Ndemla amechukua uamuzi wa miaka miwili nyuma

SAIDI Ndemla amekwenda kwa mkopo katika klabu ya Mtibwa Sugar akitokea Simba. Ni uamuzi ambao alipaswa kuufanya miaka miwili nyuma. Pengine sasa hivi angekuwa anasajiliwa na klabu moja kubwa nchini kama sio Simba yenyewe, Yanga au Azam.

Rafiki yake, Hassan Dilunga aliwahi kuchukua uamuzi huu wakati eneo la kiungo la Yanga liliposheheni mafundi kama Thaban Kamusoko na Haruna Niyonzima. Dilunga alikosa nafasi akaenda zake Mtibwa Sugar. Akaibuka kuwa staa mkubwa akarudi katika timu nyingine ya Kariakoo.

Ndemla ana kipaji kikubwa lakini kwa muda mrefu alikuwa ameridhika kukalia benchi Simba. Wenyewe huwa wanaamini kwamba ni afadhali ukalie benchi Simba na Yanga kuliko kucheza timu za mikoani. Timu za mikoani zina uchumi mbovu na maisha ya shida.

Ndani ya msimu mmoja wa mkopo akiwa na Mtibwa, Ndemla atakuwa akicheza karibu kila wikiendi na ataimarisha kiwango chake huku pia akiimarisha uwezo wake wa kujiamini. Atataka kusimama na kuwa mchezaji muhimu zaidi Mtibwa kuliko wengine wote. Na wenzake pia watamuheshimu kwa sababu wanajua kiwango chake.

Bahati mbaya ana mkataba wa miaka miwili Simba. Hata atakapomaliza kipindi chake cha mkopo atajikuta anahitajika kurudi klabuni. Vinginevyo namtabiria kwamba atafanya makubwa na angeweza kupata mkataba mnono kwingineko kwa kiwango ambacho ataonyesha Mtibwa.

Kama vile haitoshi hii itakuwa fursa nyingine kwa Ndemla kurudi katika kikosi cha timu ya taifa. Akicheza mara kwa mara atakaa vema katika jicho la Kim Poulsen. Aina ya mpira ambao Ndemla anacheza ni ule ambao unatakiwa na Kim Poulsen. Sitashangaa akirudi Stars kwa kishindo.

Kila la kheri kwake. Wachezaji wengine pia wasihofie kuchukua uamuzi mgumu wa kuondoka Simba na Yanga kwa ajili ya kuimarika kwingineko. Kitu cha msingi ni kujiamini na kujiwekea malengo. Maisha ya soka ni mafupi kuliko ambavyo wachezaji wanafikiria.