Prime
Maswali tata zawadi za Yanga Kombe la FA

Muktasari:
- Mvutano huo unahusu madai ya Yanga kwa TFF juu ya zawadi zao za ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) za misimu mitatu ambayo timu hiyo imetwaa ubingwa huo mfululuzo.
UKIPITA mitaani kuanzia vijiwe vya kahawa, maskani za bodaboda, na hata katika daladala hadi mitandaoni, mjadala mkubwa ni mvutano uliopo baina ya Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na Klabu ya Yanga.
Mvutano huo unahusu madai ya Yanga kwa TFF juu ya zawadi zao za ubingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) za misimu mitatu ambayo timu hiyo imetwaa ubingwa huo mfululuzo.
ISHU ILIPOANZIA
Hadi kufikia katika mvutano huo, ilianzia katika mechi ya Dabi ya Kariakoo ambapo Yanga imeendelea kusisitiza haitacheza Juni 15 mwaka huu dhidi ya Simba hadi Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) itakapotimiza matakwa yao manne ambayo kwanza Kamati ya Usimamizi wa Ligi ivunjwe.
Pili inataka Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao ajiuzulu, tatu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi, Almasi Kasongo kuachia ngazi na nne ambalo ni la mwisho ni kutaka kuona Bodi inakuwa huru.
Sakata la mchezo huo wa dabi lilianza baada ya Machi 8 mwaka huu kuahirishwa na kupangiwa kuchezwa Juni 15, huku Yanga ikisema kanuni hazikufuatwa wakati wa kuahirishwa kwake.
Kasongo alikiri kupokea mambo hayo manne kutoka Yanga na kusema watakwenda kuyafanyia kazi, akini akasisitiza bado mchezo huo namba 184 uliopangwa kupigwa Juni 15 upo pale pale kama ambavyo ulitangazwa hadi itakapotangazwa tofauti.
“Katika haya mambo manne ni jambo moja ambalo lipo kwenye mamlaka ya Mwenyekiti wa Bodi ambalo ni muundo wa Kamati ya Usimamizi wa Ligi, lakini haya mengine yanahitaji muda na kuamuliwa kwenye vyombo vingine tofauti.
“Haya yanahitaji muda kuweza kupata muafaka wake hayawezi kufanyika kwa haraka hata kama ukitaka kuyafanyia kazi kwa hiyo kwa mamlaka yangu au wa nafasi yangu naweza kusema ratiba inabaki vilevile kama ambavyo ilipangwa mpaka hapo itakapoamuliwa vingine,” alisema Kasongo muda mfupi baada ya kukutana na viongozi wa Yanga, Jumatatu wiki hii.
Jioni ya Jumatatu baada ya Kasongo kuyasema hayo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliibuka na tuhuma mpya juu ya fedha za ubingwa wa Kombe la FA.
Kamwe alisema endapo Yanga haitapewa majibu sahihi juu ya fedha za ubingwa wa Kombe la FA walilotwaa msimu uliopita hawatacheza fainali ya msimu huu dhidi ya Singida Black Stars iliyopangwa kufanyika Juni 28 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Baada ya hilo, TFF ilitoa taarifa kwa Umma ikiwataka wataalamu wa fedha wa Yanga Jumatano ya Juni 11, 2025 saa 4:00 asubuhi kufika makao makuu ya shirikisho hilo, kujadiliana kwa kina juu ya sakata hilo ili kufikia uamuzi wa mwisho kwani Yanga haidai bali inadaiwa, jambo ambalo viongozi wa Yanga walitii, lakini ikawa tofauti.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika ofisi za TFF, alisema; “Wewe umeona wapi hela ya zawadi ikakatwa kwenye madeni? Sisi kwa upande wa Yanga hatutaki kujadiliana jambo lolote kwa sasa zaidi ya kudai haki yetu ya msingi ambayo ni fedha za ubingwa.”
Kwa upande wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, alisema Yanga hawakutaka kuzungumza chochote katika kikao walichoitiwa, zaidi ya kuleta barua kisha kuondoka.
Akizungumzia bingwa wa Kombe la FA anachukua kiasi gani, Ndimbo alisema hakuna sehemu yoyote iliyotangazwa kiasi cha fedha kuongezeka kama Yanga inavyodai, akimaanisha imeendelea kubaki Sh50 milioni.
Katika taarifa kwa Umma iliyotolewa na Yanga Juni 10, 2025, ilidai TFF imeshikilia fedha zote za ubingwa wa michuano hiyo iliyotwaa kwa misimu mitatu, 2021-2022 (Sh50 milioni), 2022-2023 (Sh50 milioni) na 2023-2024 (Sh200 milioni), jambo ambalo ni kinyume na taratibu.
CHA KUJIULIZA
Wakati kukiwa na mvutano wa fedha za zawadi kwa mshindi, Aprili 2, 2024 siku ambayo TFF iliingia makubaliano ya mdhamini wa michuano hiyo, ilielezwa ni mkataba wa miaka mitatu na nusu wenye thamani ya Sh3.76 bilioni.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema benki hiyo itatoa Dola 100,000 za Marekani(takriban Sh255 milioni) kwa TFF kwa lengo la kufanikisha mechi zilizobaki za msimu huo 2023-2024 ambapo ilikuwa hatua ya robo fainali. Pia itatoa Sh800 milioni kwa msimu wa 2024-2025 na baadaye Sh1 bilioni kwa msimu wa 2025-2026 na kumalizia Sh1.2 bilioni msimu wa 2026-2027.
“Fedha hizi tutakazozitoa zinajumuisha zawadi ya mshindi wa michuano yaani timu bingwa, mchezaji bora wa kila mechi na mchezaji bora wa mzunguko, goli bora la mechi na goli bora la msimu pamoja na timu bora ya msimu,” alinukuliwa Nsekela.
Ukiweka kando michuano hiyo, katika Ligi Kuu Bara zawadi zake zinazotolewa na mdhamini mkuu sambamba na wenye haki za matangazo, zipo wazi.
Kwa upande wa mdhamini mkuu NBC, zawadi za bingwa anaondoka na kiasi cha Sh100 milioni, lakini mwenye haki za matangazo, Azam Media anatoa bonasi ya Sh500 milioni na kumfanya bingwa kukunja jumla ya Sh600 milioni.
Mbali na bingwa, pia kuna fedha zingine za bonasi timu zinapewa kutoka kwa mwenye haki za matangazo kwa kila nafasi na kufanya timu zote 16 shiriki kuambulia mgao.
UTATA ULIPO PIA
Kwa msimu huu, hadi michuano hiyo inafika hatua ya fainali, tumeshuhudia zawadi ya mchezaji bora wa mechi ikitolewa, huku ile ya mchezaji bora wa mzunguko na bao bora la mechi haikuwahi kutolewa.
Wakati hali ikiwa hivyo, upande wa zawadi za mchezaji bora wa mechi, imekuwa ikitolewa huku ikidhibitishwa na uongozi wa Singida Black Stars kupitia kiungo wa timu hiyo, Emmanuel Keyekeh baada ya kuibuka mchezaji bora wa mchezo wa nusu fainali dhidi ya Simba.
KLABU ZASHTUKA
Mwanaspoti limezungumza na baadhi ya viongozi wa klabu zinazoshiriki michuano hiyo kutaka kutambua ufahamu wao wa zawadi upoje ambapo walisema madai ya Yanga yamewafungua akili, hata hivyo, bado wameendelea kusisitiza kwamba wanafahamu zawadi za mshindi ni Sh50 milioni.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam FC, Thabiti Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema: “Hili lililoibuliwa linapaswa kutuamsha klabu nyingine kuanza kuulizia juu ya zawadi halisi za washindi na mambo yawekwe hadharani kwani ni fursa kwa klabu kujua kwa sababu tangu michuano iliporejea ikiwa kama ASFC, zawadi ilikuwa ni Sh 50 milioni tu.”
Ofisa Habari wa Singida Black Stars iliyotinga fainali ya michuano hiyo msimu huu, Hussein Massanza alisema hawajapata mabadiliko yoyote juu ya ulipwaji wa fedha za bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho na sasa wapo katika mchakato wa kufuatilia kabla ya kuvaana na Yanga Juni 28.
“Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu ameanza mchakato wa kufuatilia endapo tutatwaa ubingwa tutapata kiasi gani kwa sasa lakini miaka yote tunafahamu ni Sh50 milion, hatuna mabadiliko yoyote tuliyoyapata,” alisema Masanza.
Mtendaji Mkuu wa Coastal Union, Omar Ayoub alisema hawana mabadiliko yoyote kuhusiana na fedha anayopokea bingwa wa mashindano husika.
“Tulicheza hatua ya fainali kiasi kinachotambulika miaka yote ndio tulichokuwa tunakifahamu kwa sasa sijui bingwa anachukua bei gani kama kuna mabadiliko sisi hatuna taarifa hiyo.”
Hata hivyo, aliweka bayana kwamba kwa utaratibu wa michuano hiyo kila hatua inayoshiriki timu kuna fedha wanapewa kwa ajili ya mechi husika, japo kwa zawadi halisi ya bingwa haijawahi kujulikana tangu mdhamini mpya alipoingia.
WACHUMI
Akizungumza na Mwanaspoti, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi na Kifedha, Aziz Rashid alisema utaratibu wa taasisi kukata fedha zinazopitia kwao kwenda kwa taasisi nyingine unatakiwa kuwa kwenye makubaliano.
Mtaalamu huyo ameyasema hayo kufuatia TFF kusema Yanga iliomba kwa barua fedha zao za zawadi katika mashindano mbalimbali zikatwe kulipia malipo wanayotakiwa kulipa kwa TFF ikiwemo ada za wachezaji.
“Suala la malipo kuna taratibu zake ambazo ni kuanzisha malipo, kuthibitisha na kuidhinisha ambapo itaonesha nani analipa, anayelipwa na kiasi husika,” alisema mtaalamu huyo na kuongeza.
“Kama kuna mtu anadaiwa, itaangaliwa kanuni au miongozo ya taasisi husika, lakini kama kuna makubaliano maalum, basi inaweza kufanyika kwamba linakatwa deni, kilichobaki kinakwenda kwa muhisika.
“Kwa levo za kitaasisi, lazima nyaraka ziwekwe wazi kuonyesha hayo malipo ya deni yalivyofanyika, haiwezi kuwa kwa kauli za mdomo tu kama mimi na wewe tunavyoongea.”
Kupitia hilo, TFF imeeleza yenyewe ndiyo inaidai Yanga kutokana na makubaliano yao ya kukata fedha za zawadi, lakini Yanga kupitia taarifa yao ya Juni 10, 2025, ilisema hakuna uthibitisho wowote wa kimaandishi kuonyesha kama TFF imewahi kulipa fedha hizo za ubingwa kwa klabu hiyo.
Mwanaspoti lilimtafuta Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi ili kuzungumzia suala hilo, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya kigogo huyo kutopokea simu na kushindwa kuonyesha ushirikiano.
Baada ya hapo, Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Ndimbo, alipopigiwa simu aliipokea lakini alipoulizwa tu swali linalohusu zawadi za fedha za mashindano hayo, hakutoa ushirikiano.
MASWALI 10 TATA
1-Kwanini TFF imekuwa ikifanya siri kubwa zawadi za washindi hadi klabu na wadau wa soka kutofahamu?
2-Klabu zinashiriki vipi mashindano bila ya kufahamu bingwa anapata zawadi kiasi gani cha fedha?
3-Viongozi wa Klabu za soka Tanzania wanaelewa umuhimu na uzito wa nafasi zao, wako kwa masilahi yao binafsi au kuwafurahisha mashabiki?
4- Ushikaji na kuendesha mambo kwa mazoea baina ya TFF na klabu nchini una masilahi kwa soka la Tanzania?
5-Kwanini TFF inakaa na zawadi za washindi kwa muda mrefu, ilihali mdhamini ameshatoa fedha? Na inajua hali ya kiuchumi ya klabu zake?
6-Kama zawadi ya fedha ni Sh50 milioni, Yanga imetoa wapi hizo Sh200 milioni inazoidai TFF? Na Je? Kama mdhamini anatoa Sh255milioni kama gharama za jumla iweje bingwa apewe Sh50milioni?
7-Licha ya mdhamini kubadilika, kwa nini zawadi wa michuano hiyo ya Shirikisho hazijabadiliki? Na kwanini wahusika hawakugawiwa vielelezo?
8-Zawadi ya bao bora la kila raundi ya mashindano zimekwenda wapi? Na kwanini klabu hazihoji kwenye vikao rasmi?
9-Zawadi ya bao bora la kila mechi zimekwenda wapi?
10-Zawadi ya mchezaji bora wa kila raundi ya mashindano imekwenda wapi na klabu zilielezwa kwanini ilitolewa?