Gumbo, Makaga wabeba matumaini ya wana Yanga
Muktasari:
- Baada ya kuwaangalia wagombea wawili wa nafasi za juu mbili za urais, Hersi Said na makamu Arafat Haji na kila nafasi ina mtu mmoja pekee anayetetea kiti chake, tunahamia kwa kuwaangalia wagombea wa nafasi za ujumbe.
HUU ni mfululizo wa makala za wagombea kwenye uchaguzi Mkuu wa Yanga utakaofanyika Agosti 2, 2026, jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwaangalia wagombea wawili wa nafasi za juu mbili za urais, Hersi Said na makamu Arafat Haji na kila nafasi ina mtu mmoja pekee anayetetea kiti chake, tunahamia kwa kuwaangalia wagombea wa nafasi za ujumbe.
Katika nafasi ya wajumbe, kuna watu 16, huku wakihitajika nane pekee ambao watachaguliwa kwenye uchaguzi huo.
Leo tunaanza na wagombea wawili wa nafasi ya ujumbe ambao ni Rodgers Hemedi Gumbo na Yanga Evarist Makaga. Kumbuka zoezi la kampeni limefunguliwa Julai 25, 2026.
RODGERS GUMBO
Yeye anataka kurudi kuendelea kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji baada ya kupata mafanikio makubwa katika awamu zilizopita.
Gumbo ambaye ni mfanyabiashara, inawezekana ndiye mgombea mwenye uzoefu zaidi miongoni mwa wagombe wa nafasi hii, akiwa ameshiriki katika kamati tendaji za awamu mbili tofauti chini ya marais wawili tofauti akitangulia kipindi cha utawala wa aliyekuwa mwenyekiti wa klabu hiyo Dk Mshindo Msolla na sasa injinia Hersi Said.
Gumbo kabla ya hata kipindi cha utawala wa Msolla alikuwa mjumbe wa kamati ya mashindano ambayo ilikuwa inatokana na uteuzi wa rais na baadaye kuamua kugombea akiwa na uzoefu mkubwa ndani ya majukumu ya klabu hiyo.
Kwenye utawala wa Hersi, Gumbo hakuwa mjumbe tu wa kamati ya utendaji alikuwa mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya klabu hiyo iliyokuwa na kazi ya kusimamia afya ya ushindani bora katika muda wote wa utawala wao.
Akiwa mwenyekiti wa kamati ya mashindano Gumbo ameiongoza Yanga ikikusanya jumla ya mataji 18 tofauti ya ndani ya Tanzania na nje huku pia Kimataifa akiweka rekodi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kuchewza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Gumbo sio mtu wa kuongea sana lakini amekuwa akijitambulisha kwa utendaji zaidi kusuka mipango ya ushindi kwenye kamati yake yenye vigogo wazito kama Lucas Mashauri, Davis Mosha, Seif Ahmed ‘Seif Magari’, Pelegrinous Rutayuga, Omar Kimosa Majid Seleman na injinia Mustapha Himba.
MFAHAMU YANGA MAKAGA
Ndani ya Yanga jina la Yanga Evarist Makaga likitajwa tu utasikia mashabiki wa klabu hiyo wanalipuka kwa furaha hii ni kutokana na kupewa jina lake likiakisi pia mapenzi ya klabu anayoish abikia ya Yanga SC.
Makaga ni mjumbe mwenye nguvu ya ushawishi akitokea Kanda ya Ziwa na unaposikia klabu hiyo inakwenda eneo hilo basi mambo mengi ya usimamizi na mapokezi yanakuwa chini ya usimamizi wake na klabu hiyo huona timu inakuwa salama.
Makaga amekuwa na nguvu ya kuisaidia klabu hiyo miaka mingi akiwa mjumbe wa kamati ya mashindano kabla ya kuingia kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji rasmi katika kipindi cha kwanza cha utawala wa Rais Hersi Said kinachomaliza muda wake.
Kigogo huyo mpole sio tu kipenzi cha mashabiki wa Yanga lakini pia hata wachezaji wakimuona wanafurahia kuwa naye kutokana na kujua kuishia nao na kutoa posho pale wanapofanya vizuri uwanjani.
Moja ya tukio kubwa ambalo Makaga amewahi kulifanya ni kuamua kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Waziri Junior wakati akisajiliwa na klabu hiyo mara ya mwisho akitokea Mbao ya Mwanza, akimaliza mchezo huo kirahisi.
Wakati huo kumbuka Yanga ilikuwa ikikabiliwa na ukata mkali wa fedha akaamua kuibeba klabu anayoishabikia akishirikiana na viongozi wenzake.
Mkaaga amekuwa akishiriki majukumu ya Yanga kwa zaidi ya miaka 20 sasa ambapo amekuwa sio mtu wa kuwabagua watu ambao wana mapenzi na klabu hiyo na moja ya jukumu ambalo huwa analibeba kwa ufasaha ni kuhakikiusha timu hiyo inashinda kwenye kila mchezo inapokwenda Mwanza ambako ndiko anakoishi.
Ukiwauliza viongozi wa juu wa Yanga kwanini wanamkubali Makaga watakwambia na sio mtu wa maneno ukiondoa salamu akipewa jukumu atalibeba kwa ufasaha kwenye utekelezaji,kigogo huyo anataka kurudi tena akionyesha bado timu hiyo inahitaji viongozi kama yeye kuipa mafanikio zaidi.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2022, Makaga aliweka rekodi ya kuwa mjumbe aliyepata kura nyingi ambapo sasa tutaona atailinda rekodi hiyo au itakuwaje? Majibu yatapatikana Agosti 2.