Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Masupastaa 30 wa kutazamwa Kombe la Dunia la Klabu

MASTAA Pict

Muktasari:

  • Kuna tofauti ya saa saba kati ya muda wa Miami na Dar es Salaam, hivyo mechi hiyo itaanza saa 9:00 alfajiri ya Jumapili kwa Afrika Mashariki.

NEW YORK MAREKANI: KIPYENGA cha fainali za Kombe la Dunia la Klabu 2025 kinapulizwa na Inter Miami ya Marekani itakata utepe na Al Ahly ya Misri uwanjani Hard Rock huko Miami, Florida, Jumamosi huko Marekani na kwa Afrika Mashariki, mechi hiyo itafanyika Alfajiri ya Jumapili.

Kuna tofauti ya saa saba kati ya muda wa Miami na Dar es Salaam, hivyo mechi hiyo itaanza saa 9:00 alfajiri ya Jumapili kwa Afrika Mashariki.

Wakati mashabiki wakisubiri kwa hamu kubwa fainali hizo za Fifa, hii hapa orodha ya mastaa wanaotarajiwa kwenda kuongeza mvuto mkubwa kwenye michuano hiyo kung’ara na klabu zao.


MAST 01

30. Stephane Aziz Ki (Wydad)

Baada ya kutamba kwa miaka kadhaa katika soka la Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na kikosi cha Yanga, staa wa Burkina Faso, Stephane Aziz Ki alipata dili la kunaswa na Wydad ya ligi ya Botola, huku usajili wake ukifanywa kwa haraka ili kwenda kucheza fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.


29. Estevao (Palmeiras)

Staa matata kwenye soka la Brazil, Estevao ni kivutio Palmeiras kutokana na kiwango chake cha uwanjani, akifunga mabao 13 na asisti tisa, timu yake ikimaliza nafasi ya pili kwenye Serie A ya Brazil. Winga huyo, 18 ni fundi anayetumia mguu wa kushoto na atajiunga na Chelsea kwa kwa ada ya Dola 75 milioni.


28. Salomon Rondon (Pachuca)

Staa wa Venezuela, Rondon walikuwa kinara wa mabao wa Pachuca ya Mexico kwenye ligi ya Liga MX Clasura 2024-25, alipofunga mabao 10 na asisti tatu. Straika huyo ni veterani, ana umri wa miaka 35 na aliwahi kukipiga West Brom. Uzoefu wake wa kucheza michuano mingine ndicho kinachowavutia wengi kumwona.


27. Miguel Borja (River Plate)

Mshambiliaji Mcolombia, Borja ataongoza River Plate, huku akiwa na rekodi ya kufunga mabao 11 kwenye ligi ya Liga Profesional 2024 huko Argentina. Staa huyo mwenye umri wa miaka 32, amecheza zaidi ya mechi 100 katika timu hiyo na kufunga mabao 60. Alishinda pia ubingwa wa Primera Division na River Plate 2023.

MAST 02

26. Jhon Arias (Fluminense)

Staa mwingine Mcolombia atakayekuwapo kwenye fainali hizo, ambaye atakipiga katika kikosi cha Fluminense. Winga, Arias, 27. Alifunga mabao 14 katika mechi 51 za michuano yote aliyocheza klabu hiyo ya Brazil, lakini kwa mwaka 2024, timu yake ilimaliza nafasi ya 13 kwenye ligi yenye timu 20. Kiwango chake binafsi ni bora.


25. Rodrigo De Paul (Atletico Madrid)

Kama kuna wachezaji wanaopambana kwa ajili ya nembo ya klabu zao, basi mmoja wao ni De Paul. Kiungo huyo Muargentika amekuwa matata kwa mapambano ya ndani ya uwanja iwe kwa klabu yake au timu ya taifa.

Hajawahi kushindwa vita kirahisi na hilo ndilo linalowafanya wengi kusubiri kumwona akifanya mambo yake.


24. Enzo Fernandez (Chelsea)

Fernandez alijitengenezea umaarufu kwenye Kombe la Dunia 2022 alipokuwa na kikosi cha Argentina na kufanikiwa kubeba ubingwa kipindi hicho akiwa Benfica kabla ya kunaswa na Chelsea. Sasa atakwenda kwenye Kombe la Dunia la Klabu kuonyesha makali yake ili The Blues ibebe ubingwa huo.


23. Khvicha Kvaratskhelia (PSG)

Anaitwa Kvaradona kwa sababu mbili, kwanza hakuna mtu anayependa kulitamka kwa usahihi jina lake na  pili ni staili ya uchezaji wake kile ambacho miguu yake inafanya kinalinganishwa na gwiji wa Argentina, Diego Maradona. Staa huyo amefunga mabao 12 na asisti tisa, hvyo atakuwapo Marekani akiwa na kikosi cha PSG.

MAST 03

22. Lautaro Martinez (Inter Milan)

Straika Lautaro Martinez amekuwa hana moto sana anapokuwa kwenye soka la kimataifa kuitumikia Argentina, lakini bila ya shaka ni matata anapokuwa na klabu yake ya Inter Milan. Aliisaidia timu yake kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita, akifunga mabao 22 na asisti saba michuano yote.


21. Gianluigi Donnarumma (PSG)

Moja ya mastaa wanaotarajiwa kwenda kuwa kivutio kikubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu ni kipa wa Paris Saint-Germain, Donnarumma. Ubora wake wa uwanjani ndicho kitu kinachovutia wengi kutaka kuona kama atakwenda kukifanya alichokifanya PSG na kuwapa taji la Mabingwa Ulaya msimu 2024-25.


20. Federico Valverde (Real Madrid)

Mpiga kazi matata wa Real Madrid, Valverde ni moja ya viungo wachache wanaocheza goli hadi goli waliopo kwenye soka la dunia kwa sasa. Ana uwezo pia wa kucheza beki wa kulia na hicho ndicho kinachofanya kuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki wanaomtarajia afanye kweli kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu.


19. Thibaut Courtois (Real Madrid)

Linapotajwa jina la Courtois, ni wachache sana wanaohitaji maelezo yake kutokana na kipa huyo wa kiwango cha dunia kuonyesha makali makubwa uwanjani. Real Madrid imekuwa kwenye mikono salama Mbelgiji huyo anapokuwa golini na hilo linatazamiwa kwenda kuonekana kwenye fainali hizo za dunia huko Marekani.

MAST 04

18. Antoine Griezmann (Atletico Madrid)

Griezmann, ni bingwa wa Kombe la Dunia 2018 alipokuwa kwenye kikosi cha Ufaransa na bila shaka amekuwa mmoja wa wachezaji mashabiki wanawasubiri kwa hamu huko Marekani. Uwezo wake wa kutumbukiza mipira nyavuni ndicho kitu kinachomfanya Griezmann awe kivutio, huku Atletico ikitegemea ubora wake uwanjani.


17. Alessandro Bastoni (Inter Milan)

Moja ya mabeki wanaochipukia kwa kasi kabisa kwenye soka la dunia kwa sasa ni mkali, Bastoni, ambaye ameisaidia Inter Milan kucheza fainali mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya miaka mitatu. Staa huyo mwenye umri wa miaka 26 ni mzoefu, akishinda Serie A, Coppa Italia na Supercoppa Italiana akiwa Inter.


16. Ruben Dias (Man City)

Beki matata kabisa, Dias alikuwa sehemu ya kikosi cha Manchester City kilichobeba Kombe la Dunia 2023. Lakini, fainali hizo ni tofauti na beki huyo wa kati wa Urenao, Dias amebeba matumaini makubwa kwa kikosi hicho cha Kocha Pep Guardiola ili kufanya vizuri kwenye fainali hizo za klabu za kusaka ubingwa wa dunia.


15. Julian Alvarez (Atletico Madrid)

Alvarez, ni mshindi mwingine wa Kombe la Dunia 2022 alipokuwa na kikosi cha Argentina na mkali huyo atakwenda kwenye Kombe la Dunia la Klabu akiwa na kikosi cha Atletico Madrid. Tangu alipojiunga na miamba hiyo ya La Liga akitokea Manchester City, Alvarez amejipambanua na kuwa straika wa kiwango cha dunia.

MAST 05

14. Jamal Musiala (Bayern Munich)

Musiala ni kipaji maridhawa kabisa kwenye soka kwa sasa tangu alipoibukia katika klabu ya Bayern Munich. Staa huyo ni fundi mkubwa kwenye miguu yake na ni moja ya washambuliaji wanaovutia kutazama kutokana na kuwa na akili mkubwa ya soka. Umri wake ni 22, lakini Musiala anacheza soka la kikubwa.


13. Lionel Messi (Inter Miami)

Supastaa, Lionel Messi amekuwa na maajabu yake anapocheza kwenye mechi kubwa na michuano mingine na pengine hilo ndilo linalomfanya mashabiki watarajie mengi kutoka kwake. Ni mshindi mara nane wa Ballon d’Or, alibeba Kombe la Dunia 2022 alipokuwa na kikosi cha Argentina. Safari hii yupo Inter Miami.


12. Desire Doue (PSG)

Kinda aliyekuwa kivutio kwenye soka la Ulaya kwa msimu wa 2024-25, Doue amekuwa moto ndani ya uwanja anapokuwa na kikosi chake cha Paris Saint-Germain. Kwa namna anavyocheza na staili yake aliyoibukia wengi wamekuwa wakimlinganisha na Neymar na Thierry Henry. Alistaa staa wa mechi ya fainali Mabingwa Ulaya.


11. Vitinha (PSG)

Vitinha ni bonge la mchezaji. Kiungo huyo wa mpira ni mkali wa timu ya taifa ya Ureno na amekuwa akili ya soka kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain huku staili yake ya uchezaji ikitazamiwa kwenda kuwa kivutio kikubwa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani. Fundi wa mpira.

MAST 06

10. Moises Caicedo (Chelsea)

Kiungo Caicedo amejitengenezea umaarufu mkubwa wa kuwa mnyang’anyaji hodari wa mipira kutoka kwenye miguu ya wapinzani ndani ya uwanja. Chelsea ililipa Dola 146 milioni kunasa saini yake kutoka Brighton. Uimara wa Chelsea kwenye eneo la kiungo unatokana na uhodari wake na hilo ndilo linalofanya asubiriwe kwa hamu.


9. Harry Kane (Bayern Munich)

Straika, Harry Kane hatimaye alimaliza gundu la kunyakua mataji msimu uliopita alipobeba Bundesliga akiwa na kikosi cha Bayern Munich. Hivyo, atakwenda Marekani kusaka taji lake la pili mwaka huu, wakati atakapokiongoza kikosi hicho kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu chini ya Vincent Kompany.


8. Nuno Mendes (PSG)

Beki wa kushoto wa Paris Saint-Germain, Nuno Mendes amekuwa gumzo kwa siku za karibuni kutokana na ubora wake wa uwanjani. Hivi karibuni alimweka mfukoni staa wa Barcelona, Lamine Yamal katika fainali ya Uefa Nations League, huku akiwafunika mawinga matata pia kama Salah, Morgan Rogers na Bukayo Saka.


7. Cole Palmer (Chelsea)

Mwingereza staa wa kikosi cha Chelsea, Cole “Cold” Palmer, ametajwa kama mmoja wa mchezaji wa kutazamwa kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu zitakazofanyika huko Marekani. Chelsea imani yao kubwa ya kufanya vizuri kwenye fainali hizo ipo kwa kinda huyo aliyefunga mabao 15 na asisti 12.

MAST 07

6. Jude Bellingham (Real Madrid)

Kiungo Jude Bellingham anakwenda kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu akibeba matumaini makubwa ya kikosi cha Real Madrid. Kwa msimu uliopita, staa huyo alifunga mabao 14 na asisti 14 na hilo ndilo linamfanya awe kivutio kikubwa kwenye fainali hizo na pengine kuna kitu bora atakwenda kukifanya.


5. Rodri (Man City)

Kiungo, Rodri alikosa karibu msimu mzima wa 2024-25 kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli ya goti iliyosababisha kufanyiwa upasuaji. Lakini, mkali huyo ndiye anayeshikilia tuzo ya Ballon d’Or na anatazamwa kama kuna kitu kikubwa atakwenda kuifanyia Man City kwenye fainali hizo za Marekani.


4. Vinicius Junior (Real Madrid)

Vini Jr ni dhahabu kwenye mchezo wa soka na Mbrazili huyo amebeba matumaini makubwa ya Real Madrid kwenda kufanya kweli kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani. Kinachovutia kwa Vini Jr ni jinsi anavyoweza kuufanya mpira ufanye kile ambacho yeye anataka ufanye. Ni kivutio cha mashabiki wengi.

MAST 08

3. Ousmane Dembele (PSG)

Kwenye hali isiyotarajiwa na wengi, Dembele ametajwa kuwa kinara kwa sasa kwenye mbio za kufukuzia tuzo ya Ballon d’Or 2025 kutokana na ubora wake alioonyesha kwenye kikosi cha PSG na alifunga mabao 33 na asisti 15, kwa maana ya kuchangia jumla ya mabao 48 katika mechi 49 alizocheza timu hiyo msimu huu.


2. Erling Haaland (Man City)

Kama kuna mwenye kuhitaji jina la straika mwenye uwezo mkubwa wa kutumbukiza mipira nyavuni basi staa wa Manchester City, Erling Haaland jina lake litabaki kuwa mbele. Staa huyo ni matata kwelikweli na ndiyo silaha ya Pep Guardiola kwenye fainali hizo akiamini atapata huduma bora hasa ya mabao ya ushindi.


  1. Kylian Mbappe (Real Madrid)

Kuna namna nyingi za kumwelezea staa wa Real Madrid, Mbappe kutokana na kile alichokifanya msimu uliopita akiwa na timu yake hiyo. Mbappe hakubeba ubingwa, lakini kiwango chake cha uwanjani kama mchezaji binafsi kilikuwa bora kabisa jambo linalomfanya awe kwenye orodha ya mastaa wanaosubiriwa kwa hamu Marekani.