Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NIONAVYO: Hongera Yanga na Tanzania, kazi imeanza

HATIMAYE timu ya Young Africans (Yanga) ya Tanzania imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika (CAF Confederation Cup).

Yanga walipata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya klabu ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini katika mchezo uliofanyika kwenye dimba la Royal Bafokeng lililoko kwenye mji wa Rustenburg. Kwa ushindi huo Yanga wanakuwa washindi wa jumla kwa magoli 4-1 kwani katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliofanyika Dar Es Salaam Yanga walishinda 2-0.
Ushindi wa Yanga na hasa nafasi ya kucheza fainali za mashindano ya Afrika unaingia katika vitabu vya historia katika mpira wa Tanzania na Afrika Mashariki kwani si vilabu vingi katika ukanda huu zilizofikia hatua hii.

Ukiangalia safari ya mafanikio ya Yanga, haikuwa rahisi kwani waliingia katika mashindano haya wakitokea kwenye Ligi ya Mabingwa ambako walitolewa na timu ya Al-Hilal ya Sudan. Baada ya kuhamia kwenye kombe la shirikisho waliifunga klabu ya Africain ya Tunisia na kuweza kutinga hatua ya makundi. Katika hatua hii Yanga waliongoza kundi lililokuwa pia na timu za TP Mazembe ya Congo DRC,US Monastir ya Tunisia na AS Bamako ya Mali.

Robo fainali walivunja mwiko wa klabu ya Rivers United ambayo ilikuwa haijafungwa nyumbani kwa kuifunga magoli mawili na kisha kutoka suluhu katika mchezo wa marudiano jijini Dar Es Salaam.
Kituo kinachofuata kwa Yanga ni mchezo wa fainali dhidi ya klabu ya USM Alger ya Algeria ambayo imefuzu kwa kuiondoa Asec Mimosas ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 2-0.

Haitakuwa rahisi kwa Yanga kwani timu wanayokwenda kukutana nayo ina uzoefu wa michezo mikubwa na inatokea Algeria,nchi ambayo klabu zake ziko kwenye kumbukumbu za kutwaa vikombe kadhaa vya Afrika. Hata hivyo,rekodi zinaonyesha kwamba Yanga katika msimu huu imekuwa ikibadilika kulingana na mshindani wanayekutana naye.Chini ya kocha Nasredine Nabi na kikosi chake kipana,hakuna timu Afrika inaweza kuichukulia Yanga kwa urahisi.

Bila shaka uongozi wa klabu, wawekezaji, benchi la ufundi na wachezaji watajiandaa kwa umakini kwa ajili ya mchezo unaokuja dhidi ya USM Algiers wakijua kuwa uwanjani si mchezo tofauti na iliyotangulia lakini fainali hiyo ya mikondo miwili ya nyumbani na ugenini imebeba fahari ya klabu na fahari ya Taifa.
Yanga ambao tayari wametia kibindoni mamilioni ya fedha kwa hatua waliyofikia, sasa wanakitolea macho kitita kinachokaribia shilingi bilioni 5 za kitanzania ambacho kimetengwa na waandaaji CAF kama zawadi ya bingwa wa kombe la shirikisho.

Juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan zimefanikisha hamasa kwa watanzania kiasi cha timu kuingia uwanjani ikiwa na sapoti ya taifa.Kumbuka Rais Samia alianza kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 5 kwa kila goli lililofungwa na klabu za Simba na Yanga wakiwa kwenye hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika na shilingi milioni 10 kuanzia nusu fainali.Mchezo wa Gallants na Yanga kule Afrika Kusini uliudhuriwa na watanzania wengi wakiongozwa na Naibu Waziri anayeshughulia na michezoMheshimiwa Hamis Mwinjuma waliufanya uwanja wa Royal Bafokeng ukawa kama uwanja wa nyumbani kwa Yanga.Bila shaka sapoti ya serikali na ya watanzania itaendelea au kuzidishwa katika hatua muhimu iliyo mbele ya Young Africans.

Hatua inayokuja ni fursa si tu kwa Young Africans kama timu bali Tanzania kama taifa na nchi itaweza kuonekana kwa kuwa mwenyeji wa fainali za Afrika.Fursa hii imekuja kwa gharama kubwa za wawekezaji,uongozi mahiri,benchi zuri la ufundi,kujituma kwa wachezaji na uungaji mkono wa mashabiki.Bila shaka Yanga watafanikiwa kuvunja miiko na rekodi nyingine kama ambavyo wamekuwa wakifanya katika kila hatua.

Mwandishi wa Makala hii ni Katibu mkuu mstaafu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).Tuma maoni yako kuhusu makala hii kwenye namba yake hapo juu.