MBIO ZA NJIWA; Unalipa kiingilio ndiyo utazame burudani
Muktasari:
- Katika sehemu mbalimbali duniani, njiwa wanatumika katika mchezo maalum wa mashindano ya mbio za njiwa na watu hulipa viingilio kwa ajili ya kutazama.
LONDON, ENGLAND: WAKATI baadhi ya jamii wakimwona ndege aina ya Njiwa kama kitoweo, wengine mapambo, sehemu nyingine mambo ni tofauti.
Baadhi ya watu wanamwona kama nyenzo ya burudani na wanawatumia kwa mashindano.
Katika sehemu mbalimbali duniani, njiwa wanatumika katika mchezo maalum wa mashindano ya mbio za njiwa na watu hulipa viingilio kwa ajili ya kutazama.
Leo tumekusogezea undani wa mchezo huu namna unavyochezwa, kanuni na jinsi njiwa wanavyofundisha hadi kufikia kuwa tayari kwa ajili ya mashindano.
HISTORIA.
Mashindano haya ya njiwa yana historia ndefu sana, yanadaiwa kuanzia karne ya 02 kabla ya kristo.
Tangu wakati huo yamedumu hadi leo. Pia kuna ushahidi wa kuwa katika karne ya 12, mfumo wa mawasiliano kwa kutumia njiwa ulianzishwa huko Baghdad.
Mchezo huu ulipata umaarufu zaidi karne ya 19 na Ubelgiji ndiyo ulikuwa ukichezwa sana kabla ya kuenea maeneo mbalimbali duniani.
AINA YA NJIWA
Mashindano haya hufanywa na aina maalum ya njiwa wanaojulikana kama Racing Homer.
Njiwa hawa wanatajwa kuwa ndio wenye kasi kubwa zaidi duniani na mafunzo huanza wakiwa wadogo, hujifunza katika mazingira ya karibu na nyumbani, kisha hupelekwa mbali hatua kwa hatua ili kuimarisha uwezo wao wa kurudi na kukumbuka njia wakati wa mashindano.
Kwa kawaida, njiwa hushiriki mashindano kuanzia umbali wa takriban kilomita 100 hadi zaidi ya kilomita 1,000. Katika baadhi ya mashindano, njiwa hawa hufikia kasi ya zaidi ya kilomita 60 kwa saa ikiwa hali ya hewa imetulia.
MAFUNZO
Kwanza kabisa njiwa huishi katika sehemu maalum inayoitwa loft na mafunzo wanayopewa huwa ni kufanya mazoezi ya kuruka hatua kwa hatua.
Kusafirishwa mbali na kuruhusiwa kurudi, njiwa dume kuwekwa mbali na mwenza wake hivyo, atatamani kurudi kwa ajili ya kumfuata.
KANUNI
Usajili wa Njiwa
Kila njiwa lazima awe amesajiliwa rasmi na kubeba pete ya utambulisho (leg band) yenye namba ya kipekee inayowekwa akiwa na umri mdogo (takriban siku 5).
Mafunzo na Utunzaji
Njiwa lazima wafundishwe na kutunzwa vizuri kabla ya mashindano.
Wafugaji wanapaswa kuhakikisha njiwa wako katika hali nzuri ya afya kabla ya kushiriki mashindano yoyote yale.
Umbali wa Mashindano
Mashindano hufanyika kwa umbali uliopimwa kwa usahihi (kwa kawaida kati ya kilomita 100 hadi 1,000 au zaidi).
Muda wa Kurudi
Muda wa njiwa kurudi nyumbani hupimwa kuanzia wakati wa kuachiliwa hadi kufika kwenye eneo la mwisho. Njiwa anayerejea kwa muda mfupi zaidi ndiye mshindi.
Njia ya Kupima Muda
Kuna njia mbili:
Njia ya kizamani ilikuwa ni kutumia pete za mpira ambazo huwa na saa maalum, lakini sasa unatumika mfumo wa RFID au vifaa vya elektroniki vinavyosoma muda kiotomatiki.
Masharti ya Uanachama
Washiriki lazima wawe wanachama wa klabu au chama cha mbio za njiwa, pia wanapaswa kufuata sheria za chama husika.
Ni marufuku kutumia dawa za kuongeza nguvu kwa njiwa (doping).
Njiwa wanaweza kufanyiwa vipimo kuhakikisha hakuna matumizi ya dawa hizo.
ZAWADI
Zawadi hutolewa kwa mmiliki wa njiwa na huwa ni pesa takribani Dola 20,000 na wakati mwingine hufikia Dola 50000. Pia huwa kuna vikombe na vyeti.