezi kufanya maamuzi kwa mujibu wa Sheria 17 za mchezo kwa sababu anawatumikia waliomlipa au kumpa rushwa badala ya kutumikia mpira.
Mara kadhaa kuna tuhuma zimewaendea viongozi wa vilabu kwamba wanashawishi na hata kutoa rushwa kwa waamuzi. Mamlaka na vyombo vinavyodhibiti rushwa michezoni na rushwa kwa jumla vinatakiwa kuwa makini na ile lakini la muhimu zaidi ni waamuzi kukataa rushwa na kutoa taarifa pale kunapokuwa na majaribu ya rushwa.

Ili kuweza kufanya vizuri waamuzi wapewe mafunzo ya kutosha na kuchujwa kulingana na uwezo na uzoefu wao. Ni juu ya shirikisho la mpira kuhakikisha yako mafunzo sahihi na kwamba waamuzi  wanapandishwa madaraja kulingana na uwezo na uzoefu.

Utimamu wa mwili ni suala la kiafya na kimazoezi. Tiba kwa waamuzi ni muhimu kwa waamuzi kama ilivyo kwa wachezaji. Waamuzi wasaidiwe matibabu nao pia wajiangalie  kwa kufanya mazoezi, kula na kulala vizuri na mitindo yao ya maisha kwa ujumla.

Hakuna jambo linalosikitisha na linalochangia waamuzi kutofanya vizuri kama kwenda kwenye vituo vyao vya michezo bila posho zao. Ni jambo lisiloingia akilini kwamba mchezaji anatoka Dar kwenda kuchezesha mchezo Mbeya bila posho ya kujikimu.

Anayemlipa mpiga zumari ndiye huchagua wimbo. Wanaowapokea waamuzi na kuwapa sehemu za kufikia wana nafasi kubwa ya kushawishi maamuziyao.
Msimu unapoanza, Bodi ya Ligi (TPLB) ihakikishe mazingira na maslahi ya waamuzi yako sawa kwani mpira uko mikononi mwao. Waamuzi wazuri wataifanya ligi hii iwe bora zaidi.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF). Mtumie maoni yako kupitia namba yake hapo juu.