Motisha kwa wachezaji husaidia saikolojia ya mafanikio ya klabu

Muktasari:
- Lakini, Jumapili, Pyramids ya Misri anayoichezea aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini mabao 2-1.
USIKU wa Jumamosi iliyopita, PSG ya Ufaransa ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada kuifunga Inter Milan ya Italia kipigo cha aibu cha mabao 5-1 jijini Munich, Ujerumani.
Lakini, Jumapili, Pyramids ya Misri anayoichezea aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifunga Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini mabao 2-1.
Vilevile hapa nyumbani, Jumamosi iliyopita, Singida Black Stars iliiondosha Simba katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya nusu fainali. Hayo yalikuwa ni mafanikio makubwa kuifunga timu iliyofika fainali Kombe la Shirikisho Afrika 2025.
Hivi sasa ligi nyingi duniani zinazofuatiliwa na wadau wa soka Tanzania zimemalizika ikiwamo EPL na La liga. Imebaki Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.
Mechi zote hizo zinatupa picha kuwa mafanikio ya timu yalivyochangiwa na uwepo wa motisha ya hali ya juu katika klabu. Ni ukweli kuwa lengo kuu la kila timu ni kuwa bingwa, ila motisha ni msingi wa kufanikiwa.
Katika saikolojia, motisha hurejelea hali ya ndani au seti ya mambo ya nje ambayo huchochea tabia ya mtu kufikia lengo mahsusi.
Malengo binafsi ya mchezaji ni kuwa bora kila siku na kusaidia timu kufikia malengo iliyojiwekea.
Kiuhalisia motisha na utendaji vinategemeana kwani motisha huendesha juhudi na mwelekeo ili kufikia malengo, wakati utendaji ni matokeo ya juhudi hizo. Motisha inaweza kuathiriwa na mambo ya ndani kama vile malengo binafsi na mambo ya nje kama vile zawadi au utamaduni. Mambo hayo ni muhimu kwa mchezaji na viongozi wa klabu kuyaelewa ili kuboresha viwango vya mchezaji.
Mafanikio ya timu kubwa za soka duniani yanabebwa na motisha kwa wachezaji. Wachezaji wenye motisha ya chini ni vigumu kuleta matokeo makubwa uwanjani.
Uwekezaji uliofanywa na PSG na Pyramids ni mfano mzuri wa kufanikiwa katika soka kwa kutumia nyenzo ya motisha kwa wachezaji.
Wawekezaji huweka bonasi mezani, huwaeleza mapema wachezaji kuwa lengo kuu ni kubeba kombe fulani. Hatua ya robo fainali bonasi italipwa kiasi fulani na ubingwa bonasi kiasi hiki.
Lakini pia katika mikataba huelezwa kuwa mshahara utapanda endapo timu itafika hatua fulani. Hii ndio inajulikana kama motisha ya nje. Inampa msukumo mchezaji kujituma ili kutimiza malengo. Vilevile wachezaji wamewekewa sheria kali na adhabu za faini endapo watazembea na kuharibu malengo ya klabu. Mfano wanakatwa mshahara kwa kuchelewa kujiunga kambini au mazoezini.
Motisha ni muhimu katika soka ili kuendesha utendaji wa mtu binafsi na wa timu, kudumisha uwiano na kukuza ukuzaji wa ujuzi wa mchezaji.
Vilevile motisha inakuza kujitolea na ufuatiliaji kwa makini malengo ya timu na hatimaye kuchangia mafanikio ya mchezaji binafsi na timu.
Motisha ni mchakato unaoanzisha, kuongoza na kudumisha tabia zinazolenga kufikia lengo au kukidhi hitaji fulani. Inamfanya mchezaji atende na kuishi kwa njia sahihi. Ni nguvu ambayo inamfanya kuwajibika bila kusukumwa na kutekeleza maelekezo kwa uwezo wa juu.
Kunywa maji wakati una kiu, kufanya mazoezi ya kuongeza nguvu ya misuli au kusoma vitabu vya mbinu za uchezaji ili kuboresha uchezaji. Vitendo hivyo vinachochewa na motisha.
Jicho la kitabibu upande wa saikolojia, mambo yafuatayo yanatupa picha ya umuhimu wa motisha katika soka ili kufanikiwa:
1. Utendaji wa kiwango kwa mchezaji
Kuongeza bidii na kujitolea, motisha humshurutisha mchezaji kufanya kazi kwa bidii zaidi katika mazoezi na mechi pamoja na kujitahidi kujitolea katika nyakati ngumu hata kama amechoka.
2. Ukuzaji wa ujuzi ulioimarishwa
Wachezaji walio na motisha na ari wana uwezekano mkubwa wa kufanya mazoezi mara kwa mara na kujitolea wakati wa kuboresha ujuzi katika mazoezi ya benchi la ufundi.
3. Ustahimilivu na uvumilivu
Motisha husaidia wachezaji kushinda changamoto na vikwazo, kudumisha umakini na azimio la timu hata wanapokabiliwa na hali ngumu. Huonyesha kudumu kucheza kwa kiwango cha muda mrefu.
4. Kujithamini na kujiamini
Motisha chanya hukuza kujiamini na imani katika uwezo wa mchezaji na kuathiri vyema utendaji na mtazamo wake.
5. Kuweka malengo na mafanikio
Motisha huwasukuma wachezaji kuweka malengo kwa uwazi na kuyafuata kwa dhamira ya dhati na kuchangia ukuaji wao na wa timu kwa ujumla.
6. Utendaji wa timu
Uwiano ulioimarishwa na uchezaji kitimu kwa pamoja na kuhamasishwa kunakuza hali ya umoja na madhumuni ya pamoja ndani ya timu.
Vilevile husababisha mawasiliano bora baina yao, ushirikiano na utendakazi mzuri kwa timu nzima.
7. Mazingira chanya ya timu
Timu yenye motisha bora ina uwezekano mkubwa wa kuwa na mazingira ya kuunga mkono lengo kuu, kufurahisha na kukuza hali ya mahusiano baina ya wachezaji na viongozi.
8. Uamuzi sahihi wakati wa kucheza
Wachezaji wenye motisha na ari wana uwezekano mkubwa wa kufanya uamuzi sahihi uwanjani, jambo linalochangia mafanikio ya timu hasa katika mechi ngumu zenye upinzani.
9. Mafanikio ya pamoja
Motisha ya mchezaji binafsi hutafsiri kuwa mafanikio ya timu ni yake pia. Timu iliyohamasishwa kwa motisha ina uwezekano mkubwa wa kufikia malengo na kushinda vizuizi vyote.
10. Ustawi wa kisaikolojia
Kuhamasishwa kwa motisha huchangia afya bora ya akili na hisia chanya, hivyo kuleta ustawi wa wachezaji na kusababisha kuwa na utulivu wa kiakili hatimaye kuwa makini katika uchezaji.
11. Nje ya Uwanja
Kuleta shauku na furaha katika klabu na mashabiki ambao ndio huwapa motisha kwa kuwahamasisha wakati wakicheza uwanjani. Maisha ya mchezaji nje ya majukumu ya uwanja huwa ni ya furaha anapokutana mtaani na mashabiki.
12. Ukuaji binafsi
Safari ya mchezaji aliyehamasishwa kwa motisha sio tu kushinda, lakini pia juu ya ukuaji binafsi, kujitambua na ukuzaji wa tabia na mienendo bora ya kimaisha.
13. Mafanikio ya muda mrefu
Kuhamasishwa ni kipengele muhimu katika mafanikio ya muda mrefu katika mchezo wa soka, kwani kunakuza kujitolea zaidi, kuleta maendeleo endelevu na kujitolea kikamilifu.
CHUKUA HII
Kutoa motisha ya nje ni kazi ya makocha, viongozi, wafanyakazi wa benchi la ufundi na timu nzima ya wataalamu inayomzunguka mchezaji. Vilevile ni jukumu la mchezaji mwenyewe kujipa motisha ya ndani.
Mchezaji aliyepewa motisha ni pamoja na kuzingatiwa maslahi yaliyopo katika mkataba, uhuru wa kutoa maoni huku pia akisikilizwa na kuheshimiwa.